23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Petroli, diseli sasa Sh 1,500

 MWANDISHI WETU –DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei elekezi za bidhaa za mafuta ya petroli nchini, zitakazotumia kuanzia leo ambazo zimeshuka kwa kiasi kikubwa. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, bei kikomo ya mafuta ya petroli kwa Jiji la Dar es Salaam itakuwa Sh 1,520 kwa lita moja na diseli itakuwa ni Sh 1,546. 

“Pamoja na kutambua bei hizo, ni muhimu kuzingatia bei za jumla na rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Mei 6, 2020. 

“Bei za mafuta ya taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Mei 6, 2020 kwani hakuna shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa mwezi Mei 2020 kupitia bandari ya Dar es Salaam,” alisema Chibulunje. 

Alisema kwa Juni, bei za rejareja za petroli zimepungua kwa Sh 348 kwa lita (asilimia 18.65) na dizeli Sh 300 (asilimia 16.25) ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.

Chibulunje alisema kwa Juni, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita. 

“Hii ni kwa sababu kwa mwezi Mei 2020, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga. 

“Kwa mwezi Juni 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli katika mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Mei 6, 2020 kutokana na kuwa hakuna shehena ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara,” alisema Chibulunje. 

Alisema hata hivyo, bei za mafuta ya dizeli zimepungua ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, ambapo kwa Juni 2020, bei za jumla na rejareja za dizeli zimepungua kwa Sh 425 kwa lita (sawa na asilimia 19.45) na Sh 423.24 kwa lita (sawa na asilimia 20.58). 

Chibulunje alieleza kuwa kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kusafirishwa hadi mkoa husika.

Alieleza kuwa mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium).

Chibulunje alisema Ewura inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo na kwamba huduma hiyo ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 74 la Februari 7, 2020.

 “Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. 

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. 

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” alisisitiza Chibulunje.

Alisema kwa mujibu wa tangazo hilo la Serikali, wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. 

 Alieleza kuwa stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles