23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ridhiwani Kikwete aahidi kupigania bajeti ya Chalinze

Na Mwandishi Wetu, Pwani

MBUNGE wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, ameahidi kushauriana na madiwani wenzake kwenda kujenga hoja katika vikao kwa ajili ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kuongezewa fedha za ujenzi wa miundombinu ya Halmashauri ya Chalinze ili ufanyike haraka kwa faida ya maendeleo ya wana Chalinze.

Akizungumza mjini hapa jana wakati wa mwendelezo wa ziara maalumu ya kutembelea ofisi za Tarura-Chalinze, Ridhiwani, ametaka kujua mpango mkakati wa namna ya kuboresha baadhi ya barabara zilizo katika halmashauri hiyo ambazo ni kero kwa kipindi kirefu.

“Chalinze tuna barabara nyingi lakini baadhi ya barabara hizo zina usumbufu mkubwa hasa baada ya wakati wa mvua hazipitiki kirahisi, je, Tarura tumejipangaje na kwa namna gani zitakavyokuwa zinapitika muda wote,” amehoji Ridhiwani.

Pia ameishukuru Tarura jinsi wanavyojitahidi kujenga miundombinu ya barabara licha ya changamoto ya bajeti ndogo wanayotengewa.

Katika hatua nyingine, amehimiza maandalizi ya marekebisho na ujenzi wa barabara korofi zote zikiwamo zile za kata za Kimange, Miono, Mkange, Vigwaza, Ubena, Talawanda, Mandela, Mji wa Chalinze na maeneo mengine kutokana na shughuli za kimaendeleo na kuchangia uchumi katika halmashauri hiyo.

Pia alitamani kujua wamejipangaje kufungua baadhi ya barabara zitakazokuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Chalinze kufikia malengo.

Awali, Meneja wa Tarura-Chalinze, Mhandisi Enrico Shauri, ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na ushauri wote uliotolewa na Ridhiwani.

Shauri amesema changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni ufinyu wa bajeti unaosababisha ufanisi wa kazi zao kusuasua.

Amesema Tarura-Chalinze ina kilomita 679 ambazo ni nyingi kwa bejeti inayotengwa ya mfuko wa barabara ambayo ni Sh milioni 700.44.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha wa 2020/2021 wameshapewa Sh milioni 200 na nyingine zitaendelea kutolewa kwa awamu na utolewaji wa haraka wa fedha hizo ndiyo utawezesha kazi ikamilike mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles