24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Raila afuata nyayo za Uhuru kukataa siasa za 2022

NA ISIJI DOMINICSIKU chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema chaguo la mrithi wake litawashangaza wengi na kwamba kwa sasa hataki wanasiasa kupiga siasa mbali kutumikia wananchi, kinara wa upinzani, Raila Odinga, naye ametoa kauli yenye mwelekeo huo huo.

Rais Uhuru akiwa kaunti ya Nyeri, aliwaambia wanasiasa kutoka sehemu hiyo kujadili miradi ya maendeleo inayogusa wananchi kuliko kufanya siasa kila mara wakati walipotaka kujua hatima yake baada ya 2022.

“Wengine wanafikiri nimenyamaza kwa sababu siwezi kuongea kuhusu siasa. Mimi bado ni mwanasiasa. Watashangaa chaguo langu muda huo utakapofika, lakini kwa sasa nataka nijihusishe na kutekeleza ahadi nilizotoa kwa Wakenya,” alisema.

Rais Uhuru wakati anaapishwa kuhudumu muhula wake wa pili, aliweka wazi ajenda nne kuu ambazo anataka kuzishughulikia ikiwamo kupambana na ufisadi ambayo alisema inarudisha nyuma uchumi wa nchi.

Ukimya wa Rais kuongea kuhusu siasa za 2022 ukizingatia bado miaka minne kufanyika uchaguzi mkuu mwingine na pia kitendo chake cha kushirikiana na Raila ambao kauli zao kwa siku za hivi karibuni zimekuwa zikishabihiana, kumewafanya wanasiasa wengi hususani kutoka chama tawala kuingiwa na wasiwasi huenda Uhuru akamuunga mkono Raila uchaguzi mkuu ujao.

Ushirikiano na Rais Uhuru na moja wa vinara wa NASA, Raila, umesababisha kiongozi huyo wa chama cha ODM kuteuliwa Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) atakayesimamia ujenzi wa miundombinu msingi barani Afrika jambo ambalo limewafanya baadhi ya wanasiasa kutoka Jubilee na hata NASA kumtaka kustaafu siasa za Kenya na kutumikia majukumu yake mapya.

Raila ambaye hajaweka wazi kama atawania urais kwa mara nyingine tena mwaka 2022, hivi karibuni akiwa kaunti ya Siaya, alikaririwa akisema ataendelea na siasa za ndani huku akifanya kazi zake za AU na kuahidi wafuasi wake hakuna kitu kitakachomtenganisha.

“Siendi popote. Uteuzi wangu mpya kama balozi wa AU umekuja na ofisi jijini Nairobi. Nitakuwa nasafiri kwenda Ethiopia, Afrika Kusini na mataifa mengine Afrika kwa kazi na kisha kurudi ofisini Nairobi ambapo kuna ofisi yangu kuu,” alisema.

Lakini katika hali ambayo inaonesha kuipa kisogo siasa za 2022 na kushughulikia majukumu yake ya AU, taarifa ya Raila kupitia msemaji wake, Dennis Onyango, ilisema kazi yake mpya haiwezi kumruhusu kujihusisha na siasa za uchaguzi mkuu ujao.

“Ili kutoa mwongoza katika masuala nyeti yanayomkabili kwenye majukumu yake na pia matamko yaliyowahi kutolewa huko nyuma, Raila anapenda kusisitiza kutojihusisha na siasa za Kenya kuelekea 2022,” alisema Onyango na kuongeza kiongozi huyo wa ODM anataka kutumia miaka hii kadhaa kutengeneza msingi barani Afrika kupitia ofisi yake mpya.

Hii ni kauli ambayo inaweza kuzima japo kwa muda mjadala wa siasa za 2022 ukizingatia baadhi ya wanasiasa kutoka Jubilee wamekuwa wakimtaka Raila astaafu siasa za ndani huku wale wa kambi ya kinara wa upinzani wakisisitiza haendi kokote.

Tukio la kusalimiana Machi 9, mwaka huu kati ya Uhuru na Raila imebadili upepo wa namna wawili hao wanavyotumia siasa kuunganisha wananchi na kuhubiri maendeleo. Ni tukio ambalo pia linaanza kumbadili mawazo Naibu Rais William Ruto ambaye anaonekana yupo katika hali ya kukampeni akizunguka nchi nzima kujaribu kuungwa mkono.

Rais Uhuru amejitahidi kutojihusisha na kampeni za Ruto hadharani lakini Naibu Rais naye amekuwa akisisitiza anazunguka nchi nzima kama msaidizi wa Rais akizindua miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi.

Kitendo cha Raila kujiweka pembeni na siasa za 2022 huenda pia ikachochea Ruto na wafuasi wake kuacha kulumbana hadharani na wanasiasa wa upinzani na pia kufikiria nani atakayemrithi Uhuru.

Miradi mingi ya Serikali imetokana na hela za kukopa ambazo hazina budi kulipwa. Hilo litafanikishwa endapo wanasiasa watajishughulisha kutunga sheria zenye manufaa kwa wananchi na kuibana serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi zake.

Aidha kauli ya Raila kutojihusisha na siasa za 2022 ni tafsiri tosha kwa wanasiasa ndani ya ODM kuanza kufikiria nani anayeweza kuvaa viatu vyake na ambaye pia anaweza kuungwa mkono na Wakenya wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles