23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘SAMAKI WA KAPU MITAANI WANASABABISHA SARATANI’

CHRISTINA GAULUHANGA NA VERONICA ROMWALD -DAR ES SALAAM


 

samakiWATANZANIA wametahadharishwa kuwa makini na samaki wanaouzwa mitaani kwani wana madhara, ikiwamo ugonjwa wa saratani.

Imeelezwa wako wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wanauza samaki katika vikapu mitaani ambao wamevuliwa kwa njia haramu ya milipuko ya baruti inayosababisha saratani.

Meneja wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam, Eliakimu Mninko, alisema hayo jana ofisini kwake alipozungumza na MTANZANIA.

“Watanzania wawe makini kwani kuna wafanyabiashara ambao si waaminifu wanavua samaki kwa kutumia milipuko, hasa baruti, samaki hao ni hatari kwa afya za wavuvi wenyewe na walaji.

“Changamoto iliyopo ni kwamba wananchi wengi huwa hawajui kutofautisha samaki aliyevuliwa kwa njia halali na yule aliyevuliwa kwa njia za milipuko.

“Tunalazimika kutoa elimu kwa jamii ili kujua tofauti zilizopo kati ya samaki hawa, kwanza samaki aliyevuliwa kwa njia ya mlipuko unapomning’iniza juu huchuruzisha damu nyingi tofauti na yule aliyevuliwa kwa njia ya kawaida,” alisema.

Aidha, Mninko alisema dalili nyingine ya samaki aliyevuliwa kwa mlipuko huwa ametoa mno macho yake nje, lakini aliyevuliwa kawaida huwa ameyatoa kidogo.

“Ukitazama uti wa mgongo wa samaki aliyevuliwa kwa mlipuko, utakuta umevunjika tofauti na aliyevuliwa kawaida huwa haujavunjika.

“Na pindi unapompasua kwa ndani, utakuta utumbo wake unaonekana kama umepasuka tofauti kabisa na wale wanaovuliwa kawaida,” alisema.

Mninko alisema kipindi cha nyuma samaki hao walikuwa wakiingizwa hadi katika soko hilo na kuuzwa kwa wachuuzi hali ambayo iliwalazimu kufanya msako.

Alisema katika msako huo wamefanikiwa kukamata wafanyabiashara 13 hadi sasa ambao walikuwa wakiuza samaki kwenye kizimba namba tano cha soko hilo na bado wanaendelea kuwasaka wengine.

Hata hivyo, alisema wafanyabiashara hao walifikishwa katika Mahakama ya Jiji Sokoine Drive na kesi yao imeshaanza kusikilizwa tangu Desemba 30, mwaka jana.

“Wapo pia mama lishe watatu ambao nao walikamatwa wiki iliyopita wakiwa na samaki ambao inaonyesha wamevuliwa kwa kutumia baruti na wamechukuliwa hatua za kisheria.

“Sasa tunajitahidi kudhibiti katika soko letu, sijui katika masoko mengine hali ikoje, na ndiyo maana ninapata mashaka pia na hao samaki wanaotembezwa huko mitaani, kwa hali ilivyo sasa si rahisi kuwaleta sokoni kwa sababu tunaimarisha udhibiti,” alisema.

Alivishauri vyombo vya dola kuimarisha ulinzi katika maeneo ya bahari na mamlaka za ukaguzi kuhakikisha zinapita kukagua sokoni mara kwa mara.

“Kwa kuwa wavuvi hao hawatumii gharama zozote, mara nyingi huuza samaki wao kwa bei ya chini hali ambayo inafanya samaki wanaokuwa wamevuliwa halali kudoda.

“Hii inasababisha soko kukosa mapato na wafanyabiashara nao kuyumba, wakati fulani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipiga marufuku samaki kuuzwa mtaani, nadhani lile wazo lake ni wakati mwafaka lifanyiwe kazi,” alishauri.

Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa samaki na makusanyo ya soko hilo kwa mwezi, alisema hutegemeana na msimu uliopo.

“Biashara ya samaki haitofautiani sana na ile ya madini, huwa ina msimu na mara nyingi hutegemea hali ya hewa iliyopo. Samaki hupatikana kwa wingi katika kipindi cha joto kwa mfano Oktoba hadi Januari.

“Lakini kipindi cha baridi na mwezi angavu au kukiwa na upepo mkali, wavuvi wanatueleza kwamba huwa wanawapata kwa kubahatisha, sasa ukiwa ni msimu wa samaki wengi hapa sokoni huwa tunakusanya kati ya Sh milioni 2.5 hadi 3, lakini ukiwa ni msimu usiokuwa na samaki wengi, huwa makusanyo yanashuka wakati mwingine hadi Sh milioni 1.5 au 1.7 kwa mwezi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles