25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jiko la mkaa laua watatu, lajeruhi wilayani chunya

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa.

Na Eliud Ngondo, Chunya

WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia na mmoja amepelekwa hospitali katika Kijiji cha Lualaje, Kata ya Kipembawe wilayani Chunya mkoani Mbeya, kwa kukosa hewa ya oksijeni baada ya kuwekwa jiko la mkaa ndani.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni baba wa familia hiyo, Leonard Mwashambwa (42), watoto wawili ambao ni Mponeje Leonard (3) na Zaituni Leonard (1).

Madusa alisema mama wa familia hiyo, Rhoda Darama (22), alikutwa ndani akiwa amepoteza fahamu na alikimbizwa katika hospitali ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kisha kuruhusiwa.
Alisema majirani wa marehemu hao walipoona kumekucha na milango haifunguliwi, waliita kwa ajili ya kuwajulia hali majirani zao bila mafanikio na ndipo walipochukua jukumu la kuvunja mlango.

Rhoda alipohojiwa, aliwaeleza kuwa kabla hawajalala, yeye na
mume wake walikuwa hawajisikii vizuri na waliamua kuwasha jiko la mkaa ili wapate joto wakiwa wamelala.

“Hawa watu walifariki kutokana na kuvuta hewa ya cabonmonoxide
iliyotokana na jiko la mkaa walilokuwa wamewasha, lakini tulipochunguza tulibaini kuwa nyumba yao haina madirisha ya kuwezesha kupata hewa ya kutosha,” alisema Madusa.
“Maelezo ya mama aliyenusurika ni kwamba yeye na mume wake walikuwa wanahisi homa, ndio maana waliwasha hilo jiko la mkaa na baadaye walipitiwa na usingizi na kisha kufikwa na mauti,” alisema Madusa.
Madusa alifika katika kijiji hicho kwa ajili ya kuwapa pole ndugu wa marehemu ambapo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuwasha mkaa usiku na kulala kwani ni hatari.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya aliwataka kuhakikisha wanapojenga nyumba zao wanaweka madirisha makubwa kwa ajili ya kuingiza hewa ndani na si kujenga nyumba isiyokuwa na madirisha, hali ambayo ni hatari pia.

Baadhi ya majirani wa marehemu walidai kuwa wakati wanapita nyumbani kwa Leonard walikuta mlango umefungwa wakati si kawaida yao kuchelewa kuamka.

Mussa Simkoko, mkazi wa kijiji hicho, alisema: “Ilikuwa si kitu cha kawaida kwa jirani zetu hawa kuchelewa kuamka,
tulipoona milango haifunguliwi, tuliamua kuwagongea lakini kukawa kimya na tuliposikiliza kwa makini, tulibaini kuwa kuna mtu alikuwa anahema kwa tabu,” alisema Simkoko.

“Tulivyosikia sauti ya mtu kuhema kwa shida ndipo tukasukuma mlango kwa nguvu, tukakuta wenzetu watatu wakiwa wamepoteza maisha huku mwanamke mmoja akiwa anahema kwa shida, tukamkimbiza hospitalini,” alisisitiza Simkoko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles