27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU- 6: Sefue: Ballali alikuwa mgonjwa tangu akiwa nchini

Daudi Ballali
Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Ballali

Na Waandishi Wetu

SAFARI ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali mkoani Dodoma ilikuwa ni wito wa kiongozi mmoja wa ngazi ya juu serikalini, MTANZANIA limebaini.

Mwenendo wa uchunguzi wa utata wa kifo cha marehemu Ballali uliofanywa na gazeti hili ambalo lilifika mjini Dodoma kufuatilia kilichojiri mkoani humo, umebaini kuwa Ballali aliitikia wito huo wakati ambao alikuwa anajitayarisha na safari yake ya kuelekea nchini Marekani mwishoni mwa Julai, 2007.

Wachunguzi wa mambo wanakisia kuwa Serikali ilikuwa inatafuta njia za kuzima kashfa hiyo ya EPA ambayo iliibuliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ambaye anabaki katika kumbukumbu kama kinara aliyeongoza vita dhidi ya wale waliochota fedha hizo ndani ya Benki Kuu.

Katika uchunguzi wake huo, gazeti hili limebaini kuwa Ballali alikutana na kiongozi huyo wa juu wa Serikali ingawa haijulikani mambo waliyozungumza.

Taarifa zilizopatikana mkoani Dodoma, Dar es Salaam na kwa watu wa karibu kabisa na Ballali nchini Marekani zinaeleza kuwa; mara baada ya kukutana na kiongozi huyo wa juu serikalini, ndipo alikwenda pia kuonana na Kamati ya Fedha na Uchumi kwa ajili ya kuhojiwa.

Wakati vikao baina ya marehemu Ballali na kamati hiyo vikiendelea, inaelezwa kuwa kulikuwa na jitihada za kumshawishi kuzungumza anachokijua kuhusu wizi huo, kitendo kilichoonekana kumkera wakati ambapo tayari alikuwa amesisitiza kuwa tuhuma dhidi yake hazina ukweli na kwamba yeye ni mtu safi.

Pamoja na Bunge kumshinikiza kuwataja waliokwapua fedha za EPA na kama alikiuka taratibu za kazi yake kutokana na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Serikali au wale wa chama tawala, Ballali bado alisisitiza msimamo wake ule ule.

Ofisa mmoja wa juu wa Bunge aliyehojiwa na gazeti hili, lakini akikubali maelezo yake yachapishwe gazetini kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema Ballali alitishia kuchukua uamuzi mgumu baada ya kukerwa na maswali ya Kamati ya Fedha na Uchumi ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mbunge wa Handeni (CCM), Dk. Abdallah Kigoda.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliozungumza na MTANZANIA, Devotha Likokola na Fatma Fereji walikiri kamati yao kukutana mara kwa mara na Ballali, kikiwamo kikao hicho cha mwisho cha Julai, 2007.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walikiri kutokea kwa mvutano mkali katika kikao hicho kilichomhusisha Ballali.

Kumbukumbu za kibunge zilizopekuliwa na MTANZANIA zimeonyesha kuwa kamati hiyo mbali na kuwa chini ya uenyekiti Dk. Kigoda, Makamu wake alikuwa Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM), Hamza Mwenegoha.

Wajumbe wa kamati hiyo walio katika kumbukumbu rasmi za Bunge walikuwa Elizabeth Batenga, Andrew Chenge na Antony Diallo, ingawa alipohojiwa na gazeti hili alikana kuwa mjumbe na kusema kuwa alikuwa akishiriki kwenye kamati hiyo kama mmoja wa watu kutoka serikalini, alikataa kuzungumzia chochote kuhusu taarifa za Ballali.

Wengine ni Fatma Abdulhabib Fereji, Josephine Genzabunge, Athuman Janguo, marehemu Siraju Kaboyonga, Eustace Katagila, Anna Maulida Komu, Clemence Lyamba, Dk. Binilith Mahenge, Monica Mbega, Hamad Rashid Mohamed, Felix Mrema na Mossy Mussa.

Pamoja na hao wamo pia Devotha Likokola, Damas Nakei, Richard Ndassa, Omary Nibuka, Suleiman Ahmed Sadia, Martha Umbulla, Mzee Ngwali Zubeir, Sijapata Nkayamba na Charles Muguta Kajege. Mtaalamu wa kamati alikuwa Laurence Makigi na Katibu wa Kamati alikuwa Michael Kadebe.

Ni mwenendo huo wa maelewano tata, ndio uliomlazimisha Ballali kutotumia muda mrefu mkoani Dodoma na inaelezwa kuwa akiwa hapo pia alipata fursa ya kukutana kwa nyakati tofauti na baadhi ya wabunge, mawaziri na maofisa kadhaa wa Bunge.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA mkoani Dodoma ambako marehemu Ballali aliitwa mwishoni mwa Julai 2007, umeonyesha kuwa baada tu ya kumaliza shughuli alizokuwa ameitiwa, aliondoka akitumia ndege ya Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.

Ripoti zilizokusanywa jijini Dar es Salaam, zimeonyesha baada tu ya kutoka Dodoma kati ya Julai 27 na 28, Ballali aliondoka na kuelekea nchini Marekani.

Kuna taarifa za kukanganya, wakati ripoti nyingine kutoka serikalini zikidai kuwa Ballali alikwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuangalia afya yake huku akiwa na matumaini ya kurejea baada ya muda mfupi.

Taarifa kutoka kwa ndugu zake wa karibu zinaeleza kuwa Ballali alikwenda nchini humo kikazi na ilionyesha angerejea baada ya muda mfupi.

Mmoja wa watu wa karibu na Gavana huyo aliliambia gazeti hili kuwa Ballali aliaga ofisini kuwa atakuwa nje ya nchi kwa muda usiopungua wiki mbili.

Katika mahojiano yake na MTANZANIA, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani wakati huo, Balozi Ombeni Sefue, alisema ingawa hakujua ugonjwa uliokuwa ukimsumbua marehemu Ballali, lakini alichokuwa akikifahamu ni kwamba Gavana huyo hakuanza kuumwa alipokwenda Marekani.

“Tangu akiwa Gavana hapa nchini, marehemu Ballali alikuwa anasumbuliwa na maradhi,” alisema Balozi Sefue, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Serikali aliyeshiriki mazishi ya Ballali.

Balozi Sefue, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi, anasema hakuwahi kumjulia hali Ballali nchini Marekani wakati akiwa mgonjwa.

“Sikuweza kumuona kwa sababu wakati mimi napata taarifa za ugonjwa wake, yeye tayari alikuwa yupo nje ya Jiji la Washington,” alisema Sefue, ambaye maelezo yake mengine aliyoyatoa kwenye mahojiano yake na gazeti hili yataendelea kuchapishwa kwenye mfululizo wa habari hii.

Wakati akiwa amefika Marekani, inaelezwa kuwa hali ya kiafya ya Ballali ilianza kuzorota ghafla tofauti na wakati ambao alikuwa anaondoka hapa nchini.

Hata hivyo, Serikali haikutoa tamko lolote kuhusu hali ya afya ya Gavana huyo na hata taarifa za ugonjwa wake zilianza kuripotiwa na magazeti.

Wakati magazeti yakianza kuripoti juu ya afya ya Ballali, wakati huo sakata la EPA lilikuwa limetanda kwenye kurasa za mbele za vyombo hivyo vya habari na serikali iliendelea kukaa kimya.

Hatua hiyo ya Serikali na taarifa zilizokuwa zikiripotiwa kwenye magazeti ziliibua hisia kinzani kutoka kwa jamii, ambako kundi moja lilikuwa na imani kuwa huenda Ballali alikuwa amedhuriwa, huku jingine likiwa na hisia kwamba alikuwa amekimbia tuhuma zilizokuwa zikimkabili au ulikuwa ni mkakati wa Serikali kumficha.

Taarifa za Ballali kulazwa hospitali zilivuja na kuvifikia vyombo vya habari muda mfupi tu baada ya kufika Marekani, hali iliyoibua utata zaidi.

Katika kipindi chote hicho, Serikali haikuwahi kutoa taarifa zozote kuhusu Ballali wala kile kilichokuwa kinamsibu hadi ilipotimu Desemba katikati.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiadhimisha miaka miwili ya utawala wake wa awamu ya kwanza aliyotimiza Desemba 21, Rais Jakaya Kikwete alikiri kufahamu kuhusu kuugua kwa Ballali, lakini alikanusha uvumi kwamba Gavana huyo alikimbia tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa BoT.

Inaelezwa wakati Rais Kikwete akiuthibitishia umma kuhusu kuugua kwa Ballali, tayari Gavana huyo alikuwa amekwisha andika barua ya kujiuzulu ambayo ilichapwa kwenye moja ya magazeti hapa nchini kabla ya serikali kukanusha taarifa hizo,

Licha ya Serikali kukana, hata hivyo katika uchunguzi wake, gazeti hili limebaini kuwa Ballali aliandika barua ya kujiuzulu wakati akiwa amelazwa hospitalini, huko Boston, nchini Marekani.

Inaelezwa kwamba siku Kikwete alipokutana na waandishi wa habari, ndiyo siku ambayo barua ya kujiuzulu iliyoelezwa kuandikwa na Ballali ilipotumwa na kupokewa Ikulu, lakini hakukuwa na taarifa rasmi juu ya suala hilo.

Baadaye waandishi wa habari walipohoji juu ya suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, aliwaambia Rais Kikwete yuko likizo na kwamba “kama kuna barua kama hiyo hushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi serikalini” na Rais kuifanyia kazi atakapomaliza likizo.

Usikose kufuatilia safari ya ugonjwa wa Ballali kesho.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles