27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea ubunge CCM kupitishwa kwenye chujio kali

 NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza utaratibu mpya utakaotumika kuwapata wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Utaratibu huo ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2015 ambao mgombea ubunge alitakiwa kupita kata kwa kata na kupigiwa kura za maoni na wajumbe wa kata wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alisema lengo la mabadiliko hayo ni kupunguza mianya ya rushwa na kutenda haki kwa kila mtu. 

“Kama 2015 mbunge alitakiwa kupita kata kwa kata na kupigiwa kura za maoni, mchakato ule ulikuwa na mapungufu na kuacha mianya ya rushwa,” alisema Polepole.

Alisema utaratibu wa sasa utahusisha Kamati ya Siasa ya Wilaya, Kamati ya Siasa ya Mkoa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambazo zitawajadili waliochukua fomu na kutoa mapendekezo, kisha Kamati Kuu itateua majina matatu yatakayopelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo.

“Majina hayo yatakuwa ni siri kubwa na yatawekwa muhuri wa moto, kisha yatarejeshwa kwenye mkutano wa jimbo ambao utakuwa na wajumbe kati ya 800 hadi 1,000 kwa ajili ya kupigiwa kura,” alisema Polepole.

Alisema mkutano mkuu wa jimbo ukishapigia kura majina hayo matatu, utatengenezwa muhtasari na kuonyesha kila mgombea na kura zake kisha yatarudishwa kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). 

“Mchakato utakaofuata utakuwa ni kuwajadili kwa mara ya pili na kutoa mapendekezo, kisha Halmashauri Kuu ya Taifa itafanya uteuzi wa jina moja litakalopelekwa NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi),” alisema Polepole. 

Alisema kupitia utaratibu huo mpya, baada ya mchakato kuanza, mwana CCM anayetaka kugombea haruhusiwi kwenda kuchukua fomu kwa mbwembwe, badala yake atatakiwa kuchukua kimya kimya na kurudi nayo nyumbani kuijaza kisha kuirejesha.

“Utakwenda kuchukua fomu ofisi ya chama ya wilaya kwa unyenyekevu mkubwa na si kwa tarumbeta, utajaza na kuirejesha, hizo tarumbeta zitakuja baada ya kupitishwa kugombea,” alisema Polepole.

Kwa upande wa Zanzibar, alisema Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ngazi ya jimbo ndiyo itakayoketi kuwajadili wagombea uwakilishi na kutoa mapendekezo.

UDIWANI

Kwa upande wa nafasi ya udiwani, Polepole alisema vikao vitakavyojadili majina ni vya kata, wilaya na mkoa.

Alisema kikao cha mkoa kitapendekeza majina matatu yatakayorudishwa kwenye mkutano mkuu wa kata.

Alifafanua kuwa mkutano mkuu wa kata utapiga kura za maoni na majina yatapelekwa ngazi ya mkoa.

“Mchakato wa udiwani uko katika ngazi ya mkoa kwa sababu ndiyo mamlaka ya uteuzi, lakini viwango na masharti ya chama yatazingatiwa,” alisema Polepole.

KADI ZA KIELEKTRONIKI

Polepole alisema katika uchaguzi wa mwaka huu watatumia kadi za kielektroniki ili kuepusha mamluki wakati wa upigaji kura.

“Sasa hivi tutatumia utaratibu wa kielektroniki na utambulisho huo utafanyika kwa vikao vyote na mkutano mkuu wa taifa wa CCM,” alisema Polepole.

RUSHWA

Polepole alisema chama hicho kiko makini katika kusimamia nidhamu na alitangaza namba mbili zitakazotumika kupokea taarifa mbalimbali za vitendo vya rushwa ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.

Kupitia namba hizo, watu wataweza kutuma ushahidi wa sauti, picha au video za wanaotoa rushwa ili kupata uongozi na kwamba taarifa hizo zitaoanishwa na vyanzo vingine ndani ya chama kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Chama kiko imara katika kusimamia maadili, ikiwemo kuwasaka kokote waliko wanaotumia rushwa kutaka uongozi, tukibaini baadhi ya viongozi walijihusisha na rushwa tutaielekeza Serikali kushughulikia maofisa waliopewa dhamana, tutawaambia hawatoshi.

“Tunaposimamia haki ipasavyo na maadili tunaweza kupata wana CCM wazuri na kukifanya chama chetu kiwe kimoja,” alisema Polepole. 

Alivitaka vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwachukulia hatua watu wanaojipitisha mikoani, wilayani, kata na kwenye majimbo kwa kisingizio cha kuchangisha fedha za fomu za mgombea urais.

“Muwatolee taarifa polisi na Takukuru hao ni matapeli, michango yoyote ya chama inafanyika kwa mujibu wa kanuni za fedha,” alisema Polepole.

WATAFITI NDANI YA CHAMA

Polepole alisema chama kupitia katika kitengo chake cha utafiti tayari kimeshafanya utafiti wa viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge.

“Kuna watu wanapita huko wanasema ni watafiti wa chama, kazi ya utafiti ilishaisha, wakionekana wapuuzwe na watolewe taarifa kwenye vyombo ya dola.

 “Hakuna mtu yeyote ametumwa na mwenyekiti wa CCM kwenda kugombea mahala popote, yeyote anayefanya hivyo kuna dawa mpya tumeiongeza ya kushughulikia watovu wa nidhamu,” alisema Polepole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles