24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

‘Pelekeni nakala ya vyeti vya ndoa RITA vikasajiliwe’

Asha Bani, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), imezitaka taasisi za dini na wasajili wote wa ndoa nchini, kuhakikisha  wanarudisha nakala za vyeti vya ndoa kwa wakati ili ziweze kuingizwa kwenye daftari la Msajili Mkuu wa Ndoa.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Mtanzania Digital.

“Viongozi wengi wanaofungisha ndoa katika makanisa na misikiti wamekuwa wakichelewa na wengine kutopeleka kabisa nakala za marejesho ya ndoa katika Ofisi ya Msajili Mkuu wa Ndoa na Talaka kila mwezi kama sheria inavyosema.

“Kwa mujibu wa Sheria ya ndoa namba 29 ya mwaka 1971 kama ilivyorudiwa mwaka 2002, kifungu cha 46 kinasema; “Kila msajili wa ndoa itambidi kumpelekea cheti kwa  Msajili Mkuu wa Ndoa nakala iliyothibitishwa kuwa ni nakala ya kweli ya ndoa zote alizoziandika kwenye daftari la ndoa alilo nalo mnamo siku 30 baada ya siku ya mwisho ya kila mwezi,” amesema.

Amesema kuna madhara endapo hakutakuwa na mrejesho huo kwa wakati ikiwa ni pamoja na kukosa takwimu halisi ya ndoa zote zinazofungishwa nchini, jambo ambalo ni hatari pale linapokuja suala la ukusanyaji wa takwimu za matukio muhimu ya binadamu kama vile ndoa.

“Sheria ya ndoa iko wazi kuhusiana na viongozi wa taasisi za kidini kuleta nakala za marejesho ya vyeti vya ndoa hivyo tunawakumbusha viongozi wote wanaofungisha ndoa katika misikiti na kanisani kutimiza wajibu wao mapema,” amesema Emmy.

Pamoja na mambo mengine, ameitaja mikoa inayoongoza kwa kutopeleka nakala za vyeti vya ndoa zao kwa ajili ya usajili katika Ofisi ya Msajili Mkuu wa Ndoa Tanzania Bara kuwa ni pamoja na Mtwara, Lindi, Geita, Rukwa, Katavi, Mara na Mbeya.

“Hata hivyo baadhi ya mikoa kama vile, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga na Dodoma inajitahidi katika kuleta nakala za marejesho hayo,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles