ROBERT SWEYA: MKUU WA SHULE ALIYEJITOLEA POSHO YAKE KUNUNULIA WALIMU CHAI

0
780
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igaganulwa, Robert Sweya
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igaganulwa, Robert Sweya

Na DERICK MILTON, SIMIYU

WALIMU hasa wa vijijini wanakabiliwa na matatizo mengi, mojawapo ni suala la mishahara duni.

Kwa kutambua changamoto wanazokabiliana nazo walimu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igaganulwa, iliyopo kata ya Dutwa, Halmashauri ya Bariadi Vijijini, mkoani Simiyu, takribani kilometa zaidi ya 20 kutoka Mjini Bariadi, Robert Sweya ameamua kutoa sehemu ya mshahara wake kuwanunulia walimu chai ikiwa ni motisha katika kuwapa ari ya kufundisha.

Mwalimu Sweya anasema; “mimi ni mwalimu kama walimu wengine, maumivu na mateso yao nayafahamu na nimeyapitia. Mwalimu Sweya anasema aliamua kuwapa motisha hiyo walimu wenzie kwa kutambua shida na tabu wanazozipata.

Anasema hatua hiyo pia imewafanya wawe na ari ya kazi na kushirkiana katika kila jambo, hakuna mgogoro wowote ambao umewahi kutokea kati yake na walimu.

Mwalimu Sweya (40) anasema Serikali ilianzisha utaratibu kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kuwapatia malipo ya madaraka, ikiwa ni nyongeza ya mashara wake kutokana na nafasi aliyonayo.

Kwa shule za msingi walimu wakuu wamekuwa wakipokea nyongeza ya Sh 200,000 kwa ajili ya usafiri na mawasiliano, hivyo anapopata fedha hizo huamua kuwagawia na walimu anaowaongoza.

Sweya anaweza kuwa ni mwalimu mkuu wa kwanza kutoa fedha zake kwa ajili ya kuwapatia motisha walimu ili kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii.

Anasema watu wengi wamezoea kuona mwajiri ndiye anayetakiwa kutoa motisha kwa watumishi wake, lakini kwa shule hiyo ambayo ni mali ya serikali, hali ni tofauti.

Kitendo cha Mwalimu Sweya kimeonekana ni cha kipekee machoni mwa wengi hata kufikia hatua baadhi ya watu wanajiuliza huenda ametumwa.

Mwalimu mkuu huyo anasema kuwa kupitia malipo ya madaraka ambayo walimu wakuu wamekuwa wakipatiwa, aliamua kuitumia na walimu wenzake.

Anasema licha ya kuwa na familia ya mke mmoja na watoto sita, ambao baadhi yao wanasoma na wengine wakiwa bado hawajaanza shule, kipato anachopata kinamwezesha kumudu maisha yake na kutunza familia.

Anasema amekuwa akitoa fedha hiyo kwa muda wa mwaka mmoja sasa, tangu ateuliwe kuwa mwalimu mkuu mwaka jana.

Walimu wa shule hiyo ambao idadi yake inafikia 22 kila asubuhi wananunuliwa chai na maandazi.

Mwalimu Sweya anasema katika fedha anayoipata huwa anatoa Sh 60,000 kwa ajili ya chai ya walimu wake.

Anasema kitendo hicho kimemsaidia mno kuwa karibu na walimu wake ambao wanafanya kazi wakiwa na shibe, tofauti na wa shule nyinginezo ambazo hakuna utaratibu wa walimu kupata kifungua kinywa kila asubuhi.

Anasema kuwa walimu wengi wamekuwa wakijisikia vibaya kwa kitendo cha mwalimu mkuu kupewa posho huku wao wakiachwa hivi hivi, hivyo hususia kazi na kumwachia mkuu ahangaike nazo hata pale anapokuwa nje ya kituo cha kazi.

“Shule nyingi mwalimu mkuu amekuwa akiachiwa kazi zote azifanye peke yake, ushirikiano umepotea kwa sababu ya posho tunayopata. Hata zikihitajika taarifa hakuna mwalimu wa kukusaidia, kila mwalimu anakwepa kukupa ushirikiani,” anasema Sweya.

Anasema hali hiyo ilianza kujitokeza katika shule yake, akawa na wakati mgumu pindi anapohitaji msaada lakini sasa hivi mambo yamekaa sawa.

“Awali ilikuwa baadhi ya viongozi wakija shuleni kuhitaji baadhi ya taarifa, usipokuwapo mwalimu mkuu basi hawampi ushirikiano. Upatikanaji wa taarifa unakuwa mgumu, tukio lolote likitokea walimu wanasema hiyo ni kazi ya mwalimu mkuu,” anasema Mwalimu Sweya.

Anasema tangu ameanzisha utaratibu huo amekuwa akifanya kazi kwa karibu mno na walimu wenzake hali inayomrahisishia utendaji wa kazi.

Mbali na hayo Sweya anasema walimu wamekuwa wakijituma kwa kiwango kikubwa kufanya kazi kitendo kinachoifanya shule yake kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa.

Anasema kutoa motisha hiyo kwa walimu wenzake kumempunguzia majukumu kwani awali alikuwa anakabiliwa na kazi nyingi.

Wakizungumzia motisha hiyo, walimu wa shule hiyo wanasema jambo linalofanywa na mwalimu mkuu wao ni kubwa si la kubezwa kwani limechangia kwa kiasi kikubwa kuwaongezea ari ya kazi tofauti na ilivyokuwa awali.

Mmoja wa walimu hao, Martha Sungwa anasema kuwa kabla ya kuanza kununuliwa chai na mkuu wao, walikuwa wakilazimika kufuata huduma hiyo takribani kilometa tatu hadi katika mji wa Dutwa, hali ambayo ilikuwa ikipoteza muda wa kufanya kazi.

“Hapa shuleni hatuna huduma ya chai wala chakula cha mchana, tulikuwa tukilazimika kwenda nje ya shule ambako ni mbali kidogo, hali iliyokuwa ikitufanya tutumie hadi muda wa kuwa darasani.

Sasa hivi hatuna muda wa kupoteza, muda wa kipindi tunakuwa darasani kila mwalimu anakuwa busy na kufundisha na si kuzurura kutafuta chakula,” anasema Mwalimu Sungwa.

Anasema kitendo kinachofanywa na mwalimu mkuu kinawahamasisha mno kupenda kazi yao, pia wanaona mabadiliko kwa wanafunzi kwani wamejikita zaidi katika kufundisha na vinginevyo.

“Ukishiba unakuwa na nguvu hata ya kufundisha, lakini ukiwa na njaa unakuwa unawaza utakula nini, wapi na saa ngapi, hata darasani unapoteza umakini.

Hata hivyo, anaiomba Serikali kumwongezea malipo mwalimu mkuu huyo ili motisha iweze kuongezeka.

Kwa upande wake Mwalimu Sai Mageta anasema; “Tunatamani hata siku moja mwalimu mkuu wetu aongezewe malipo haya, ili nasi tunufaike pia hata kwa kupatiwa huduma ya chakula cha mchana hapa shuleni, tukipatiwa huduma hii ni imani hata matokeo ya darasa yajayo ya darasa la saba yatakuwa yamepanda kwa kiasi kikubwa kwa kuwa muda mwingi tutakuwa tunautumia tukiwa shuleni hata habari ya kuwahi kurudi nyumbani hatutakuwa nayo.”

Naye Mratibu wa Mpango wa Kuboresha Elimu shuleni wa Halmashauri ya Bariadi, Isaya Adam anasema jambo linalofanywa na mwalimu mkuu huyo linapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wakuu wengine wa shule.

Anasema kufanyika kwa jambo hilo ni matokea chanya ya Mpango wa Kuboresha Elimu Shuleni (Equip), ambapo mwalimu huyo alianza utaratibu huo baada ya mpango huo kuanzishwa.

“Kupitia mpango huo walimu wamekuwa wakipewa mafunzo mbalimbali ya kuboresha elimu shuleni kwao, moja ya mafunzo hayo ni kujituma kufanya kazi ili kuongeza ufaulu,” anasema Adam.

Anasema kupitia mradi huo jumla ya waratibu elimu kata 21, walimu wakuu 73 na walimu wakuu wasaidizi 73 wamepata mafunzo ya uongozi bora wa shule.

Agosti mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI ulieleza mkakati wa kuanza kutoa posho ya madaraka kwa viongozi wa sekta ya elimu.

Waraka ulielekeza kwamba posho hizo zilianza kuingia Julai, 2016 kwenye akaunti za baadhi ya shule kwenye kata husika zenye shule za msingi na sekondari.

Ulibainisha wazi nyadhifa za viongozi wa elimu watakaopata hizo posho na viwango vya posho hizo,  kama ifuatavyo:
Wakuu wa shule, kwa maana ya shule za sekondari posho yao ya madaraka ni Sh 250,000.

Waratibu elimu kata ambao katika kata zao kuna shule za msingi na sekondari, posho yao ya madaraka ni Sh 250,000.
Walimu wakuu wa shule za msingi posho yao ya madaraka ni Sh 200,000.

Posho hii ya madaraka kwa viongozi wa elimu imekuja wakati ambapo kuna elimu bure, maana yake ni kwamba shuleni hakuna michango ya aina yoyote ile inayomuhusisha mwanafunzi moja kwa moja, kwa maneno rahisi shuleni hakuna chanzo cha fedha zaidi ya miradi midogomidogo ya shule ambayo hawawezi kuitegemea.

Pamoja na kwamba posho hii ni msaada mkubwa kwa viongozi elimu, yaani wakuu wa shule na waratibu elimu kata, ikumbukwe kwamba viongozi hawa wa elimu hawafanyi kazi peke yao.

Kuna kundi kubwa la walimu nyuma yao ambao ndiyo watendaji na watekelezaji wakuu wa mipango na mikakati ya elimu.

Ni dhahiri kwamba kundi hili kubwa la walimu ni muhimu sana kumulikwa kwa kuwa ndiyo kila kitu katika elimu ya taifa letu.

Kama hali itabaki hivi, matabaka kati ya mkuu wa shule na walimu wake ni lazima litakuwapo.

Walimu wanahisi kwamba huu ni mwendelezo wa kusahaulika, kudharaulika na kutokutambiliwa kwa mchango wao na serikalini. Jambo linalowapunguzia ari ya kufanya kazi kwa bidii. Ndio maana Mwalimu Sweye akaamua kujiongeza.

Posho hii imejenga makundi kati ya walimu wakuu na walimu wa kawaida, hivyo hasara yake ni kwamba tunaweza tusipate matokeo tuliyoyatarajia.

Haya yote yamekuwa sugu kwa visingizio vingi ikiwemo uhakiki kwa sasa, lakini tunashuhudia migawanyo mipya ya hela kila kukicha.
Sasa basi, Serikali inapaswa kutambua ni kipaumbele gani muhimu cha walimu ili kifanyiwe kazi kwa namna itavyowezekana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here