26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Daktari ataja sababu tatizo kukosa usingizi

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya ubongo, mfumo wa fahamu na mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk. Laurent Lemery amesema matumizi ya simu wakati wa kulala na msongo wa mawazo huweza kusababisha tatizo la usingizi.

Akizungumza na MTANZANIA wakati wa mahojiano maalumu Dar es Salaam jana, Dk. Lemery alisema sababu nyingine ya matatizo ya usingizi ni mazingira duni ya kulala.

 “Matumizi ya simu inaweza kuwa sababu mojawapo ya mtu kutokulala muda ambao ameupanga, utakuta mtu anapitiwa kutokana na ‘kuchati’ muda mrefu na kuathiri muda wa usingizi, hivyo ni bora mtu anapolala anaweka simu mbali ili kulala kwa wakati.

“Vitu vingine mfano kutumia kompyuta mpakato kitandani, unataka upate usingizi itakuwa sio rahisi au kuangalia luninga, ukiwa kitandani na unaangali mpira lakini unajua kuwa unatakiwa kulala, hilo linaweza kuwa tatizo la kutokulala kwa muda unaotakiwa.

“Tatizo la mawazo (cycological stress) linaweza kusababishwa na kazi unazofanya au hata mahusiano, vinaweza vikawa kwa njia moja au nyingine zinaathari katika mfumo wa mawazo, kwahiyo mtu anakosa usingizi.

 “Unalala kwenye watu wengi, wakati wewe unapata usingizi wao ndiyo kwanza wanaanza kupiga kelele au  wanaanza kufanya shughuli zingine, haya ni mazingira duni, lakini pia taa zenye mwanga mkali, au unalala kwenye jua, kuna mwanga huwezi kupata usingizi,” alisema Dk. Lemery.

Alisema usafi wa chumba unacholala na nguo unazotumia zikiwa hazina usafi zinaweza kuchangia kutokupata usingizi wa kutosha.

Dk. Lemery alisema kutokuwa na ratiba maalumu ya kulala huweza kuwa sababu za kutokupata usingizi wa kutosha.

“Kama muda wako wa kulala ni saa tatu au nne usiku, lazima wakati huo  uwe umepanda kitandani, hii mara nyingi inakuwa ni tatizo kubwa na inasababisha watu kutokupata usingizi,” alisema Dk. Lemery.

Alisema ufanyaji mazoezi muda mfupi kabla ya kulala humfanya mtu kushindwa kupata usingizi kutokana na mfumo wa usingizi kuathiriwa.

Dk. Lemery alisema lazima wakati wa jioni watu kukwepa matumizi ya vyakula au vinywaji ambavyo vinachangamsha mwili.

“Mfano unakunywa kahawa nyingi halafu unataka kupata usingizi, inaweza kuleta shida, asilimia 90 ya watu wakinywa kahawa mapigo ya moyo yanaenda mbio, wanatoa jasho na wanakuwa wako macho kwa muda mrefu, basi hii kahawa na vyakula vya ‘kafeni’ viepukwe wakati unakwenda kulala,” alisema Dk. Lemery.

Alisema wakati mtu akiwa amelala, mifumo ya mwili kama ubongo, mifumo ya fahamu, mifumo ya upumuaji, mifumo ya moyo na usukumaji wa damu, mifumo ya chakula, haja kubwa, mkojo, mifupa, misuli na mifumo ya kinga ya mwili   huanza kujiandaa kwa siku nyingine.

Kwa mujibu wa Dk. Lemery, usingizi kwenye mfumo wa fahamu husaidia kutunza kumbukumbu vizuri na kuboresha umakini.

“Mifumo ya mwili inajitengeneza na kujiweka vizuri kwa ajili ya kuanza siku nyingine na kuwezesha mwili kufanya vile inavyotakiwa,” alisema Dk. Lemery.

Alisema kwa wakati huo mifumo ya kinga mwili  inapata muda wa kujiweka sawa kwani kipindi hicho sumu zinaondolewa mwilini na kingamwili kutengenezwa. 

 “Mfumo wa kinga unapata muda mzuri wa kuweza kujiandaa kwa ajili ya kulinda mwili, kwahiyo unaona wakati huo mifumo yote inajiweka tayari kwa ajili ya kujisafisha na kuanza kazi mpya siku inayofuatia,” alisema Dk. Lemery.

Alisema baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba watoto wakilala wanaongeza homoni za ukuaji.

“Hii inazalishwa kwa kiwango kikubwa kipindi wakiwa wamelala kwenye usingizi mzito na hii inasaidia watoto kukua vizuri katika kimo na uzito ukilinganisha na watoto kulala masaa machache, chini ya saa sita.

 “Kwa watoto ambao wanasoma shule, kwa siku nzima wanakuwa wamesoma vitu vingi, vile vitu haviwezi kuwepo kama kumbukumbu kwa muda mfupi, inabidi wakati wakiwa wamelala muda wa kutosha ubongo unafanya kazi taratibu ya kuchukua zile kumbukumbu na kuziweka sehemu ambapo zinakaa kwa muda mrefu na inakuwa rahisi   kuzikumbuka,” alisema Dk. Lemery.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles