23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Sakata la CAG lazidi kutikisa


*Wabunge wa CCM wadai kauliza Zitto zinataka kuigawa nchi

*ACT Wazalendo nao wasema Watanzania wanajua nani mpotoshaji

RAMADHAN HASSAN na AGATHA CHARLES-DAR ES SALAAM/DODOMA

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe, ni mwongo na kauli zake zinakusudia kuigawa nchi baada ya kukimbilia Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kupinga Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana Dodoma, wabunge hao walisema baada ya kukaa Kamati ya Wabunge wa CCM (Caucus) wamemwona mbunge huyo ni adui namba moja.

Akisoma taarifa ya wabunge hao kwa niaba ya Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, alisema hatua zilizochukuliwa na Zitto kuzuia mamlaka ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutekeleza wajibu wake wa kumtaka CAG kwenda kuhojiwa ni kinyume cha sheria na dharau.

Alisema mbunge huyo anayo nafasi kupitia kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kumshauri Spika katika Kamati ya Uongozi kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge kama ilivyoelekeza kanuni ya 2 (3) ya nyongeza ya nane ya kanuni za Bunge.

Pia alisema kitendo cha Zitto kwenda mahakamani hivi karibuni kupinga au kuandika barua kwa mabunge ya nchi zingine ni dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika na mhimili wa Bunge kwa ujumla.

“Kanuni ya 5 (4) na (5) ya kanuni za kudumu za Bunge imeweka utaratibu ambao mbunge ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa Spika anaweza kupinga uamuzi huo. Mbunge atawasilisha sababu za kutoridhishwa kwa Katibu wa Bunge,” alisema na kuongeza:

“Zitto ni mbunge mkongwe ambaye anazielewa taratibu za kikanuni zinazosimamia shughuli za Bunge. Si mara ya kwanza kufanya upotoshaji wa aina hii kwa umma.

“Kitendo cha Zitto kukimbilia mahakamani wakati anayo fursa kama mbunge ya kuujadili muswada na kuufanyia marekebisho ni kitendo kinachoonesha kwamba ana uelewa mdogo wa kanuni za uendeshaji wa shughuli za Bunge.”

Pia alisema taarifa iliyotolewa na Kambi ya Upinzani kwamba kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuwa zimevunjwa si za kweli.

“Hivyo basi tunapenda kuwataarifu kuwa PAC na LAAC hazijafutwa, bali wajumbe wake wametawanywa katika kamati zingine hadi wito wa Spika kwa CAG utakapotekelezwa,” alisema Mapunda.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mlalo, Rashidi Shangazi, alisema kila mmoja ana haki kikatiba lakini Zitto ameitumia vibaya haki yake.

“Tunaona haki ya kwenda mahakamani ni ya kila Mtanzania, anapoona kuna jambo ambalo haliendi sawa, lakini mwenzetu ameitumia vibaya haki hii. Kifupi alitaka kulizuia Bunge lisifanye kazi yake kikatiba,” alisema Shangazi.

Naye, Mbunge wa Siha, Godwin Molel, alimshambulia Zitto kwa kudai kwamba alihusika na ufisadi wakati akiwa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

“Zitto tumwangalie kipindi cha nyuma, ufisadi mkubwa ambao Rais anapambana nao ni uliotokea wakati akiwa Kamati ya PAC na kazi aliyokuwa anaifanya yale maufisadi makubwa ilikuwa ni sehemu ya ufisadi huo. Kimantiki Zitto alitakiwa awe amekamtwa kwa sababu anahusika na ule ufisadi lakini alichokuwa akikifanya ni kutumia mdomo wake na kupokea rushwa na wale waliokuwa hawampi rushwa ndio aliokuwa akiwataja,” alisema Molel.

Kwa upande wake, Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama, alidai Zitto ni kama ameishiwa hoja.

“Rais amemaliza hoja zote sasa hivi wanadandia tu hoja, kuna vyama vinajiendesha kama saccos, mwenyekiti wewe, mhasibu wewe na jamaa alizoea kupiga hivyo ni lazima achanganyikiwe,” alisema Mhagama.

Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Mariamu Ditopile, alisema kama Zitto anaona Bunge ni dhaifu ajiuzulu na awaachie nafasi watu wengine wagombee jimbo lake.

Naye Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, alisema hawatasita kumwelekeza Zitto pindi atakapokwenda kombo.

“Haya yameisha yule ni mwenzetu lazima tumweleze ukweli upo wapi,” alisema Mwamoto.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde maarufu kwa jina la Kibajaji alimtaka Zitto kuacha kutumia siasa za kushinda mahakamani kama zilizokuwa zikifanywa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila.

“Rai yangu kwa Zitto akiendelea kufanya siasa ambazo anaendelea atashitakiwa na mke wa Mtikila, maana anachukua style za marehemu Mtikila za kushinda mahakamani badala ya kushinda kutafuta hoja za watu wake wa Kigoma,” alisema Lusinde.

Alisema Zitto yupo ACT Wazalendo lakini akili anazotumia ni za Mtikila na mke wa Mtikila kama kungekuwa na sheria ya kusimamia stahiki za mumewe ana uwezo wa kumshtaki Zitto ili aweze kumlipa fidia.

“Unawezaje kusema sheria hii ikienda bungeni itapita kwa sababu wabunge wa CCM wote ni makasuku wakati bungeni yupo mkewe (Halima Bulembo) na mkwewe (Abdallah Bulembo) yupo sawa? Zitto anapaswa kujitafakari upya kwa sababu anakoelekea anaenda shimoni kabisa,” alisema Lusinde. 

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Zitto kwa njia ya simu ili kujibu hoja za wabunge hao lakini hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi aliotumiwa.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alitoa taarifa jana iliyosambazwa na Zitto kwa vyombo vya habari kuhusu hoja za wabunge hao.

Ado alisema alifuatilia hoja za wabunge juu ya walichokiita ‘kupambana dhidi ya Zitto Kabwe na wapinzani kwa ujumla wake katika upotoshaji wanaoufanya’ ambako aliunga mkono hatua hizo.

“Leo (jana) ninakusudia kuwaunga mkono wabunge wa CCM kwa azimio lao la kula sahani moja na Zitto kwa kuzijibu hoja zake badala ya kumuachia Spika au Serikali peke yake kujibu. Kama wabunge kwa ujumla wao wataweza kukabiliana na hoja zilizotafitiwa za wapinzani ni mjadala mwingine ambao sitaki kuuingia kwa leo (jana),” alisema.

Ado alisema walichopanga kukifanya wabunge wa CCM, bila kujali wanatumia hoja yenye uzito gani kujibu, ndiyo maana hasa ya siasa.

“Kutarajia mashambulizi ya hoja za kisiasa kujibiwa kwa vitisho na mabavu ya vyombo vya dola kama ambavyo imeanza kujengeka katika miaka ya hivi karibuni ni utamaduni wa ovyo. Kumtisha, kumdhuru au kumuweka korokoroni mtoa hoja badala ya kuikabili hoja yake si siasa,” alisema.

Ado alisema siasa inaleta radha mmoja anaposema, mwingine ajibu au mmoja anapotoa madai mwingine akanushe.

“Refa wa mchezo wa siasa ni umma. Umma wa Watanzania unafahamu nani anasema kweli na nani anapotosha. Umma wenyewe unao uwezo wa kujua mchele ni upi na pumba ni zipi,” alisema.

Pia alisema hatarajii hoja ya kisiasa ijibiwe kwa vitisho kwa sababu si lililokusudiwa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles