24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rc Mwanza aiagiza Sengerema kutatua changamoto ya afya kwa wananchi

Na Clara Matimo, Sengerema

Vijiji 16 kati ya 71 vilivyopo Halmashauri  ya Wilaya ya  Sengerema Mkoani Mwanza  havina zahanati kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi hivyo kuleta usumbufu wanapohitaji huduma hiyo ambapo hulazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kuifuata

Hayo yamebainika Juni 24, mwaka huu kwenye Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani  uliolenga kujadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameiagiza halmashauri hiyo  kujenga zahanati katika vijiji hivyo  ili kuwasogezea huduma ya matibabu wananchi kwa kuwashirikisha wenyewe pamoja na wadau wengine wa maendeleo badala ya kusubiri serikali.

Alisema changamoto haziondoki kwa njia ya maombi bali kwa juhudi , maarifa na ubunifu wa viongozi kwa kuwashirikisha wananchi kwani kuna miradi mingi ambayo inatekelezwa kila mwaka inayohusisha nguvu za jamii na wananchi hivyo waone namna ya kushirikishana.

“Kuna viongozi wa aina mbili, anayesubiri fedha zije ndiyo ashughulikie changamoto iliyopo  na kiongozi halisi ni yule anayetumia mbinu zake ikiwemo ubunifu ili kuleta mabadiliko na mageuzi kwenye eneo lake mbinu ziko nyingi hata kwa kutumia harambee naomba shirikianeni wataalamu na madiwani sababu wote kwa pamoja ni mapacha wasiogawanyika,”alisema na kuongeza

“Sisi tumebarikiwa rasilimali nyingi sana  tuna ardhi, mchanga, mawe, watu na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi ambacho ni chama kinachotekeleza ilani yake,  wekeni utaratibu mzuri wa kuwahusisha wananchi na wadau wote wa maendeleo hivyo tuweke lengo la kupiga mshale kwenye jua usipofika utaishia kwenye mwezi lakini itaonekana kuna mshale huko juu umerushwa na shujaa ambaye ni ninyi.

 “Miradi mnayoisimamia wataalamu waheshimiwa madiwani, mbunge na mheshimiwa rais waliahidi kwa wananchi wakati wakiwaomba kura  kwa hiyo sisi kutotekeleza ahadi hizo za waheshimiwa ni kutotendea haki Chama Cha Mapinduzi, madiwani, mbunge na mheshimiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wekeni mipango ya kujenga zahanati hizo inawezekana kwa kushirikiana,”alisema.

 Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje (CAG) Mkoa wa Mwanza, Waziri  Shabani, alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilipata hati yenye shaka huku akitaja sababu kubwa ya hoja kutokufungwa au kutekelezwa kikamilifu kuwa ni pamoja na majibu ya menejimenti kukosa vielelezo na ushahidi wa kutosha pia uongozi wa  kutokuweka mikakati ya dhati ya kujibu hoja kikamilifu.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike, aliitaka menejimenti kuzingatia sheria katika matumizi ya fedha za jimbo ili kuepuka CAG kuibua hoja.

“Bora tukuhukumu kwamba mkurugenzi yule anasimamia sheria, kanuni na taratibu zitakulinda hivyo zingatieni sheria msije mkapitisha fedha hovyo hovyo bila kufuata taratibu za kisheria na kikanuni  mkipitisha bila kufuata hiyo misingi kwanza mnaibua hoja mjitahidi kuweka nguvu kwenye kuzuia hoja,”alisema Samike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles