25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

RAILA ODINGA AOMBA MSAADA KWA SERIKALI YA ULAYA

NAIROBI, KENYA

MUUNGANO wa vyama vya upinzani nchini Kenya, National Super Alliance (NASA) umeandikia rasmi barua kwa Serikali ya Ufaransa kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8 na baadaye matokeo ya urais kufutwa na Mahakama ya Juu kutokana na dosari mbalimbali, zikiwamo kukosa uhuru na haki, huku ukisisitiza kuomba msaada zaidi katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 17.

NASA uliihimiza Serikali ya Ufaransa kuchunguza shirika la teknolojia ya mawasiliano la Safran na maofisa wake kwa madai ya kuwa kikwazo cha demokrasia nchini Kenya, kutokana na kile walichokiita kufanya uhalifu na kuingilia uchaguzi uliopita.

Muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga, kupitia barua iliyoelekezwa kwa maofisa wakuu wanne wa Ufaransa, ikiwamo Waziri wa Usalama, Balozi wa Ufaransa Kenya, Waziri wa Masuala ya Kigeni na Waziri wa Haki, uliihimiza Serikali ya Ufaransa kuanzisha uchunguzi katika kampuni ya Safran na maofisa wake kwa madai ya kuingilia demokrasia nchini Kenya.

Habari kuhusu barua hiyo zilisambazwa mtandaoni mara ya kwanza na mwanasiasa sugu wa NASA, Junet Mohammed. Taarifa zinasema kuwa, kampuni mbili za mifumo ya teknolojia ya habari kutoka Ufaransa, Safran na OT-Morpho, zilitoa huduma zao kwa Tume Huru na Mipaka ya Uchaguzi (IEBC) wakati wa uchaguzi wa awali.

Hata hivyo, NASA imetofautiana na kampuni hizo, ikidai kuwa yalisaidia chama cha Jubilee kuiba kura katika uchaguzi kwa kuingilia mitambo ya tume hiyo.

Hata hivyo, taarifa ya kampuni hizo imesema kuwa, kazi yao ni kusimamia mitambo ya IEBC na hivyo shutuma nyingine zinapaswa kupuuzwa kuwa mitambo hiyo iliingiliwa. Uchaguzi wa marudio unatarajiwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu.

TUME YATOA RATIBA MPYA

Katika hatua nyingine, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imetoa ratiba mpya iliyorekebishwa kabla ya uchaguzi wa marudio wa urais ifikapo Oktoba 17, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Wafula Chebukati, inasheheni mfumo wa matokeo ya uchaguzi yaliyorekebishwa, uidhinishaji wa usajili wa wapiga kura na teknolojia iliyoboreshwa pamoja na uteuzi na mafunzo ya maofisa wa uchaguzi, uhamasishaji wa wapiga kura na maandalizi ya siku ya uchaguzi.

Zikiwa zimesalia siku 37 pekee kabla ya uchaguzi, tume ya uchaguzi tayari imewasilisha bajeti yake kwa Hazina ya Kitaifa, ikiwataka wadau husika kutoa fedha zinazohitajika haraka ili kukamilisha zoezi la uandaaji wa uchaguzi huo. Suala kuu litakalozingatiwa na IEBC ni mafunzo ya ICT.

Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kubaini kuwa, usambazaji wa matokeo katika uchaguzi Agosti 8 haukutekelezwa ipasavyo, na baadhi ya maofisa wa hawakuzingatia masharti yaliyokuwapo. Ni muhimu kwa wagombea pia kuwatumia maajenti wenye tajiriba na waliojitolea katika maeneo yote nchini ili kuimarisha uwajibikaji na uwazi wakati wa mchakato wa uchaguzi.

“Matokeo yetu ya awali yalifichua kuwa vyama vya kisiasa havikudhibiti maajenti wao na katika baadhi ya sehemu, hakukuwa na maajenti wowote,” alisema Chebukati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,454FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles