22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Rasimu ya usalama wa mitandao yaja Oktoba

Profesa Faustin Kamuzora
Profesa Faustin Kamuzora

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

SERIKALI inakusudia kukamilisha Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mitandao mwezi Oktoba, mwaka huu ambayo ni utekelezaji wa Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ya mwaka 2016.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustin Kamuzora, katika hotuba yake ya kufunga kongamano la wiki moja la wadau wa usalama wa mitandao lililofanyika Dar es Salaam.

Alisema kukamilika kwa rasimu hiyo ni moja ya hatua za kuweka mazingira salama ya mitandao.

“Serikali inajitahidi kuweka mazingira salama ya mitandao na kwa wiki moja tumewakutanisha wadau wa mitandao kujadili mambo muhimu ya kuweka kwenye Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mitandao ambao utakamilika Oktoba mwaka huu,” alisema Prof. Kamuzora.

Alisema suala la usalama wa mitandao haliishi katika teknolojia bali linahusu pia utamaduni wa watu kuitumia vizuri hivyo ni muhimu elimu ya usalama wa mitandao kutolewa kwa watumiaji.

Alisisitiza kuwa changamoto za mitandao ikiwemo uhalifu wa mitandao ni fursa za ajira pamoja na uwekezaji katika kutafuta mbinu za kukabiliana nazo.

“Tafiti zinaonyesha kwa mwaka jana duniani kote kulikuwa na upotevu wa dola za Marekani bilioni 400 uliosababishwa na uhalifu wa mitandao lakini pia utafiti huo unaonyesha kwa miaka ijayo mataifa yatawekeza zaidi ya dola bilioni 650 kukabiliana na uhalifu huo.

“Hivyo tunaweza kuona kuwa uwepo wa changamoto ndio unaoleta fursa hivyo kama Serikali na watu binafsi tunatakiwa kuwekeza katika kutoa elimu ya masuala haya kwa vijana wetu ili wapate ajira za kupambana na uhalifu huu,” alisema Prof. Kamuzora.

Alisema Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia (NFAST), itasaidia kuwajengea uwezo Watanzania katika kushughulikia changamoto za usalama wa mitandao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles