26.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Reli mpya kujengwa Dar es salaam

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), linatarajia kujenga reli mpya katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari.

Mradi huo ambao uko katika hatua za usanifu utaenda sambamba na ule wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na uboreshaji reli ya kati.

Akizungumza jana, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alisema kutokana na ongezeko la idadi ya watu katika jiji hilo usafiri wa reli ndio njia pekee inayoweza kuchukua watu wengi na kuondoa msongamano.

“Kwa Jiji la Dar es Salaam lilivyo mwaka 2030 idadi ya watu inaweza kuwa mara mbili ya ilivyo sasa, huwezi kuwahudumia kwa kutumia mabasi tu usafiri pekee unaofaa na kwa wakati ni reli,” alisema Kadogosa.

Alisema reli hizo mpya zitahusisha usafiri wa kutoka Dar es Salaam – Bagamoyo, Dar es Dalaam – Mbagala na Dar es Salaam – Uwanja wa Ndege.

Alisema hivi sasa wanafanya upembuzi yakinifu na kwamba kutakuwa na timu ya wataalam itakayohusisha vyombo vyote kuhakikisha suala hilo linasimamiwa kwa umakini.

“Kuna watu wamevamia maeneo ya reli, walijaribu kitafuta hati hawajapewa lakini kwa sababu ya ukaidi wamejenga, sasa ambaye amejenga maeneo ya reli aondoke na chochote kitakachofanyika kitakuwa ndani ya sheria,” alisema.

Katika hatua nyingine alisema wameanza kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote inakopita reli ya kisasa (SGR) ili kuzuia uvamizi.

“Tumeanza ‘ku – design’ njia yote kuanzia Dar es Salaam na kandokando ya reli kutakuwa na maeneo yatakayojulikana shughuli zake,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuelekea katika uchumi wa kati reli hiyo ni fursa kubwa katika uchumi wa viwanda na biashara ya bandari na kuwataka wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema pia reli ya kisasa itawekwa uzio ili kuepusha mdhara kwa sababu itakuwa na mwendo mkali.

Kuhusu ukarabati unaoendelea katika reli ya zamani, alisema umefikia katika hatua nzuri na kwa ile ya Tanga – Arusha walishapita Mombo na hivi sasa wamefikia katika eneo la Same.

“Reli ya zamani bado ni muhimu kwa sababu hata sasa ndiyo inayotumika kusafirisha vifaa vya ujenzi wa SGR na wananchi wanaitegemea. Na reli zote zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja kama ilivyo katika nchi zingine,” alisema Kadogosa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,509FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles