Asifiwe George na Jenipher Thomas(DSJ), Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema linaendelea na upelelezi wa wafanyakazi na viongozi 38 wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC).
Watu hao wanadaiwa kusambaza taarifa za matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijayatangaza.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,   Suleimani Kova, alisema watu hao wanatuhumiwa kukusanya na kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya  jamii Novemba 9 na 10 mwaka huu.
Alidai  watuhumiwa hao wanatuhumiwa  kuingilia majukumu ya (NEC)   kwamba wakati   matokeo ya kura za uchaguzi mkuu wa 2015 yalikuwa yakisubiriwa,  wao walikuwa wakisambaza taarifa za matokeo kupitia mitandao ya  jamii.
Kova alidai  vijana hao walikiuka maadili ya uangalizi wa uchaguzi na kutangaza matokeo kabla ya NEC kuyatangaza.