24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi waua majambazi wawili wakati wa kurushiana risasi

Na JANETH MUSHI – ARUSHA

 WATU wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi, wameuawa wakati wa majibizano ya risasi na polisi, baada ya kuwekewa mtego.

Jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine watatu waliokimbia.

Katika tukio hilo, pia zilipatikana silaha mbili ambazo ni shotgun iliyokuwa na risasi tisa na bastola aina ya Bereta iliyokuwa na risasi nne ndani ya magazine.

Akitoa taarifa ya kuuawa kwa watuhumiwa hao jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 18 mwaka huu saa 7:10 eneo la Olkerian, Kata ya Moshono.

Aliwataja waliouawa ni Bashiri Ally maarufu Shehe (45), mkazi wa Kimara, Dar es Salaam na mwingine aliyefahamika kwa jina la Mohamed.

Alisema kuuawa kwa watuhumiwa hao, ni mwendelezo wa upelelezi na ufuatiliaji wa matukio mbalimbali ya ujambazi yaliyotokea mkoani hapa.

Alidai tukio mojawapo ni lililotokea Septemba 26, mwaka huu eneo la Kijenge, ambako mtu mmoja aliyetambulika kwa sura na kukadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 na 40, aliuawa baada ya kupigwa risasi akiwa na wenzake wanne wakati walipomvamia mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa).

“Walimvamia mfanyabiashara huyo kwa lengo la kumpora pesa alizokuwa nazo na baada ya tukio hilo wenzake walikimbia na kutelekeza pikipiki moja na simu,” alidai Kamanda Hamduni.

Alisema upelelezi na ufuatiliaji wa tukio hilo uliendelea na kubaini mmoja wa watuhumiwa (Ally) alikimbilia Dar es Salaam na kufanikiwa kumkamata.

Ally anadaiwa kukiri kuhusika na tukio hilo la Kijenge na kuwataja wenzake ambao wapo Arusha.

“Mbali na kuwataja wenzake, alitaja silaha walizokuwa wanatumia na kuahidi kutoa ushirikiano kwa polisi kuonyesha sehemu walipo pamoja na silaha hizo.

“Jeshi la Polisi liliweka mtego kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa wengine ambapo Ally aliwasiliana na wenzake bila wao kujua ni mtego, walijua ni mipango ya kwenda kufanya ujambazi na walikubaliana wakutane eneo la Olkerian.

“Baada ya kufika eneo hilo, mtuhumiwa alipewa uhuru wa kwenda kuonana na wenzake wasije wakashtuka kama ameambatana na polisi, ila alipowakaribia alianza kupiga kelele za kutoa ishara ya uwepo wa polisi eneo hilo na polisi walifyatua risasi juu kumuonya asikimbie.

“Badala yake aliendelea kukimbia na washirika wenzake walianza kujibizana risasi na polisi hali iliyopelekea Ally na mwenzake kujeruhiwa na kufariki wakiwa njiani wanapelekwa hospitali,” alisema Kamanda Hamduni.

Alisema wakati watuhumiwa hao wanapelekwa hospitali, Mohamed alihojiwa kabla ya mauti kumkuta na kutaja majina ya wenzake waliotoroka na kueleza kuwa walikuwa na silaha mbili, moja aina ya shotgun na nyingine aina ya pistol ambayo alidai alikuwa anaitumia na aliiangusha eneo la tukio.

“Kwa kuwa kulikuwa na giza kali na ukizingatia silaha aina ya bastola ni ndogo, upekuzi wa eneo hilo ulifanyika tena Oktoba 18 kwa kushirikiana na wananchi ambapo bastola hiyo isiyo na namba ilipatikana,” alisema Kamanda Hamduni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles