ROMA AMEONYESHA MFANO, WASANII SAIDIENI ELIMU

0
938

NA MWANDISHI WETU

IKIWA ni miezi miwili ipite toka msanii wa Bongo Fleva katika miondoko ya hip hop, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ kutekwa na watu wasiojulikana na baada ya siku tatu kuonekana akiwa mwenye maumivu makali mwilini, wiki hii alitembelea Shule ya Msingi Mchikichini, iliyopo Mbagala Rangi Tatu, jijini Dar es Salaam na kuonyesha namna anavyoweza kutumia nafasi yake kwenye jamii kusaidia sekta ya elimu.

Nyimbo zake nyingi za harakati toka alipoingia kwenye muziki mwaka 2007, Roma amekuwa kama taa ya kuangaza matatizo mbalimbali, yakiwamo ya walimu na kuyaimba kwenye nyimbo zake ambazo zimefanikiwa kuwashtua wahusika na kufanya maamuzi yenye tija.

Katika mahojiano yake na waandishi wa habari shuleni hapo, Roma aliweka wazi kuguswa zaidi na sekta ya elimu, hasa ukizingatia kitaaluma yeye ni mwalimu wa sekondari, licha ya kutofundisha kwa muda mrefu kutokana na kujikita zaidi kwenye muziki wa hip hop uliompa mafanikio.

Alieleza namna alivyo na uhusiano mzuri na somo la hisabati na pale pale shuleni alionyesha ni jinsi gani anavyoweza kufundisha somo hilo na wanafunzi wakamwelewa vizuri.

Alifafanua namna anavyowapenda walimu, ndiyo maana kwenye nyimbo zake nyingi amekuwa akiwaimba na kuzitaja changamoto zao, kifupi amekuwa kama msemaji wao kupitia muziki.

Aliahidi pia kutoa vitabu vya hisabati kwa darasa moja au mawili kulingana na uwezo alionao, ili pia kutoa fursa kwa wengine kuunga mkono wazo lake hilo na kuchangia vitabu, madawati, chaki nk.

Tukio la Roma kusaidia sekta ya elimu nalifananisha na lile alilolifanya mwanamuziki wa Marekani, Rihanna kupitia taasisi yake ya Rihanna’s Clara Foundation, alipotembelea nchi ya Malawi na kusaidia shule kadhaa ambazo wanafunzi wa kike walikuwa wakipata tabu kutokana na umbali kutoka nyumbani mpaka shule.

Kwa hiyo, ni jambo la kawaida wasanii kusaidia jamii, ingawa hapa nyumbani suala hilo limekuwa adimu kidogo, licha ya wasanii wake kuingiza fedha nyingi, wameshindwa kurudisha kwa jamii na kutatua changamoto kwenye sekta mbalimbali.

Naamini Roma ameonyesha njia ili wasanii wengine wapite, ni jambo jema staa kutumia umaarufu wake kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na si jambo baya hata shule za mikoani zikapata misaada kama hii kwa kuwa nazo zina uhitaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here