31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

TACAIDS yaagizwa kuwawezesha Vijana

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kudhibiti maambukizi mapya ya VVU kwa kundi la vijana ambalo linachangia kwenye maambukizi mapya ya kitaifa kwa asilimia 40, na asilimia 80 yake ni vijana wa kike, Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imeagizwa kuwawezesha vijana katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU kwa kujikita kwenye nyanja zingine badala ya kujielekeza kwenye VVU na UKIMWI pekee.

Katibu Mkuu -Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji, Doroth Mwaluko(katikati)

Hayo yamelezwa leo Novemba 29, na Katibu Mkuu -Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, uratibu na uwekezaji, Doroth Mwaluko wakati alipokuwa akihitimisha kilele cha wiki ya kijiji cha vijana kilichokuwa kinafanyikia kwenye Viwanja vya Mandela Pasua Manispaa ya Moshi ambapo maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duaniani kitaifa yanaadhimishwa hapa.

Amesema kuwa, kwa kila siku nchini watu 200 wanapata maambukizi mapya ya VVU ambapo kati yao asilimia 40 ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 ,ambapo pia kati ya hao  asilimia 80 ya vijana  wa kike hivyo inahitajika juhudi mbadala kwa kuwawezesha vijana kiuchumi sambamba na elimu ya UKIMWI.

“TACAIDS mmekuwa mkiratibu masuala yote ya UKIMWI hapa nchini, nawaagiza katika kundi hili la vijana muwapatie fursa kwa kuwa kiungo katika kuwawezesha kupata elimu ya mikopo, mitaji na elimu ya ujasiriamali ili waweze kujitegemea wenyewe, hivyo itawawezesha kuwa na kipato chao wenyewe hawawezi kudanganyika kwa minajili ya pesa,” amesema Mwaluko.

Ametumia nafasi hiyo pia kuziagiza asasi zote hapa nchini zinazoshughulika na masuala ya UKIMWI kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi hatua ambayo itawawezesha kupunguza maambukizi mapya kwa vijana kwa kuweza kujitegemea kiuchumi hivyo kupunguza vishawishi.

“Novemba 20, ya mwaka huu nilizungumza na vijana kupitia vyombo vya habari nilielezea hali ya maambukizi mapya ya VVU kwa vijana ambapo baada ya vijana kusikia kuwa vijana wa kike wanachangia asilimia 80 ya maambukizi mapya ya kila siku wengi walinitumia ujumbe kuwa nisiwatishe na mimi naendelea kuwatisha hali si nzuri kwa vijana,” amesema Mwaluko.

Amebainisha kuwa watanzania wanakadiriwa kuwa milioni 60 ambapo asilimia 68 ni vijana ambapo pia kwa mujibu wa sera ya Taifa ya vijana, sera inawatambua vijana ni wale wenye umri wa miaka 15-35 hivyo maambukizi kwa vijana ni zaidi ya asilimia 50.

Sambamba na hilo ameagiza TACAIDS kufika maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na msanii, Masanja Mchekeshaji kutoa elimu ya UKIMWI kwa vijana wa maeneo ya vijijini  haraka iwezekanavyo ili na wao waweze kupata elimu ya UKIMWI  hatua ambayo itawawezesha kuchukua hatua.

Aidha, aliwataka wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kutumia fursa hiyo katika kutembelea maadhimisho hayo ili waweze kupata elimu ya VVU na UKIMWI, kupima afya zao ushauri nasaha akiwasisitiza kwa wingi wao kushiriki kilele cha maadhimisho hayo Desemba mosi, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi.

Awali, akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Lonard Maboko amesema kijiji cha Vijana ambacho hufanyika kila mwaka kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani kikilenga kuwafikia vijana, kuwapatia elimu ya VVU na UKIMWI, ushauri nasaha kuzungumza nao na kuwaelezea mwitikio wa maambukizi ya UKIMWI umekuwa na manufaa makubwa katika kutekeleza afua za UKIMWI kwa vijana.

“Mwaka 2017, Waziri Mkuu alituagiza TACAIDS tuhakikishe tunawatafuta na kuwafikia vijana kwa kutumia majukwaa ya Sanaa na ndipo tulipoanzisha Kijiji cha Vijana ambapo huu ni mwaka wa tatu kila maadhimisho tumekuwa na kijiji kwa muda  wa wiki nzima vijana wa mkoa huu na mikoa ya jirani imepata fursa ya kujua mwitikio wa hali ya maambukizi ya VVU hapa nchini kwa vijana,” amesema Dk. Maboko.

Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Lonard Maboko

Amesema, TACAIDS kuanzia mwaka 2017 imekuwa ikijikita kwenye majukwaa mbalimbali ya vijana kama Tigo Fiesta, Wasafi Festival, pamoja na Bongo Star Search ambayo kwa mwaka huu bado inaendelea na TACAIDS tunashiriki katika kutoa elimu mbalimbali za vijana na mwitikio umekuwa mkubwa zaidi ya milioni moja tumewafikia, amesema.

Ametumia fursa hiyo kuwasihi wanaume kujitokeza katika kupima afya zao kwa kuwa kundi la wanaume ndilo liko nyuma katika tisini zote tatu hivyo kurudisha nyuma mpango wa Taifa wa kuhakikisha unadhibiti maambukizi mapya ya VVU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles