31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Iddi Simba, Nsa Kaisi wafariki dunia

Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

WAZIRI wa zamani wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya awamu ya tatu, Iddi Simba, amefariki dunia jana Dar es Salaam, wakati akitibiwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Mbali na Simba, kiongozi mwingine aliyefariki ni Kanali mstaafu, Kabenga Nsa Kaisi aliyewahi kuwa msaidizi wa muda mrefu wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa taarifa ya familia jana jioni, mwili wa Iddi Simba ambaye alikuwa mshauri maalumu wa Mufti wa Tanzania, leo utaswaliwa katika Msikiti wa Manyema baada ya swala ya Ijumaa na baadaye kuzikwa makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam

Akizungumza na MTANZANIA jana, mtoto wa marehemu, Sauda Simba Kilumanga, alithibitisha kuwa baba yake alifariki dunia saa tano asubuhi wakati akitibiwa JKCI.

Sauda alisema kwa wakati huo, mara tu baada ya kutokea kwa msiba huo, familia yake ilikuwa ikiendelea kufanya mawasiliano kuandaa taratibu za mazishi ya kiongozi huyo mstaafu ambaye aliwahi pia kuwa mbunge wa Ilala.

“Ndiyo kwanza tumepata taarifa rasmi za uthibitisho kutoka kwa madaktari kuwa baba amefariki. Ni mshtuko na kwa sasa familia bado inaendelea kufanya mawasiliano kwa ajili ya kuandaa utaratibu, ukiwa sawa tutawafahamisha,” alisema Sauda alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana mchana.

Iddi Simba ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Ilala (CCM), mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kisha kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa miaka miwili – 2001 hadi 2002, kisha kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) alikuwa kimya kwa muda mrefu katika medani ya siasa, hadi alipofariki dunia.

Katika nafasi yake ya uwaziri, Iddi Simba alilazimika kujiuzulu mwaka 2002, kutokana na kashfa ya uingizwaji wa sukari mbovu nchini.

Akiwa mbunge Iddi Simba, atakumbukwa kwa msimamo wake kutetea wazawa katika masuala mbalimbali, ikiwamo uwekezaji nchini.

Alilazimika kuandika kitabu kinachotetea uzawa jambo lililomfanya kutofautiana na sera za chama chake cha CCM.

Katika kitabu hicho aliwatetea Watanzania wazawa kwa kueleza kwamba wanastahili kuwekewa mazingira fulani ya kisera ili wajiendeleze na waendeleze rasilimali zilizopo.

Dhana hiyo ilipingwa na kuitwa ni dhana yenye kuchochea hisia za kibaguzi ambapo baadhi ya viongozi wa CCM wakati huo waliwatahadharisha wanachama wao kwamba dhana ya uzawa ni ya Iddi Simba na ni mawazo yake binafsi hayafungamani kabisa na sera za CCM.

Akiwa mbunge mbunge, Idd Simba aliwahi kukaririwa bungeni akisema kwamba lugha ya Kiingereza imesababisha Tanzania iwe na sheria mbaya zikiwamo za madini.

Alisema anaona aibu kwa kuwa alishiriki kupitisha sheria mbaya za madini zinazotumika kuinyonya nchi.

 “Zile sheria ni mbaya na mimi naona aibu kwamba zilipitishwa wakati nikiwa kwenye lile Bunge, lakini unatarajia nini wakati sheria zile zinatungwa kwa Kiingereza, na si wabunge wengi wanaoelewa lugha hiyo,” alisema Iddi Simba wakati huo.

Juni 19, 2013 Iddi Simba alifutiwa kesi iliyokuwa ikimkabili, iliyokuwa na mashtaka manne likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uda.

Kesi hiyo ilifutwa baada ya Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa kuwasilisha hati ya nuio la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kuifuta.

Kanali Kaisi naye afariki dunia

Aliyewahi kuwa msaidizi na mshauri wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Kanali mstaafu Kabenga Nsa Kaisi amefariki dunia jana.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoituma kupitia akaunti yake ya Twitter, aliyewahi kuwa waziri katika Serikali za awamu ya kwanza hadi ya tatu, Profesa Mark Mwandosya, alisema amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha kiongozi huyo mstaafu jana.

Mwanodya aliandika: “Nimepokea kwa masikitiko na majozi makubwa taarifa za kifo cha Kanali (mstaafu) Kabenga Nsa Kaisi, kaka, mwandishi mahiri wa Uhuru na Nationalist, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na Mshauri wa Rais Mkapa. Nafsi yake ipumnzike mahala pema.”

Wakati wa uhai wake, Kanali Kaisi aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kagera, Mara kisha kuwa Kamishna Tume ya Nidhamu ya Viongozi.

Katika kitabu cha historia ya maisha yake, Mkapa anamtaja Kanali Kaisi kuwa mtu muhimu ambaye ndiye aliyebuni jina la ‘Azimio la Arusha’ wakati wawili hao walipokuwa wakifanya kazi katika gazeti la kiingereza la CCM lililoitwa The Nationalist.

Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Kuwaenzi Waasisi wa Taifa, wenye lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanganyika na Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles