24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, May 28, 2022

Pluijm achekelea kifaa kipya Jangwani

Hans van der Pluijm
Hans van der Pluijm

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kiwango kilichoonyeshwa na kiungo, Juma Mahadhi, kilichangia kuongeza kasi ya mchezo na kusaidia kupata ushindi mnono dhidi ya Majimaji juzi.

Mchezo huo ambao ni wa tatu kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulichezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo wenyeji Yanga walishinda mabao 3-0.

Matokeo ya juzi yaliiwezesha Yanga kufikisha pointi saba na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi unaoongozwa na Azam FC waliofikisha pointi 10, baada ya kushuka dimbani mara nne.

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya mchezo huo, Pluijm alikiri kuwa wachezaji wake walipotezana uwanjani katika kipindi cha kwanza na kushindwa kupeleka mashambulizi ya nguvu langoni kwa Majimaji.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema baada ya kugundua udhaifu wa kikosi chake, alifanya mabadiliko kipindi cha pili na kumuingiza Mahadhi ambaye aliongeza kasi ya mchezo na kusababisha kupatikana kwa mabao mawili ndani ya muda mfupi.

“Washambuliaji walishindwa kuzitumia vyema nafasi walizopata kipindi cha kwanza baada ya kubanwa sana na wapinzani, lakini mabadiliko niliyofanya yalichangia kuongeza kasi na kuwazidi maarifa wapinzani wetu,” alisema.

Pluijm alidai kuwa ushindi wa juzi umewaongezea wachezaji morali ya kuendelea kufanya vizuri katika michezo mingine inayowakabili kwenye ligi hiyo, baada ya awali kulazimishwa suluhu na Ndanda FC.

Alisema sasa kikosi hicho kinaanza kujiwinda kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Mwadui FC, utakaochezwa Septemba 17, mwaka huu katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Majimaji, Peter Mhina, alisema ukata unaokikabili kikosi hicho ndio umechangia kupunguza morali ya ushindi kwa wachezaji tangu kuanza kwa ligi msimu huu.

Tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti 20, mwaka huu Majimaji haijafanikiwa kuonja ladha ya ushindi baada ya kucheza michezo minne, ambapo inashika mkia kwenye msimamo ikiwa haina pointi yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,577FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles