23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

STEREHE KWA SANA, UBINAFSI NI TATIZO KWA SANAA YETU

HAKUNA msanii ambaye hapendi kupanda juu kisanii. Kila msanii anapenda kufanikiwa. Muhimu kwao ni kuwa na mafanikio.

Kinachoendelea ni kutafuta njia za kupanda zaidi na zaidi kisanii. Hapo sasa wengine hujikuta wakiingia kwenye njia zisizofaa.

Wapo wale wanaoamini mambo ya kishirikina. Hao huenda kwa sangoma kwenda kuangalia namna ya kupandishwa nyota zao ili wapate mashabiki wengi.

Wengine ni wale wanaoamini katika kiki. Hawa ni sampuli za akina Pen Pol, Diamond, Harmonize, Harmorapa na wengine wa namna hiyo. Hao wanaamini bila kiki hawataweza kuwa juu kisanii.

Lakini kuna wale wenye mitazamo mizuri zaidi; hawa huamini katika kazi. Naweza kuwataja wasanii wachache ambao kazi zao zinaongea badala ya kiki.

Msanii wa kike asiyechuja kwenye Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Jaydee’ ni mfano wa wasanii wanaoamini katika kazi bora.

Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ni aina ya wasanii ambao wanaamini kwenye ubora wa kazi. Mfano ukimwangalia Profesa Jay, hata kabla hajawa Mbunge wa Mikumi, mavazi yake yalikuwa ya heshima.

Ni wapi umemuona Profesa Jay akivaa mavazi ya hovyo? Hakuna. Wakati mwingine alipanda jukwaani na suti. yote hiyo ni kulinda heshima yake. Aliamini kwenye mashairi yake na si mavazi.

Bongo Muvi yupo Jacob Stephen ‘JB’, Single Mtambalike ‘Richie’, Ndumbangwe Misayo ‘Thea’, Ahmed Salim ‘Gabo’ na wengine ambao kazi zao ndizo zinazowaweka juu badala ya kujiingiza kwenye kiki.

Ni suala la staili tu, huku lengo likiwa ni lilelile – kutusua kisanii. Tatizo ni pale ambapo tayari msanii ameshapata mafanikio na anapotakiwa kutunza asitetereke.

Wasanii wetu wengi wanashindwa kujua kuwa ustaa unatakiwa kutunzwa. Unaweza kuwa juu leo, lakini miaka mitatu baadaye ukashuka na kusahaulika kabisa.

Ili jambo hilo lifanikiwe, lazima wasanii waache ubinafsi, washirikiane na wenzao na wasifanye starehe kupita kiasi. Ustaa unalindwa.

Ni rahisi kupaa kisanii lakini ni ngumu sana kutunza ustaa wako. Lazima ubunifu uchukue nafasi, uwekezaji wa rasilimali sanaa na hata mali nyingine za kawaida.

Mfano wewe ni msanii, lakini ni vyema kuwekeza kwenye biashara mbalimbali. Tumia jina lako kutengeneza fedha. Kipaji chako kiwe na maana kwako.

Ukishtuka, badilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles