22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Pasaka 2019 yaja kivingine

Na MWANDISHI WETU 

-DAR ES SALAAM

WAKATI leo waumini wa madhehebu ya Kikristo nchini wakiungana na wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, kwa mwaka huu imeonekana kuwa tofauti na ile ya mwaka jana.

Wafuatiliaji wa mwenendo wa mambo wanasema Pasaka ya mwaka huu imepita ikiwa na ‘utulivu’.

Wanasema hivyo wakirejea ile ya mwaka jana, ambayo Wakristu na hasa viongozi wa dini walionekana kuandaa nyaraka zilizotumika katika kipindi cha kuelekea maadhimisho ya Pasaka kutafakari mustakabali wa nchi na mwenendo wa mambo katika nyanja ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, hali iliyoibua mijadala mikali.

Tofauti na Pasaka ya mwaka jana, mwaka huu hakukuwa na kanisa lolote lililotoa waraka zaidi ya kutoa mahubiri kuanzia Ibada ile ya Ijumaa Kuu kutoa ujumbe mzito wakikemea watetezi feki wa wanyonge, utesaji, utumwa, matumizi yasiyofaa ya simu ambayo yameziweka ndoa nyingi shakani na kuhubiri amani, uhuru, upendo na kujitoa kwa ajili ya wengine.

Mahubiri ya aina hiyo, ambayo pia yanatazamiwa kutolewa hata leo, baadhi wanaona kuwa bado yanaitofautisha Pasaka ya mwaka jana na ile ya mwaka huu.

Juzi wakati wa maadhimisho ya Ijumaa Kuu, katika ibada ya Kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Lukajange, Karagwe mkoani Kagera, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Karagwe, Dk. Benson Bagonza, aliitumia siku hiyo kupeleka ujumbe wa kuonya juu ya watu wanaojidai kutetea wanyonge kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe na zaidi akionya wale wenye tabia ya utesaji na kugeuza wenzao watumwa.

Si Askofu Bagonza tu, naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea,  Damian Dallu, katika mahubiri yake ya Ijumaa Kuu kwa mwaka huu alikemea tabia ya woga na kushindwa kuhubiri ukweli dhidi ya watu wenye nia ovu.

Wakati kauli hizo za kukemea katika Pasaka ya mwaka huu zikionekana kutolewa kwenye mahubiri tu, Itakumbukwa mnyukano wa hoja ulioshuhudiwa mwaka jana katika kipindi chote cha Kwaresma kuelekea Sikukuu ya Pasaka ulichagizwa na Waraka uliotolewa wa maaskofu 35 wanaounda Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) mwanzoni mwa safari ya siku 40 ya mfungo wa Kwaresima na ule uliotolewa baadaye kidogo na Maaskofu 27 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT).

Nyaraka hizo mbili, ambazo ziliibua mijadala mikali, pamoja na mambo mengine, uligusa na kuonya mwenendo wa masuala ya uchumi, siasa na kijamii.

Mwanzo wa mijadala na malumbano hayo kuelekea Pasaka ya mwaka jana ni Waraka wa TEC uliotolewa Februari 9, 2018, ukiwa ni ujumbe wa Kwaresima chini ya kaulimbiu “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu: Mt.28:19”.

Ni waraka huo na ule uliokuja baadaye wa Maaskofu 27 wa KKKT, ndio uliotajwa kuwa nyuma ya kauli ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, ambaye mapema alilitumia kongamano la vijana lililofanyika Bagamoyo kuupinga, akisema viongozi wa dini hawapaswi kuchanganya siasa na kazi yao ya kitume.

Waraka wa TEC ulichambua mambo mbalimbali, ikiwamo kuwakumbusha  waumini maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji  kwa mwaka huu wa 2019.

Pia ulichambua uminyaji wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari kwa ufafanuzi wa kwamba shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola.  

Waliainisha mambo ambayo wanaona pengine hayako sawasawa na waliyodai kuwa yanavunja Katiba na Sheria za nchi kama shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, ambazo walidai zimekoma hadi uchaguzi mwingine, mfano mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, mambo ambayo walidai kuwa ni haki ya kila raia. 

Ukiacha waraka huo wa TEC, waraka wa Pasaka uliotolewa na Baraza la Maaskofu wa KKKT na ambao ulikusudiwa siku ya Pasaka mwaka jana ndio ulionekana kuchochea zaidi wingi wa matamko wa ama kuwapinga au kuwaunga mkono viongozi hao wa kiroho kuelekea sikukuu hiyo.

Waraka huo wa KKKT ambao uliandaliwa na maaskofu 27, akiwamo Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Fredrick Shoo, ulichambua masuala ya jamii, uchumi, maisha ya siasa, umuhimu wa Katiba Mpya na matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi ya Taifa. 

Ni waraka huo ndio ulioibua mgogoro ndani ya kanisa hilo kwa baadhi ya Maaskofu wake kutousoma katika makanisa yao kama walivyoelekezwa na hivyo kuishia kupewa adhabu ambayo ilitishia kazi yao ya kitume.

Miongoni mwa Maaskofu hao ni Askofu Dk. Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambaye aliadhibiwa kwa usaliti.

Uamuzi huo wa Baraza la Maaskofu wa KKKT uliwagusa kwa namna nyingine maaskofu wengine wawili wa kanisa hilo.

Maaskofu hao ni Askofu wa Dayosisi ya Kusini na Mashariki, Lukas Mbedule  na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomoni Massangwa, ambao walipewa sharti la kuomba radhi na kuwa ndani ya Dayosisi zao.

Itakumbuwa waraka huo wa KKKT katika eneo la uchumi ulionya kile ilichokiona kuwako kwa dhana ya serikali kutaka kushindana na wadau wa maendeleo, lakini pia mfumo usio sahihi wa ukusanyaji kodi na ambao unafilisi wafanyabiashara.

Kuhusu siasa, waraka huo ulikumbusha misingi ya siasa safi na uongozi bora na kuonya serikali kuminya demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa Bunge na vyombo vinavyotoa na kusimamia haki kama Mahakama na Tume ya Uchaguzi.

Zaidi ulizungumzia dhana ya kile kinachodhaniwa baaadhi ya wanasiasa kununuliwa na gharama za kurudia uchaguzi, huku katika suala la ajira kwa vijana ukitaka jitahada za wazi zifanyike na kuonya elimu kuchokonolewa.

Waraka huo ulisema suluhisho la yote hayo ni upatikanaji wa Katiba mpya, ambayo ina maoni ya wananchi na kupendekeza suala hilo lifanyike kabla ya uchaguzi wa mwakani.

Wakati hayo yakionekana kuibua mjadala katika Pasaka hiyo ya mwaka jana, zaidi kitendo cha Askofu Pengo kuibuka siku moja baadaye baada ya KKKT kutoa waraka huo na kukosoa ule uliotolewa na TEC, kiliibua mjadala mpya na hata kujenga hisia kwa baadhi kwamba huenda alilenga kujibu nyaraka zote mbili.

Siku moja baadaye baada ya waraka huo wa KKKT kutolewa, Rais Dk. John Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), aliwaomba Maaskofu na viongozi wengine wa dini kuhubiri ujenzi wa viwanda vya dawa.

Hata hivyo, katika kipindi chote cha Kwaresma ya mwaka huu, Askofu Pengo hajasikika akitoa jambo lolote ambalo limechukua mjadala na hata juzi wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu, licha ya kushiriki katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, hakuhubiri, badala yake kazi hiyo ilifanywa na Mkurugenzi wa Utume na Familia, Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Padri Novatus Mbaula.

Padri Mbaula katika ibada hiyo alishauri kupunguza matumizi ya simu za mikononi ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia mafarakano kwa wanandoa na jamii kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,057FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles