28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Ruge aliza wengi

PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTINA GAULUHANGA –Dar es Salaam

MSIBA wa Mkurugenzi wa Vipindi na Utayarishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, umeliza watu wa kada mbalimbali, huku familia ikitangaza mwili wake utaletwa nchini Ijumaa na utazikwa Bukoba Jumatatu.


Ruge alifariki dunia juzi akiwa nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu ya figo zilizoanza kumsumbua mwaka jana.


Jana mamia ya wakazi wa Dar es Salaam wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walijitokeza nyumbani kwa baba wa marehemu, Mikocheni kutoa pole, huku wengine wakitumia mitandao ya kijamii kueleza hisia zao.

MAJALIWA


Waziri Mkuu Majaliwa aliwasili nyumbani hapo saa 5:30 asubuhi akiongozana na viongozi wengine na alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali.


Akizungumza msibani hapo, Majaliwa alisema Watanzania wanatambua mchango alioutoa Ruge kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Majaliwa alisema wakati anaugua, Serikali ilikuwa ikifuatilia mwenendo wa matibabu yake pamoja na kushirikiana na familia ya marehemu ili kuangalia namna ya kusaidiana.


Alisema Ruge kwa upande wa Serikali amefanya kazi kubwa kuanzia Serikali ya awamu ya nne hadi ya tano, hasa katika suala la kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo katika nchi yao na kutambua fursa zilizopo.


“Katika uhai wake, marehemu alikuwa anatoa fedha zake binafsi kwa ajili ya kuwasaidia vijana ili waweze kuchangamkia fursa, kazi ambayo ilipaswa kufanywa na Serikali, lakini aliweza kufanya mwenyewe bila ya Serikali,” alisema Majaliwa.


Aliongeza kuwa Ruge aliweza kuzunguka nchi nzima na kukutana na makundi ya vijana wa Kitanzania ili kuwaeleza uzalendo na kutumia rasilimali zilizopo katika kuendeleza taifa lao.


Alisema vijana walikuwa na kiongozi aliyeweza kuwaongoza katika mambo ya fursa, aliweza kuwafungua mawazo na kutambua umuhimu wao ili waweze kupata uelekeo.


“Kuna vijana walikuwa wanashindwa kujiongoza, hivyo basi walipokuwa wanahudhuria semina za fursa, aliweza kuwashika mkono na kuwaelewesha ili waweze kujitambua na kuzifuata,” alisema.

DK. TULIA


Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema Ruge alimshauri kugombea ubunge, lakini kabla ya kugombea alimwambia anapaswa kufanya kitu cha tofauti ambacho kitaleta mwamko kwa jamii.


“Aliponiona nina ‘impact’ kwa jamii, alinishauri kugombea ubunge, lakini kabla sijafanya hivyo, alinambia kwanza nifanye kitu katika jamii ambacho kitaweza kuleta ushawishi, ndipo nilipoanzisha mfuko wa ‘Tulia Trust’ ambao unajihusha na jamii moja kwa moja,” alisema.


Tulia alisema kuwa Ruge aliongeza kumwambia kuwa mfuko hautoshi, hivyo basi anapaswa kufanya kitu kingine ambacho kitahusisha jamii na kuleta tija, ndipo alipoamua kuanzisha tamasha la ngoma asilia.


Alisema wakati anaumwa, alipata nafasi ya kwenda kumuona na alimwambia kuwa akifa wasilie wala kupiga nyimbo za mazishi kwenye msiba wake, bali wafanye sherehe ili kufurahia yale aliyofanya katika uhai wake.


“Kama binadamu hauwezi kuacha kulia kwenye msiba kwa sababu ukiondokewa na mpendwa wako, ila tutayakumbuka na kuyaenzi yale aliyoyaanzisha,” alisema.

MWIGULU


Mbunge wa Iramba Mashariki, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema kuwa Ruge alikuwa kielelezo cha ubunifu jambo ambalo lilikuwa msaada mkubwa kwa taifa na lilimgusa Rais Dk. John Magufuli.


“Alikuwa akitambua fursa na kushirikisha vijana, ambayo ilikuwa inazunguka nchi nzima, mara ya mwisho kuwasiliana nae ni pale alipoanza kuugua na aliweza kufuatilia afya yake mara kwa mara,” alisema.
Alisema hili ni pigo la taifa na tasnia ya habari, jambo ambalo limemfanya Rais Magufuli kuwa wa kwanza kutoa salamu za rambirambi.

ZITTO


Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa kifo cha Ruge si kilio ni sherehe kwa sababu ameacha alama kwa vijana na taifa kwa ujumla.


Alisema amefanya kazi kubwa ndani ya jamii ya kufungua fursa kwa vijana na matokeo chanya yanaonekana.
“Ruge ameondoka, hatutamuona tena, lakini huu sio msiba ila ni sherehe ya kusherehekea mazuri aliyofanya kwa sababu ameacha alama, ni jukumu letu kama jamii kujiuliza tukifa tutaacha alama gani,” alisema Zitto.

DK. ABBAS


Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema kuwa kuondoka kwa Ruge kuna maana kubwa katika sekta ya habari kwa sababu aliajiri vijana wengi na kuwapa nafasi ya kuonesha vipaji.


“Uthibitisho ni vijana waliopo katika kituo chake cha televisheni ambao wanaonyesha uwezo mkubwa na tayari alikuwa na mpango wa kuanzisha kituo cha vijana wenye vipaji, hivyo basi tuna changamoto kubwa ya kufuata nyendo zake,” alisema Dk. Abbas.

MHAVILE
Mkurugenzi wa ITV, Joyce Mhavile alisema kifo cha Ruge ni pigo kwa tasnia ya habari kwa sababu alikuwa anaelimisha vijana kuchangamkia fursa na kuonesha namna ya kuzitumia.

KIKWETE


Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliandika; “Nimelemewa! Nakosa maneno ya kuelezea huzuni na majonzi niliyonayo kwa kifo cha Ruge Mutahaba.


“Taifa limepoteza kijana wake mahiri, mbunifu na mzalendo wa kweli. Nimepoteza rafiki, mshirika mwaminifu na mtu ambaye amenisaidia kwa mengi katika uongozi wangu na hata baada ya kustaafu.
“Moyo wangu uko pamoja na wazazi wake, ndugu zake na familia yake katika kipindi hiki kigumu. Namuombea kwa Mola ampe mapumziko mema peponi. Ameen.”

LISSU
Kupitia mtandao wa kijamii, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliandika; “Inaelekea huu ni msiba mkubwa sana kwa taifa letu. Viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi mbalimbali na wananchi wa kawaida wamejitokeza hadharani kutoa salamu zao za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki zake Ruge.


“Hii ni sawa sawa, kwani Ruge Mutahaba hakuwa mtu mdogo kwenye jamii yetu. Hivyo, na mimi naungana na waombolezaji wengine kumuomboleza kijana huyu.


“Naomba nikiri mapema mimi sikumfahamu sana Ruge. Nilikutana naye mara mbili au tatu aliponifuata bungeni mwaka 2012 (kama sikosei) ili nisaidie kumpatanisha yeye na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Mh. Josef Mbilinyi ‘Sugu’. Nilifanya hivyo.


“Zaidi ya hapo, nilimfahamu kwa juu juu kama mmoja wa wakurugenzi wa Clouds Media Group.
“Kwa hiyo siwezi kumzungumza sana kwa mema au kwa mabaya yake. Siyafahamu sana. Ninachotaka kukizungumzia ni haya maombolezo ya kifo chake.”

FAMILIA
Akitoa ratiba ya mazishi, msemaji wa familia Annick Kashasha, alisema mwili wa marehemu utawasili nchini kesho ukitokea Afrika Kusini.
“Machi 2 itakuwa siku ya kuaga ili kutoa fursa kwa waombelezaji kutoa heshima zao za mwisho na Machi 3, utasafirishwa kuelekea mkoani Kagera katika eneo la Kizilu na mazishi kufanyika Machi 4,” alisema Kashasha.

MATIBABU YAKE
Februari 18, mwaka huu ndugu wa Ruge waliomba msaada wa fedha kulipia gharama za matibabu yake.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha Clouds, Mbaki Mutahaba ambaye ni kaka wa mkurugenzi huyo, alisema Ruge anapatiwa matibabu Afrika Kusini ambako kwa siku gharama ni Sh milioni 5.
“Alianza kuumwa mwaka 2018, alilazwa katika Hospitali ya Kairuki kisha akapelekwa India, ‘sapoti’ ni kubwa tunashukuru na hata Rais Dk. John Magufuli ametoa mchango na anaendelea.


“Ana figo ambayo haipo sawasawa, ilikuwa lazima wambadilishe. Madaktari wa Hospitali ya Kairuki na Muhimbili wakashauri apelekwe Afrika Kusini maana ni karibu zaidi, lakini gharama ni kubwa.
“Kule (Afrika Kusini) mfumo wao wa malipo ni tofauti, unapaswa kulipa fedha taslimu. Kuna namba rasmi imeandikishwa kwa jina la mdogo wetu Kemilembe Mutahaba, unaweza kutusaidia kwa namba hiyo,” alisema.

HISTORIA YA RUGE
Ruge Mutahaba alizaliwa mwaka 1970 huko Brooklyn, New York nchini Marekani.
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Arusha kuanzia darasa la kwanza hadi la sita kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Mlimani, Dar es Salaam kukamilisha elimu yake ya msingi.


Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam kwa masomo ya awali ya sekondari na kisha masomo ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha San Jose nchini Marekani kusomea shahada za kwanza katika masoko na fedha.
Wakati akiendelea na masomo nchini Marekani, bosi mwenzake katika CMG, Joseph Kusaga alikuwa akiendesha Klabu ya Disko la Usiku (Night Club Disco), ambayo pia ilijulikana kama Clouds Disco.


Hivyo, Ruge akawa mgavi pekee wa vifaa vya kuendeshea klabu hiyo ya usiku, yaani akiifanya kazi hiyo akiwa nchini Marekani.
Wakati aliporudi Tanzania baada ya kukamilisha masomo yake ya chuo kikuu, aliunganisha nguvu na Kusaga kuanzisha CMG wakati huo ikiwa katika Jiji la Arusha.


CMG hulenga kuchochea na kuwezesha vijana wa Kitanzania chini ya miaka 35 kupata fursa zitakazowawezesha na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa lao.
Ruge hajaoa rasmi, lakini alikuwa akiishi na mtangazaji Zamaradi Mketema na wana watoto wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles