25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Rugemalira ataka BoT kutaja waliochota mabilioni ya Escrow

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MFANYABIASHARA James Rugemalira, amemtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) atoe orodha ya waliopewa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow ili yeye asafishike kwa sababu hajalipwa hata senti moja kutoka katika akaunti hiyo.

Mshtakiwa huyo pia ametoa notisi kwa taasisi nyeti tisa akitaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) nchini amwondoe kwenye kesi ya uhujumu uchumi, asipofanya hivyo atawasilisha hoja rasmi za kuondolewa katika kesi hiyo.

Rugemalira alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiarifu mahakama kwamba upelelezi unaendelea na akaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusema hayo, Rugemalira alinyoosha mkono akiomba kuzungumza ndipo Hakimu Shaidi alipomruhusu.

“Kuna maombi nilitoa Januari 30 mwaka huu, naamini yalikubaliwa, nilitegemea upande wa Jamhuri walete ufafanuzi kuhusu Benki ya Standard Chartered Hong Kong iliyokwepa kodi ya Serikali ya Sh bilioni 1.5.

“Nimeandaa nyaraka ya nyongeza nitakabidhi kwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania) ili wakija waje na taarifa kamili. Februari 11 mwaka huu nilitoa notisi ikieleza matatizo yenyewe yalivyo, kuna vipengele vya sheria havitekelezwi,” alisema Rugemalira.

Alisema katika notisi hiyo alieleza kwamba asipoondolewa katika shauri hilo, upelelezi hauwezi kukamilika akiwa gerezani.

“Mheshimiwa hakimu, nilitoa notisi sehemu mbalimbali ikiwemo kwa DPP na imepokelewa, nilitegemea naachiwa leo kwa kuondolewa katika shauri hili,” alidai Rugemalira.

Alidai miongoni mwa taasisi alizopeleka notisi ni Ofisi ya DPP kwa Biswalo Mganga, DCI Robert Boaz, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa BoT, Kamishna TRA, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba na Kamishna wa Magereza.

“Naomba Mahakama ya Kisutu iondoe kesi kama DPP hajawasilisha nole ya kuniondoa katika shauri hili,” alidai Rugemalira.

Alidai kuna barua alimwandikia Gavana wa BoT akieleza kwamba hajawahi kulipwa hata senti moja kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow.

“Fedha nilizolipwa na PAP (Pan Africa Power Solution Tanzania Ltd) ni kutokana na amri ya mahakama, naomba Gavana aorodheshe majina ya wote waliopewa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow ili mimi niwe msafi.

“Gavana amejibu kwamba hatatoa listi ya majina hayo mpaka apate amri halali ya mahakama,” alidai Rugemalira.

Mshtakiwa huyo alimalizia kwa kudai kwamba tarehe ijayo kesi itakapotajwa Februari 27 kama atakuwa hajaondolewa katika kesi, atawasilisha maombi rasmi mahakamani ya kuondolewa kwenye kesi hiyo.

Oktoba 10 mwaka jana, Rugemalira alidai mahakamani  kuwa amemwandikia barua DPP, akimwomba kumwachia huru ili washirikiane kupata Sh trilioni 37 anazoidai Benki ya Standard Chartered na pia Serikali itapata kodi ya zaidi ya Sh trilioni sita.

Rugemalira aliandika barua Oktoba 4 mwaka jana kwenda kwa DPP na kupokewa Oktoba 5, akiomba aachiwe huru ili aweze kushirikiana na Serikali kupata Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered na washirika wake.

Mshtakiwa huyo ameainisha vielelezo kadhaa vinavyoonyesha Standard Chartered ilivyohusika katika sakata la Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).

Miongoni mwa vielelezo hivyo ni gharama zilizokuwa zinatozwa na IPTL dola za Marekani 1.06 kwa kWh ni za chini kuliko zilizokuwa zinatozwa na Kampuni ya Songas dola za Marekani 4.31 kwa kWh.

Kielelezo kingine ni barua aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu Januari 17 mwaka huu akiomba majina ya watu waliolipwa Sh 144,947,669,844.2 zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow kati ya Julai 5, 2006 na Machi 19 mwaka 2014.

Wakati sakata la Escrow lilivyoingia bungeni mwaka 2014 na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa akauti hiyo kwa maelezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilielezwa kuwa fedha za Rugemalira zilikuwa kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi ambazo baadhi aligawa kwa watu waliotajwa.

 Pia inaelezwa fedha nyingine za PAP, ziliwekwa katika akaunti ya kampuni hiyo ya Harbinder Singh Sethi ambapo taarifa ya PAC bungeni ilisema zilisombwa kwa sandarusi na watu ambao hawakutajwa na sasa Rugemalira anataka majina ya watu hao kuwekwa wazi.

Pia katika barua yake hiyo kwa DPP, Rugemalira anadai alieleza PAP kukiri kulipwa na Benki Kuu Sh 164,513,630,314.15 na dola za Marekani 22,198,544.60 na si Sh 309,461,300,158.27 na dola za Marekani 22,198,544.60 kama ilivyokuwa katika hati ya mashtaka kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017.

Aliambatanisha pia nakala ya barua ya BoT yenye kumbukumbu namba NC.130/170/01 iliyoandikwa Februari 18, 2018 (2019) ikiwa ni majibu ya barua yake ya Januari 19, 2019.

Kiambatanisho kingine ni cha gazeti la Financial Times la Julai 20/21 2019 lililotoa taarifa kuwa wadau wameituhumu Benki ya Standard Chartered kwa Serikali ya Marekani kwa kutoa dola bilioni 57 isivyo halali na benki hiyo ilifikia makubaliano na mamlaka za nchi hiyo kwa kukubali kulipa faini ya dola bilioni moja.

“Ninatumaini kwa maelezo hayo yaliyoainishwa katika nyaraka hizi zilizotolewa na ofisi yako kati ya Juni 18, 2019 na Julai 22 2019, utaweza kutumia mamlaka yako chini ya kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi kuniachia huru katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka 2017 ili niendelee na juhudi zangu za kuisaidia Jamhuri kurejesha zaidi ya Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered,” alieleza Rugemalira.

Alieleza hana tatizo na Jamhuri kwa kuwekwa mahabusu kwa muda wote aliokaa huko, kwa kuwa anaamini hatua hiyo ilichukuliwa kwa Jamhuri kupotoshwa na Benki ya Standard Chartered.

Alimwomba DPP kutumia mamlaka yake aliyopewa katika Kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2016 kuagiza aachiwe huru ili achukue hatua katika kesi zake dhidi ya Benki ya Standard Chartered kupitia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

“Iwapo nitaondolewa mashtaka yanayonikabili, itaniwezesha kuendelea na kesi nilizozifungua dhidi ya Standard Chartered na washirika wake ambapo nadai Sh trilioni 20, kiasi ambacho kitaiwezesha TRA kukusanya kodi kutoka kwenye hiyo fedha Sh trilioni 6,” alisema.

Katika barua yake, alieleza kuwa viambatanishi vingine ni nakala ya tozo iliyokuwa imeandaliwa na Tanesco ikionyesha tozo zilizotakiwa kutozwa na IPTL, ambazo zilikuwa ndogo kuliko za kampuni nyingine.

Ameambatanisha pia taarifa ya Dk. Camilo Schutte ya Oktoka 12, 2012 kwenda Benki ya Standard Chartered (SCB), Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) Ltd (SCBHK) na Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd (SCBTZ) iwapo hawataondoa malalamiko yao ya kisheria dhidi ya Tanesco katika kesi ya ICSD namba ARB/10/20, Kampuni ya VIP itaibua madai ya zaidi ya dola milioni 485 kama gharama za usumbufu.

Pia ameambatanisha nakala ya taarifa yake kwa Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd na Jamhuri ya Juni 11, 2013 ikieleza kuwa VIP imechukua hatua ya kukata rufaa kwenye mahakama ya juu ya New York nchini Marekani kwa madai hayo ya dola milioni 485.

Ameambatanisha pia nakala ya Kampuni ya VIP yenye kumbukumbu namba Ref: VIPEM: JB/41/2013 kwenda kwa Gavana wa BoT ya Desemba 5, 2013 kutoiruhusu PAP kulipwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kutoka BoT kwa niaba ya IPTL.

Nyingine ni nakala ya barua yenye kumbukumbu namba NC.53/135/085 ya Desemba 12, 2013 kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndulu ikimweleza Rugemalira kuwa kwa hati ya mahakama iliyotolewa Septemba 5, 2013 Serikali na IPTL malipo yote yameshatolewa kwenye akaunti ya Escrow na kuhamishiwa IPTL Novemba 28, 2013.

Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.                                    

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa mwingine Mwanasheria wa Kampuni ya IPTL, Joseph Makandege, anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles