28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

POSTA NAO KUNUNUA NDEGE

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM                        |                               


SHIRIKA la Posta Nchini lipo katika mchakato wa kununua ndege kwa ajili ya kusambaza vifurushi na huduma nyingine ili kurahisisha huduma kwa wateja wao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe, alisema ununuzi wa ndege hiyo unatokana na mafanikio yaliyopatikana tangu bodi iteuliwe mwaka 2016.

Alisema mchakato wa ukamilishwaji wa ndege hiyo unaendelea na kwamba utawapunguzia muda wateja kupata mizigo yao pindi inapotumwa kupitia shirika hilo.

Katika hatua nyingine, alisema kutokana na kukua kwa teknolojia, shirika hilo limeanzisha duka la mtandaoni, ambalo tayari lina wateja kutoka duniani kote.

Alisema tayari wameunganisha ofisi 125 za posta kwenye mfumo wa kutolea huduma kielektroniki unaojulikana kama Postglobal netsmart na mpango wa kuunganisha nyingine 27 utakamilika mwishoni mwa Septemba, mwaka huu.

“Maboresho na mifumo hiyo ya mawasiliano inalenga kuboresha huduma ya biashara mtandao nchini na nje ya nchi na kuwafanya wateja wa shirika hilo kufurahia huduma zetu’’.

Aliongeza kuwa, wamefanikiwa kuboresha huduma za kisasa katika ukanda wa Afrika kwenye kufikisha huduma kwa wateja,  hasa maeneo korofi kwa kutumia ndege zisizo na dereva zijulikanazo kama ‘drones’.

Naye Mwenyekiti wa bodi wa Shirika hilo, Dk. Haroun Kondo, alisema tangu bodi yake iteuliwe wameweza kuzalisha faida.

Dk. Kondo alisema kutokana na hilo, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 walitoa gawio la Sh milioni 250 kwa Serikali, huku mwaka huo wa fedha 2017/2018 wanatarajia kutoa gawio la zaidi Sh bilioni moja.

Dk. Kondo alisema hilo limetokana na jitihada za Bodi na Menejimenti ya Shirika katika kulifanya lijiendeshe kwa faida tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ambapo lilikuwa likizalisha hasara tu.

Amesema lengo lao kuanzia sasa ni kuchangia pato la taifa kwa kutoka gawio la kuanzia Sh bilioni na kuendelea, kwa madai kuwa shirika lina uwezo huo kupitia rasilimali ilizo nazo, ikiwamo majengo na viwanja wanavyovimiliki.

Alisema katika mafanikio hayo alipitia changamoto mbalimbali, kama Mwenyekiti, ikiwamo kulalamikiwa kuwa mbabe kwa kuwaondoa baadhi ya wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kulisababishia shirika hasara na kufikishwa katika vyombo mbalimbali, lakini hakujali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles