28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

PPRA yaokoa Bilioni 16 kwenye zabuni 2021/22

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

KATIKA Mwaka wa Fedha 2021/22 na 2022/23, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefanikiwa kuokoa jumla ya fedha za umma kiasi cha Sh bilioni 16.27 katika zabuni mbalimbali zilizotekelezwa.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 13.83 ilitokana na kuingilia kati kwa Mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato (Disqualified).

Kiasi cha Sh bilioni 2.44 ni kiasi kilichorudishwa na wasambazaji wa bidhaa (Suppliers) na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na Taasisi Nunuzi.

Hayo yameelezwa leo Aprili 9,2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na Kujenga Uwezo, PPRA, Mhandisi Amini Mcharo, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu katika ununuzi wa umma.

Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6), Mamlaka ilifanya uchunguzi kwa zabuni zilizotekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22 na 2022/23, na kufanikiwa kuokoa jumla ya fedha za umma kiasi cha Sh bilioni 16.27.

Amesema kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh bilioni 13.83 ilitokana na kuingilia kati kwa Mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato (disqualified).

“Na kiasi cha Shilingi Bilioni 2.44 ni kiasi kilichorudishwa na wasambazaji wa bidhaa (suppliers) na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na Taasisi Nunuzi,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema Mamlaka imekuwa ikifanya kaguzi na uchunguzi mbalimbali na mapambano dhidi ya rushwa kwenye taasisi nunuzi.

“Lengo la kazi hii ni pamoja na kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na viashiria vya rushwa,” amesema.

Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, Mamlaka hutoa taarifa zake kwa taasisi nunuzi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita (6) chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan, umefanyika uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma unaojulikana kama National e-Procurement System of Tanzania (NeST).

“Kabla ya uwekezaji huu, ununuzi wa umma ulikuwa ukifanyika kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS) ambao ulijengwa na kampuni ya kigeni kutoka Ugiriki,” amesema Mkurugenzi huyo.

Amesema serikali ilibaini changamoto nyingi kwenye ununuzi uliokuwa ukifanyika kupitia mfumo wa TANePS ikiwemo taarifa zote za Ununuzi wa umma kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni nje ya nchi.

“Changamoto hii na nyinginezo zilipelekea uamuzi wa kuanzisha mfumo mbadala ambao utakuwa bora zaidi, wenye kuleta tija, unaojengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na serikali,” amesema Mkurugenzi huyo.

Amesema PPRA ina dhamana ya kusimamia sekta ya ununuzi wa umma kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa thamani ya fedha kwenye ununuzi na ugavi.

Pia, kuhakikisha uzingatiaji wa haki, ushindani, uwazi na kufuatilia uzingatiaji wa sheria kwa taasisi za umma, pamoja na kujenga uwezo katika Ununuzi wa umma kwa kushirikiana na wadau.

Pia, Mamlaka ina dhamana ya kuhakikisha Taasisi nunuzi zinatoa upendeleo kwa wazabuni wa ndani katika zabuni za bidhaa, kazi za ujenzi na huduma. Utekelezaji wa malengo ya uanzishwaji wa PPRA umelenga katika kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Amesema katika kufikia malengo ya uanzishwaji wake, PPRA imeendelea kuandaa mipango na bajeti zake kwa kuzingatia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango Mkakati wa PPRA (2021/22 -2025/26).

Pamoja na makubaliano mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda yenye lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa fursa za ununuzi na ugavi wa umma kwa wazabuni wote wenye nia ya kufanya biashara na serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles