Samatta kuanza kibarua na Watford

0
1198
Mbwana Samatta akiwa jijini Birmingham kwa ajili ya kujiunga na timu ya Aston Villa.

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

NAHODHA wa Timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta anatarajia kuanza kuichezea timu yake mpya ya Aston Villa, itakapoumana na Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England, utakaochezwa kesho kutwa  Uwanja wa Villa Park jijini Birmingham.

Samatta anasubiri kutangazwa kuwa mchezaji mpya wa Aston Villa wakati wowote, baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili, ikiwemo kufuzu vipimo vya afya alivyofanyiwa juzi.

Mshambuliaji huyo anatua Villa kwa dau la Pauni  milioni 8.5 (Sh Bilioni 25 za Tanzania), akitokea KRC Genk ya Ligi Daraja la Kwanza Ubelgiji, aliyoiwezesha kutwaa ubingwa msimu uliopita na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Taarifa kutoka Birmingham yaliko makazi ya Villa, zinadai  kuwa, Samatta  aliwasili jijini humo tangu Alhamisi iliyopita, ambapo Ijumaa alifanya mazoezi ya pamoja na kikosi hicho kabla ya kupimwa afya usiku.

Samatta atakuwa mchezaji watatu kujiunga na timu hiyo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili la Januari,  baada ya kutanguliwa na mlinda mlango wa zamani wa Liverpool, Pepe Reina aliyetua kwa mkopo akitokea AC Milan ya Italia.

Mchezaji mwingine aliyenaswa na Villa ni kiungo wa Chelsea, Danny Drinkwater aliyejiunga kwa mkopo.

Baada ya kutambulishwa rasmi, Samatta anatarajia kuanza kibarua chake katika mchezo ujao dhidi ya Watford, hiyo inatokana na kocha wa kikosi hicho kuhitaji mshambuliaji,  baada ya aliyekuwa akiiongoza safu hiyo, Wesley kupata majeraha.

Kocha wa Villa, Dean Smith aliushawishi uongozi wa klabu hiyo kufanya haraka kuinasa saini ya Samatta,  baada ya mpachika mabao wake huyo raia wa Brazil kuumia, hivyo kulazimika kucheza bila mshambuliaji halisi wakati mwingine.

Hakuna ubishi kuwa Samatta atapewa jukumu la kuongoza mashambulizi ya Villa, kutokana rekodi nzuri za upachjikaji mabao alizotokanazo Ubelgiji dhidi washambuliaji, Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’ na Anwar El Ghazi waliopo kwenye kikosi hicho

Samatta alimaliza nafasi ya pili kwenye chati ya wafungaji bora msimu uliopita kwa kupachika mabao 23, mabao mawili nyuma ya kinara,Hamdi Harbaoui wa Zulte Waregem aliyechukua kiatu cha ufungaji bora.

Tangu kuanza msimu huu, Samatta ameifungia Genk mabao 10, huku matatu akifunga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika michezo dhidi ya Liverpool na RB Salzburg ya Austria.

Hadi anaondoka Genk, Samatta amefanikiwa kuifungia ti mu hiyo mabao 76, pasi za mabao 20,  katika michezo 191 aliyoichezea timu hiyo tagua alipojiunga nayo Januari 29, mwaka 2016.

Mpachika mabao huyo wa zamani wa klabu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo(DRC) na Simba ya hapa nchini, amefanikisha uhamisho wa kukipiga Ligi Kuu England  na kuwa Mtanzania wa kwanza,  ikiwa ni muda mfupi tangu ajiunge na kampuni ya Spocs Consultant, ambayo pia inamsimamia nyota  wa Liverpool, Mohamed Salah,  katika masuala ya uhamisho.

Samatta amejiunga na kampuni hiyo akitokea First For Players iliyokuwa ikimsimamia awali, ikiwa ni mkakati ya kutimiza ndoto za kukipiga katika ligi hiyo pendwa zaidi duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here