28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta awavutia mawakala Ulaya

IMG_4679*Lowassa, Malinzi wammwagia pongezi

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

SASA ni wazi kuwa siku zinahesabika kwa mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta kuendelea kubaki kuichezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakati zikiwa zimesalia siku 53 dirisha dogo la usajili kufunguliwa barani Ulaya, juzi Samatta alimulikwa na mawakala wengi kutoka barani humo na hapa Afrika kwenye mchezo wa fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Ukiondoa bao alilofunga kwenye fainali hiyo na kumtengenezea lingine Roger Assale, Samatta pia alifunga bao katika fainali ya kwanza waliyoshinda mabao 2-1 ugenini, hivyo TP Mazembe imetwaa ubingwa kwa ushindi wa jumla wa 4-1.

Mbali na Samatta na Thomas Ulimwengu kuandika rekodi ya kuwa Watanzania wa kwanza kutwaa ubingwa huo na kufika fainali ya michuano hiyo, Samatta ameweka rekodi nyingine ya kuwa miongoni mwa wafungaji bora akilingana mabao na Bakri Al-Madina wa El Merreikh wote wakiwa wamefunga saba.

Samatta pia yumo kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania uchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ligi ya ndani, huku akitajwa kupewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake binafsi pamoja na klabu yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana Meneja wa straika huyo, Jamal Kisongo, alisema kuwa wanatarajia kupokea ofa nyingi kutoka Ulaya kwani mawakala wengi wanaotafuta wachezaji walikuwa uwanjani kumshuhudia Samatta pamoja na wachezaji wengine kwenye fainali hiyo.

“Vyombo mbalimbali vya Uingereza vimeripoti habari hiyo na kumwelezea Samatta hivyo tunatarajia kupokea ofa nyingi wiki hii kabla ya kuangalia mwelekeo wake ujao barani Ulaya pale mkataba wake utakapomalizika mwakani.

“Lakini tayari tumekubaliana na mmiliki wa TP Mazembe aondoke usajili wa dirisha dogo Januari mwakani japo anamaliza mkataba Aprili, hivyo hawezi kukataa kwani ameshakubaliana na hilo na Samatta ataondoka kama mchezaji huru lakini itakapotokea hali yoyote ya kuzuiwa Januari, tutaufidia mkataba wake wa miezi mitatu utakaokuwa umebakia kwa kuuvunja,” alisema.

Kisongo alizungumzia pia mafanikio aliyopata Samatta na kudai kuwa: “Hayakuja kama ajali, ni kijana mwenye nidhamu, anajitambua na anajua anafanya nini, hakutanguliza fedha mbele bali malengo, amekataa fedha nyingi sana za Zamalek ya Misri iliyokuwa ikimtaka, lakini ndoto yake ilikuwa ni kutaka kuingia kwenye soko Ulaya na sasa inakaribia kutimia.”

Aliongeza kuwa wanachosubiria kwa sasa ni Samatta kutangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kama hakutakuwa na siasa kwenye tuzo hiyo anayoiwania, huku akidai mshambuliaji huyo anatosha kabisa kupewa heshima hiyo kutokana na mafanikio aliyopata.

Lowassa, Malinzi, Lyon wasifu

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, naye amempongeza Samatta kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa miongoni mwa wafungaji bora barani Afrika kwa mabao yake saba sawa na Bakri Al-Madina.

Lowassa ambaye alifuatilia mchezo huo kwa njia ya runinga, alisema Samatta amedhihirisha kuwa wanasoka wa Tanzania wakiamua kujituma na kuwa wavumilivu wanaweza kufika mbali.

“Yule kijana na yule mwenzake (Thomas Ulimwengu) ni wavumilivu na wanajua nini wanatafuta hivyo watafika mbali sana, hii ni fahari kwa taifa letu, tunao uwezo wa kuwa na kina Samatta wengi zaidi kama tukiwekeza zaidi kwenye soka,” alisema.

Waziri Mkuu mstaafu huyo alisema ni muhimu sana kwa Serikali kuwekeza katika vyuo vya michezo.

“Moja ya sera za Chadema na Ukawa ni kuondoa ushuru katika vifaa vyote vya michezo pamoja na kuanzisha shule maalumu za soka (Youth Academy), ambazo zitasaidia kukuza vipaji na kuwatoa kina Samatta,” amesisitiza na kuongeza: “Serikali ya CCM isione aibu kuchukua sera hizo kwa manufaa ya michezo nchini.”

Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amewapongeza Samatta na Ulimwengu kutokana na klabu ya TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga USM Alger ya Algeria katika mchezo wa fainali juzi.

Amewataka washambuliaji hao waongeze juhudi ili waweze kufanya vizuri na kuisaidia timu yao katika michuano ya Kombe la Dunia la Mabara itakayofanyika mwezi ujao nchini Japan.

Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Watanzania wanaopenda soka, Malinzi aliwataka pia wajitume zaidi kwenye kikosi cha timu ya soka Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi dhidi ya Algeria utakaochezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Naye mmiliki wa timu ya African Lyon zamani Mbagala Market, Rahim Zamunda, ambako Samatta alianzia soka lake alisema: “Ni jambo la kujivunia kila Mtanzania kwa mafanikio waliyopata (Samatta na Ulimwengu), Samatta alikuwa ni mchezaji wetu na ameitangaza vilivyo klabu yetu kwa uwezo alionao na mafanikio waliyopata yatawasaidia vijana wengine kujifunza kutoka kwao,” alisema.

Zamunda alisema ili Tanzania ipate wachezaji wengine aina ya Samatta na Ulimwengu ni lazima uwekezaji mkubwa ufanyike kupata viongozi bora, uwekezaji wa soka la vijana na ligi bora.

“Lazima tupate viongozi bora watakaoongoza soka, vile vile lazima tuboreshe ligi yetu iwe bora katika mfumo utakaoendeshwa kibiashara na yote hayo yatapatikana kwa kuleta wataalamu na si mfumo tunaotumia kwa sasa,” alisema.

Samatta alianza kulipwa laki moja

Kabla ya Samatta kutua African Lyon zamani Mbagala Market 2008, alianzia kucheza soka la mchangani katika timu ya mtaani kwake ya Kimbangulile, iliyopo Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Usajili wake wa kwanza ulikuwa ni pale alipojiunga na timu ya African Lyon (zamani Mbagala Market) akiichezea katika Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kupanda Ligi Kuu ambapo inaelezwa alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 100,000.

Lakini hivi sasa tangu ajiunge na TP Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba, Samatta analipwa zaidi ya Dola za Marekani 10,000 (zaidi ya Sh milioni 22 za Kitanzania kwa mwezi).

Kwa mujibu wa mtandao transfermarkt.co.uk, umechambua thamani aliyonayo Samatta hivi sasa, ambayo inafikia euro 350,000 (zaidi ya milioni 900 za Kitanzania), lakini hivi karibuni aliwahi kutakiwa na timu ya Zamalek kwa dau linalofikia euro milioni moja (zaidi ya bilioni 2.3 za Kitanzania).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles