26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bashungwa aiagiza WMA kupima mita za maji

Mwandishi Wetu-Dodoma

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ameiagiza Wakala wa Vipimo (WMA),  kuhakiki mita za maji ili matumizi sahihi ya vipimo yazingatiwe ili mamlaka na watumiaji waweze kunufaika bila kuwa na malalamiko upande wowote.

Aliyasema hayo jana mkoani Dodoma wakati WMA ikitoa taarifa ya utendaji kazi kwenye semina waliyoandaa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi kuhusu mita hizo hivyo ni vyema wakawatembelea wananchi  na kuwasikiliza ili kuondoa changamoto zinazowakabili.

“Serikali kwa sasa inatekeleza miradi mikubwa ya maji hivyo matumizi sahihi ya vipimo lazima yazingatiwe ili mamlaka na watumiaji wa maji wote wanufaike bila kuwa na malalamiko,” alisema Bashungwa.

Pia aliipongeza WMA, kwa utendaji mzuri na amewaagiza waendelee kujitangaza ili wafahamike zaidi na iwapo WMA itajitangaza wananchi wengi watafahamu faida za kuuza na kununua bidhaa kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Aliitaka WMA kufanyia kazi changamoto zilizotolewa  na wabunge wa kamati ya Viwanda na Biashara na kwenda mikoani kutoa elimu kwa umma ili wananchi wajue kazi za taasisi hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Dk. Ludovick Manege, alisema wamewapeleka katika mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi watumishi wake 49.

Alisema WMA kwa kutumia uwezo wake wa ndani imefanikiwa kununua vitendea kazi mbalimbali ikiwemo kompyuta 26, vifaa vya kitaalamu, mizani na mawe ya kupimia madini.

Aidha, alisema wakala umefanikiwa kujenga kituo kikubwa cha kupimia malori ya kubeba mafuta Misugusugu mkoani Pwani kinachotoa huduma kwa malori ya ndani na nje ya nchi.

Dk. Ludovick alisema kituo hicho kina uwezo wa kupima zaidi ya malori 60 kwa siku wakati kituo cha zamani kilikuwa na uwezo wa kupima magari nane tu kwa siku.

Alisema WMA imeendelea kuhakiki vipimo kwa weledi mkubwa zaidi na kupanua wigo wa huduma ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na Tanzania kuwa mwanachama wa mashiria ya kikanda na kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Suleiman Sadiq, alipongeza kazi zinazofanywa na WMA huku akiwahimiza waongeze bidii kutatua kero za wananchi.

Aliitaka wakala kuhakikisha inafuatilia vituo vya mafuta, mita za maji pamoja na kutoa elimu zaidi kwa wakulima hasa kwa wakulima wa korosho na pamba ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati.

Mwisho

Tume ya Haki za Binadamu, TLS wakubaliana kushirikiana

Na Mbaraka Kambona

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, ametembelea Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) jijini Dodoma na kuhimiza ushirikiano baina ya taasisi hizo.

Jaji Mwaimu alitoa kauli hiyo juzi alipofanya ziara katika ofisi za chama hicho kwa lengo la kufahamiana na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano.

Akiongea katika kikao hicho kifupi, Jaji Mwaimu alimueleza muwakilishi wa Rais wa TLS jijini Dodoma, Mary Munissi kuwa tume inafahamu kuwa TLS imekuwa msaada mkubwa kwa jamii katika  utoaji wa msaada wa kisheria na kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao.

“Majukumu yetu kwa kiasi kikubwa yanafanana, hivyo itakuwa vizuri tukishirikiana katika kuwasaidia wananchi kupata na kufurahia haki zao.

“Ni jukumu letu sisi sote kuwahudumia na kulinda haki za wananchi na kuhakikisha wakati wote wanaweza kupata haki na kufikia kwa urahisi vyombo vinavyohusika na utoaji haki nchini.

“Tumekuja hapa kuonesha nia yetu ya kutaka ushirikiano, kushirikiana na wadau kwetu sisi ni moja ya kipaumbele chetu, hivyo niwaeleze kuwa tupo pamoja, tuunganishe nguvu na tufanye kazi kwa dhumuni la kuwahudumia wananchi,” alieleza Jaji Mwaimu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mohamed Hamad, alisema tume wakati wote imekuwa na ushirikiano mzuri na asasi za kiraia nchini na mpaka sasa wameshaingia mkataba wa ushirikiano na asasi 21.

“Sisi tume tunaamini haki za binadamu ni suala mtambuka ambalo linahitaji jitihada za pamoja kutekeleza, tume peke yake haiwezi, jambo muhimu ni kuunganisha nguvu zetu ili kutekeleza na kusimamia haki za binadamu nchini,” alisema Hamad.

Kwa upande wa Munissi alisema amefurahishwa na ziara hiyo ya viongozi wa juu wa tume kutembelea ofisi hizo na kuahidi salamu hizo atazifikisha kwa Rais wa TLS na kuahidi watatumia vyema ushirikiano huo ambao utasaidia kurahisisha utendaji wa kazi.

Katika hatua nyingine, TLS imeiomba tume kuwapa ushirikiano wa karibu hususanI katika eneo la haki za binadamu, na kuangalia uwezekano wa kuwasaidia kuwakwamulia vikwazo wanavyokutana navyo wakati wa utekelezaji wa mradi wao wa upatikanaji wa haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles