24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Wazazi simameni kwenye nafasi zenu kudhibiti mienendo mibovu ya watoto

Na Samwel Mwanga, Simiyu

Mabadiliko ya mazingira na nyakati katika jamii yanasababisha wazazi wengi kukosa muda wa kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao.

Kwa hali ya sasa kazi kubwa ya malezi ya watoto inafanywa na wasaidizi wakazi na hii inasababisha mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii.

Kwa sasa katika jamii yetu kumekuwa na ripoti nyingi za kuongezeka kwa matukio ya ukatili, unyanyasaji na mauaji kwa watoto yanayosababishwa na tatizo la wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto wao.

Wasaidizi wa kazi nyumbani ndiyo kwasasa wamepewa jukumu kubwa la malezi ya watoto hao ndiyo wanamhudumia kwa muda wote wanapokuwa nao wengine kuanzia nyakati za asubuhi hadi usiku.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, mwaka huu wilayani humo katika kijiji cha Kadoto aliwaomba wazazi kutenga muda wa kuwa na watoto nyumbani kwa ajili ya malezi yao tangu wakiwa na umri mdogo.

“Wazazi tunapaswa kutenga muda wa kuwa na watoto tangu wakiwa na umri mdogo na kuwafanya marafiki zetu itawasaidia kuwa na ujasiri wa kueleza changamoto wanazopitia wakiwa shuleni au nyumbani.

“Tuwalee watoto katika uwazi, tusiache jukumu laalezi ya watoto kwa wasichana wa kazi, bibi au shangazi, tusimame kama wazazi katika nafasi zetu, uwazi ndiyo utamwezesha mtoto kumueleza mwalimu jambo lolote hata ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa na jamii inayomzunguka,” anasema Kaminyonge.

Anasema kuna umuhimu mkubwa kwa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao tangu wakiwa na umri mdogo.

Anafafanua zaidi kuwa ushiriki hafifu wa malezi kwa wazazi umesababisha watoto kukua katika tabia na mienendo isiyofaa.

“Tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa jamii na nchi ambazo uchumi unakua kwa kasi kama ilivyo nchi yetu Tanzania” anasema Kaminyonge.

Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Binza wilayani humo, Joseph Mgeta anasema kuwa wanapokea wanafunzi ambao kitabia wako tofauti na muonekano wa wazazi wao kutokana na kutopata malezi kutoka kwa wazazi.

“Sisi walimu tunaowapokea watoto hapa shuleni ukiangalia kitabia na mienendo tofauti na muonekano wa wazazi na hali hii inasababishwa na jukumu la malezi ya watoto hao kuwa juu ya wafanyakazi wa ndani, hivyo kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na wazazi kuhakikisha kiuwa wanatenga muda kwa ajili ya kuangalia watoto wao ili waishi na kukua kwenye mstari ulionyooka,” anasema Mgeta.

Aidha, anaongeza kuwa hata wanapokuwa wanafanya makosa shuleni ya mara kwa mara kujirudia na unapowaita wazazi wao ili kuwaeleza makosa waliyofanya naye anashangaa lakini ukifuatilia kwa undani zaidi utakuta muda mrefu walilelewa na wafanyakazi wa ndani kutokana na wazazi kuwa na majukumu ya kazi.

Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Maswa, Basila Bruno anasema pamoja na wazazi kuwa na majukumu ya kazi kwa ajili ya kuendesha familia lakini kisiwe kigezo cha kuacha kuwapatia malezi watoto wao na kuwaachia wafanyakazi wa ndani.

Anasema ni vizuriwazazi wakatenga muda kwa ajili ya malezi ya watoto wao na kupata taarifa mbalimbali za malezi juu ya watoto wao pindi wanapowaachia wafanyakazi wa ndani na wengi wao huwa na umri mdogo hivyo suala la malezi ya watoto wengine huwa ni kitu kigeni.

“Hata sisi wazazi kama tuna majukumu yetu lakini tutambue ya kuwa suala la malezi ya watoto wetu liko mikononi mwetu, tusiwaachie wasaidizi wetu wa shughuli za ndani maana hilo si jukumu lao na ukizingatia wengi wao umri wao ni mdogo hivyo hata malezi ya watoto hawayajui,”anasema Bruno.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles