24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

THRDC wasema wako tayari kumsaidia mtoto aliyevunjwa uti wa mgongo na mwalimu


Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema  upo tayari kumsaidia kisheria aliyekuwa  mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke, Hosea Manga (10), mkazi wa Kijiji cha Madeke Kata ya Mfriga wilayani Njombe, anayedaiwa kupigwa na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu  na mwalimu anayetajwa kwa jina la Focus Mbilinyi, miaka miwili iliyopita na kusababishiwa kuvunjika uti wa mgongo.

Tukio hilo ambalo limedaiwa kufanywa na mwalimu  huyo  ambaye kwa sasa  inasemekana amehamishiwa  Kata ya Mtwango, lilitokea Machi 21, mwaka 2017 wakati Hosea akiwa na umri wa miaka (8) ambapo mtuhumiwa huyo  anadaiwa kumwadhibu viboko kumi baada ya kukosa hesabu.

Akizungumza na gazeti hili Mratibu wa THRDC ,Onesmo Olengurumwa, alisema  mtandao huo huwa  una utaratibu wa kuwasaidia watu  wanaohitaji msaada wa kisheria kwa kufuata taratibu ambazo zimewekwa.

“Sisi tukipata taarifa kuhusu kesi kama hiyo tunatumia wanachama wetu ambao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  ambapo tutawatumia  taarifa  za namna ya tukio lilivyotokea ambazo tunakuwa tumezipata kutoka kwa wahusika na wao najua watakapoanzia na  kwa tukio hili kuna watu maalumu ambao wanawasaidia watoto,” alisema Olengurumwa.

Alisema ili wahusika waweze kushughulikiwa tatizo lao wanapaswa kuwa na nyaraka zote  za muhimu  na taarifa kamili ya tukio zima  ikiwezekana wanaweza wakatoa mawazo yao nini wanahitaji.

Kauli ya THRDC imekuja  wakati ambao  baba  mzazi wa mtoto  huyo, Hosea Manga, akidai kuwa pamoja na  kuendelea kumtibia mtoto wake lakini anahitaji msaada  zaidi ili haki itendeke kwa kuwa kesi  ya Jinai namba 83 ya mwaka 2017 waliyoifungua  ili kumshtaki mwalimu huyo katika Mahakama ya Mkoa wa Njombe ilifutwa.

Alisema kesi hiyo ilifutwa baada ya  daktari aliyemtibu mtoto huyo mara ya mwisho katika Hospitali ya Muhimbili kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.

Gazeti hili pia bado linaendelea kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Ole Sendeka, ambaye aliahidi kulishughulikia suala hilo kwa kuwa alishapokea malalamiko hayo ofisini kwake.

Mbali na Ole Sendeka, Mwanasheria Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Wakili Helman Danda, alikiri kesi hiyo kufutwa kwa sababu Jamhuri ilishindwa kupeleka shahidi ambaye ni daktari wa mwisho aliyemtibia mtoto huyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli nimefuatilia nimeona kesi ilifutwa na sababu ni upande wa ushahidi ambaye ni daktari wa Muhimbili kushindwa kuja kutoa ushahidi, kwa mazungumzo zaidi mtafute Mkuu wa Mkoa,” alikaririwa Mwanasheria huyo alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili mkoani Njombe.

Mwandishi wa gazeti hili alifika nyumbani kwa mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la tatu Kijiji cha Madeke umbali wa kilomita 103 kutoka Njombe mjini mapema.

Akizungumza na gazeti hili mtoto huyo alisema tukio hilo lilitokea Machi 21 mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka (8) ambapo alipigwa na mwalimu kwa sababu ya kukosa hesabu.

Alisema siku ya tukio akiwa darasani kwenye kipindi cha somo la hesabu lililokuwa likifundishwa na mwalimu aliyemtaja kwa jina la Focus Mbilinyi ambaye aliwataka kufanya majaribio, yeye na wenzake wawili walikosa hesabu zote 10.

“Ilikuwa asubuhi tukiwa darasani tunasoma somo la hesabu mwalimu alitupa hesabu 10 na akasema ukikosa utachapwa kulingana na hesabu ulizokosa, hivyo mimi  nilikosa hesabu zote na kutakiwa kuchapwa fimbo 10, mwalimu wakati anatuchapa, tulikuwa watatu, alituning’iniza kichwa chini miguu juu katika moja ya dirisha la darasani ndipo nilipoangukia mgongo na kuhisi  maumivu makali yaliyosababisha hadi leo natumia muda mwingi nikiwa hapa  kitandani,” alisema Hosea.

Kwa sasa mtoto Hosea anatumia muda wake mwingi akiwa amelala kitandani  kutokana na maumivu makali anayoyapata baada ya tukio hilo la kuumia mgongo lililosababisha kutokea kwa kidonda kikubwa sehemu ya chini unapoishia uti wa mgongo.

Zaidi wakati wote wa ugonjwa wa takribani miaka miwili, ameshindwa kuendelea na shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles