TCRA washtukia biashara haramu ya simu Kanda ya Ziwa

0
723

BENJAMIN MASESE-MWANZA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema imebaini kuwapo na ongezeko la biashara holela ya vifaa vya mawasiliano katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku baadhi ya maduka yakijihusisha na uingizaji, usambazaji bila leseni na uuzaji wa simu za wizi na zisizo na ubora.

Pia imetangaza kuanza kuwakamata  watu binafsi na watumishi wa kampuni za mawasiliano nchini ambao wanatembea mitaani kusajili laini za simu huku wakijihusisha na uuzaji wa simu ambazo zinadaiwa kutokuwa na ubora kitendo kinachokwenda kinyume na sheria za TCRA inayoelekeza kudhibiti ubora ili kumlinda mtumiaji.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Mwanza na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo wakati akizungumza na maofisa biashara kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, askari polisi kitengo cha makosa ya mtandaoni, wawakilishi wa kampuni zote za simu na viongozi wa umoja wa mafundi simu.

Mihayo alisema TCRA imeshtushwa kwa namna ya maduka ya vifaa vya mawasiliano yanavyoanzishwa kiholela  huku simu za mikononi zikiuzwa kwa kutembezwa na nyingine kuwekwa mezani mfano wa nyanya au vitunguu sokoni.

“Swali la kujiuliza je, vifaa hivi vinapitia katika utaratibu gani kabla ya kumfikia mtumiaji? Je, vinapouzwa vinatakiwa kuuzwa kama bidhaa nyingine mfano wa  nyanya ama vitunguu sokoni? Je, vinapaswa kutembezwa na kuuzwa mkononi kama bidhaa nyingine? Jambo hili halikubaliki ndiyo maana hivi sasa watu wanalalamika simu zinakuwa za moto pale wanapoongea.

“Kuzagaa kwa vifaa vya mawasiliano kumesababishwa na maduka mengi kufanya biashara ya kuagiza, kusambaza na kuuza vifaa vya kielektroniki bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

“Tumebaini baadhi ya simu zinazoibwa na wezi huuzwa katika maduka yasiyokuwa na leseni, hivyo watu wengi bila kujua hujikuta wananunua simu za wizi, isitoshe maduka hayo yamekuwa kichocheo cha ongezeko la wizi wa simu.

 “Baadhi ya maduka ya simu yasiyokuwa na leseni yamekuwa yakiuza simu zilizotumika, yaani mitumba ambazo mara nyingi huwa za wizi au hazifai katika matumizi, huku zikiwa hazina muda wa uangalizi (guarantee) na huuzwa bila ya stakabadhi ya malipo.

“Jambo ambalo pia tumelibaini ni watumishi kutoka kampuni za mawasiliano nchini kwenda kusajili laini mitaani kwa njia ya vidole, lakini wanajihusisha na uuzwaji wa simu.

“Sasa TCRA tunasema ni marufuku kuuza simu mitaani na tutaanza kuwakamata muda wowote, pia wale wanaouza simu kwenye meza au wametengeneza mfano wa kabati mitaani nao wataingia mikononi, operesheni hiyo itaambatana na polisi,” alisema.

Mihayo alisema kutokana na kukithiri maduka hayo yasiyo na leseni, Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, James Kilaba ameelekeza viongozi wa kanda kukutana na maofisa biashara wote kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, polisi  Kitengo cha Makosa ya Mitandaoni, mafundi simu na wawakilishi wa kampuni za simu kuelimishana na kuweka mikakati ya kushirikiana kutokomeza jambo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here