24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi waruhusu ACT- Wazalendo kufanya mkutano

kamishna-Nsato-Mssanzya1NA MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi nchini, limetoa ruksa kwa Chama cha ACT-Wazalendo kufanya mkutano wa Kamati Kuu, licha ya kuwapo zuio la kufanyika mikutano ya kisiasa ya ndani na nje nchi nzima.

Uamuzi  wa kuzuia mikutano ya ndani yakiwamo maandamano ya Operesheni Ukuta yaliyokuwa yamepangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wiki iliyopita, ulitangazwa na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya.

Alisema katika siku za hivi karibuni jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa, vikitaka kufanya mikutano na maandamano, lakini walivizuia hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Bila kutaja ni vyama gani, Kamishina Mssanzya alisema walibaini kuwapo kwa uvunjifu wa amani jambo ambalo alisema hawawezi kukubali litokee.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana kuhusu Chama cha ACT-Wazalendo kufanya mkutano wake wa ndani wa Kamati Kuu, Kamishina Mssanzya alisema jeshi hilo limetumia busara kuruhusu mkutano huo.

“Tangu mwanzo Jeshi la Polisi halikuwa na tatizo lolote la mikutano ya ndani, lakini wakati Ukuta wanatangaza mikakati ya kupambana  na askari wetu walioko uraiani tulishutuka juu ya jambo hilo.

“Lakini si hilo tu ni mengi ambayo yalisababisha polisi tutoe tamko hili, jambo kubwa Ukuta walitaka kutumia vibaya nafasi hiyo.

“Kuhusu huu mkutano wa ACT-Wazalendo, nasema sijatoa kibali kama mtawala natumia busara ndugu yangu mwandishi, tunaamini kuna mikutano ya ndani kama hii ambayo haina uchochezi ruksa kuendelea kwa chama chochote cha siasa,” alisema Kamishina Mssanzya na kuendelea.

“Si nia ya Jeshi la Polisi kukandamiza  demokrasia, mambo ya vyama lazima yaendelee ndugu yangu, hapa nimetumia busara zaidi…mbona siku ile tumemruhusu Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) kuitisha ‘press conference’ kutangazia wafuasi wake usitishaji wa maandamano  waliyokuwa wameyaitisha Septemba mosi?” alihoji.

Lipumba atajwa ACT-Wazalendo

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti  wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, anatajwa kuwa huenda akajiunga na Chama cha ACT-Wazalendo.

Profesa Lipumba kwa sasa ana mgogoro na chama chake cha CUF kutokana na uamuzi wake wa kutangaza kujiuzulu nafasi yake kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana na baadaye kutangaza kubatilisha uamuzi huo hivi karibuni.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa jina la mwanasiasa huyo mkongwe pamoja na baadhi ya wafuasi wake wamekuwa katika harakati za kutafuta njia mbalimbali za kufanya mazungumzo na viongozi wa ACT-Wazalendo ili kuangalia uwezekano wa kuhamia kwenye chama hicho.

Taarifa hizo zilizagaa jana kwenye mitandao ya kijamii wakati chama hicho kikiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu, hali iliyomlazimu Kiongozi Mkuu wa chama hicho,  Zitto Kabwe kukanusha taarifa hizo na kusema katika kikao chao hawana ajenda iliyomuhusu Profesa Lipumba kujiunga na ACT-Wazalendo.

“Hatuna mjadala kuhusu wanachama wapya. Mkumbuke tu hao wanaoeneza tuna wanachama wapya ndiyo waliosema hivyo 2015, ikawaje?,” alihoji Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles