25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi watakiwa kutumia nguvu kulingana na tukio husika

Christina Gauluhanga- Dar es Salaam

KAMISHNA wa Opareshini na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Liberatus Sabasi, amewataka askari polisi nchini kutathimi utendaji kazi wao na kutumia nguvu kulingana na tukio lililopo.

Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya nne ya vyuo vinne vya polisi nchini ambapo maofisa wa jeshi hilo zaidi ya 300 wamehitimu kozi ngazi ya shahada na stashahada kwa mwaka wa masomo 2017/ 2018 na 2018/2019.

Sabasi alisema katika kuyakabili matukio mbalimbali ni vema kuangalia uzito wa tukio, jinsi ya kulikabili na kujihami.

“Ninawaagiza askari wangu katika kukabili matukio mbalimbali nguvu iendane na ukubwa au udogo wa tukio ili kuondoa malalamiko, nashauri kama kuna tukio  unalokabiliana nalo watuhumiwa wanaotumia bunduki nanyi tumieni bunduki lakini kama hakuna bunduki angalieni namna bora ya kudhibiti,”alisema Sabasi.

Sabasi alisema kwa sasa uhalifu umebadilika kwa sababu ya kukua kwa teknolojia hivyo ni vema kujifunza mbinu mpya kwa kuzingatia nchi si kisiwa.

Alisema polisi wanatakiwa hivi kujifunza mbinu mpya za kihalifu kupitia mitandao na kujiendeleza ili kufahamu teknolojia mbalimbali.

Pia aliwaagiza makamanda wa polisi nchini kuhakikisha wanawapanga polisi katika kazi kulingana na taaluma zao na kuacha ubaguzi wa kuwalundikia kazi baadhi ya watu.

Pia aliwataja polisi kutenda haki na kukemea rushwa kwa kuacha kushawishi au kuipokea.

Alisema ubambikiaji kesi wananchi unalitia doa jeshi hilo na hakuna haja ya kufanya hivyo kwakuwa jeshi hilo lina uwezo wa kufanya upelelezi na kubaini makosa.

“Matukio ya kubambikia kesi wananchi kama yapo acheni kwasababu uwezo wa kupeleleza kesi tunao, zingatieni weledi na utendaji kazi uliotukuka, na watakaokiuka maadili wachukuliwe hatua za kisheria”alisema Sabasi.

Naye, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Profesa Elifasi Bisanda, alilitaka jeshi hilo kujenga misingi imara ya utendaji kazi kuwa na wataalam waliobobea katika fani mbalimbali na kuwa kinara wa tafiti.

“Naomba jeshi la polisi libadilike kwani uwezo tunao ukiangalia mfano mdogo tu wa simu zilianza kutumika jeshini zaidi ya miaka 10 baadaye ndio wananchi wakaanza kuzimiliki hivyo tuna kila sababu ya kuwa wabunifu wa kucheza na teknolojia kwakuwa uwezo na mbinu tunazo,”alisema Bisanda.

Aliiomba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kufungua fursa kwa maofisa wake na kuondoa baadhi ya changamoto zinazojitokeza ili kufanyakazi kwa weledi wa hali ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles