28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS AMTUHUMU MAKAMU WAKE KUWA FISADI ECUADOR

QUITO, ECUADOR

RAIS wa Ecuador, Lenin Moreno, ametangaza kumwondolea majukumu ya kiofisi makamu wake, Jorge Glas kwa kile alichosema amekuwa mzigo mkubwa wa aibu kwa Serikali.

Hata hivyo, kwa sababu za kikatiba amesita kutangaza kumfukuza msaidizi wake huyo, ambaye walichaguliwa pamoja kuingia madarakani Mei 24 mwaka huu.

Rais huyo alisema makamu wake amekuwa chanzo cha kila aina ya hisia mbovu katika taifa hilo na pia kwa washirika wa maendeleo kutokana na kuandamwa na tuhuma za ufisadi.

Katika taarifa rasmi ya Serikali, Rais Moreno allisema kuwa alikuwa akimwondolea majukumu yote rasmi, ambayo hutekelezwa na ofisi yake kwa mujibu wa maelekezo ya ofisi ya rais.

Glas, ambaye ameitumikia nafasi ya umakamu wa rais tangu 2013, amekuwa akihusishwa na ufisadi kutoka kwa upinzani, ikiwamo tuhuma za kuhusika na kashfa ya hongo zinazoikabili kampuni kubwa ya mafuta ya Brazil, Odebrecht, ambazo zimetikisa eneo hilo.

Uamuzi huo wa Rais Moreno ulikuja baada ya Glas kutoa mlolongo wa shutuma dhidi ya kiongozi huyo mpya wa mrengo wa kushoto.

Glas ambaye alishikilia wadhifa huo wakati wa utawala wa mtangulizi wa Moreno, Rafael Correa, alichapisha orodha ndefu ya tuhuma dhidi ya Moreno, ikiwamo madai kuwa alikabidhi vyombo vya habari vya umma kwa wawakilishi wa vyombo binafsi na amekuwa na mbinu haramu za kushughulisha takwimu za kiuchumi.

Moja ya majukumu aliyoondolewa Glas ni usimamizi wa mradi wa mabilioni ya dola wa ujenzi wa nyumba zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi lililoua watu 600 mwaka 2016.

Hata hivyo, taarifa zinasema Glas alitoa shutuma baada ya kupata dokezo kuwa Moreno amepatiwa taarifa za siri zinazomhusisha na hongo kutoka kwa makandarasi wa miradi ya Serikali.

Glas amekuwa akikana kuhusika na ufisadi serikalini na badala yake akitaka Moreno awajibike kwa ukosefu wa imani na Serikali yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles