25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

PROF. NDALICHAKO ATOA ANGALIZO BILIONI 250/-

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ametoa angalizo la matumizi ya Dola za Marekani 120 sawa na Sh bilioni 250 zilizotengwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa elimu na ujuzi kwa kazi zenye tija (ESPJ).

Benki ya Dunia kupitia Mradi wa vituo vya ubora Tanzania, Afrika Mashariki na Kusini (ACE II), pia imetenga Dola za Marekani milioni 24 kwa ufadhili wa vituo vinne, ambapo vituo viwili vipo Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika juzi jijini hapa, Profesa Ndalichako alizitaka taasisi zitakazotekeleza miradi hiyo kuhakikisha zinakwenda na kasi ikiwamo kuwa makini katika matumizi ya fedha hizo muhimu kwa taifa.

Akifafanua kuhusu mradi wa elimu na ujuzi kwa ajili ya kazi zenye tija, Profesa Ndalichako alisema Serikali imepiga hatua ya maendeleo yaliyoainishwa kwenye mpango wake wa miaka mitano wa maendeleo 2016-2012 uliojikita katika ujenzi wa viwanda na kupanua viwanda muhimu.

“Kwa sasa asilimia 84 ya watu wana ujuzi mdogo, asilimia 13 ujuzi wa kati na asilimia tatu ujuzi wa juu. Ili kufikia hadhi ya taifa la kipato cha kati, kutahitajika mageuzi katika muundo wa sasa wa ujuzi wa watu kwenda asilimia 35 ya wenye ujuzi mdogo, asilimia 33 ujuzi wa kati na asilimia 12 ujuzi wa juu.

“Programu ya ESPJ iliyotengewa Dola za Marekani 120, itasaidia sehemu kubwa ya mkakati taifa wa kuendeleza ujuzi. Lengo lake likiwa ni kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa mfumo wa kuendeleza ujuzi na kukuza upanuzi na ubora wa fursa za maendeleo zinazosukumwa na soko la ajira,” alisema Profesa Ndalichako.

Alizitaja fursa zinazosukuma soko la ajira ni katika sekta za utalii na ukarimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na Nishati ambapo programu hiyo ilianza kufanya kazi Januari 2017 ikitekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

“Kuna wakati mwingine kumekuwa na urasimu, katika mradi huu nisingependa kuruhusu urasimu. Wote wanaohusika kwenye mradi huu wakae mkao wa kuwajibika ipasavyo.

“Haiwezekani Taifa likapoteza fursa ya kupata fedha zilizotengwa tayari kwa sababu ya urasimu wa mtu kushindwa kufanya uamuzi wa haraka. Sisi tutamfanyia huyo mtu uamuzi wa haraka ikiwamo kutafuta mwingine wa kusimama kwenye nafasi hiyo,” alisema Prof. Ndalichako.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Karoli Njau, alisema vituo viwili vilivyopo kwenye Taasisi yake vitatekeleza mradi wa utafiti, ubora katika ufundishaji na uendelevu katika chakula na lishe na mustakabali wa miundombinu ya maji na nishati endelevu (WISE).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles