27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA yakamilisha tathmini ya vihatarishi vya usalama, afya Bwawa la Mwl. Nyerere

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umekamilisha tathmini ya awali ya vihatarishi vya usalama na afya (baseline occupational safety and health risk assessment) katika eneo la mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwl. Julius Nyerere (JNHP) lililopo Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (watatu kulia) akiambatana na baadhi ya viongozi wa OSHA katika ziara yake ya kutembelea mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa lengo la kufuatilia zoezi la tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya katika mradi huo iliyofanywa na wataalamu wa OSHA hivi karibuni.

Kwa mujibu wa kifungu Na. 60 cha Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, wamiliki/wasimamizi wa sehemu za kazi wanawajibika kuhakikisha kwamba maeneo yao ya kazi yanafanyiwa tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya walau mara moja kwa mwaka ili kupata taarifa muhimu zinazohitajika katika kuandaa mikakati madhubuti ya kulinda uwekezaji na kuwakinga wafanyakazi dhidi ya athari za vihatarishi katika eneo la kazi husika.

Taarifa ya kukamilika kwa zoezi la tathmini ya vihatarishi imetolewa na Mtendaji Mkuu wa OSHA ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini, Khadija Mwenda, alipofanya ziara katika eneo la mradi hivi karibuni kama sehemu ya kukamilisha kazi hiyo ya tathmini.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (katikati) Pamoja na baadhi ya viongozi wa OSHA wakipokea maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja wa Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Mhandisi. Mathew Bundala wakati wa ziara iliyolenga kufuatilia zoezi la tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya katika mradi huo iliyofanywa na wataalamu wa OSHA hivi karibuni

Akizungumza baada ya ziara hiyo Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi yenye dhamana ya masuala ya usalama na afya mahali pa nchini amesema: 

“Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya sheria tajwa, mwaka 2022, Shirika la Umeme (Tanesco) kwakuzingatia uzoefu wetu na uwepo wa wataalam wa kutosha waliobobea katika masuala ya usalama na afya kazini, lilituomba kufanya tathmini ya awali ya vihatarishi katika eneo la mradi na kutoa ushauri elekezi kuhusiana na uimarishaji wa mifumo ya kudhibiti vihatarishi mahali pa kazi.

“Hivyo, baada ya wataalam wangu kukamilisha kazi niliyowatuma nami nimeona ni muhimu kufika katika eneo la mradi kuona kama kazi hiyo imefanyika kikamilifu. Aidha, imekuwa ni muhimu pia kuja kuona hali ilivyo baada ya mtambo mmoja kuwashwa kwani wakati tathmini inafanyika uzalishaji ulikuwa bado haujaanza,” amesema Mwenda.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya katika maeneo ya kazi wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Aidha, Mwenda, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na kumpongeza Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wote waandamizi wa serikali kwakuwa na dhamira ya dhati ya kutekeleza mradi huo wa pili kwa ukubwa Barani Afrika ambao ni dhahiri kuwa utamaliza changamoto ya upungufu wa nishati ya umeme nchini pindi utakapokamilika.

“Hatua iliyochukuliwa na serikali yetu kutekeleza mradi huu wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji (hydropower generation) ni ya msingi sana na yenye tija kubwa katika kuchagiza ukuaji wa uchumi hapa nchini,” amefafanua Mtendaji Mkuu.

Akielezea mchango wa OSHA katika mradi huo, Kiongozi huyo amebainisha kuwa Taasisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi wa usalama na afya mara kwa mara tangu mradi ulipoanza na hivyo kupunguza ajali, magonjwa na vifo miongoni wa wafanyakazi wa mradi.

Ameongeza kuwa kaguzi, miongozo na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA umesaidia kwa kiwango kikubwa mradi huo kutekelezwa kwa mafanikio ikiwemo kukamilika kwa wakati na katika viwango stahiki kutokana na kuwa na nguvukazi yenye afya njema pamoja na zana na mitambo yenye ufanisi wa kutosha.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda pamoja na baadhi ya viongozi na watumishi wa OSHA wakifuatilia muhtasari wa mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) na namna ambavyo mradi huo utamaliza kero ya umeme nchini pindi utakapokamilika uliowasilishwa na Mhandisi Dismas Mbote (mbele).

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mradi huo kutoka TANESCO, Mhandisi Mathew Bundala, ameushukuru uongozi wa OSHA kwa ushirikiano wao katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya kwa wafanyakazi katika mradi huo jambo ambalo limesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali, magonjwa na vifo vya wafanyakazi katika eneo la mradi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, OSHA itaendelea kufanya ukaguzi wa usalama na afya katika eneo la Bwawa hata baada ya shughuli za ujenzi kukamilika ili kuhakikisha kwamba uzalishaji unakuwa endelevu na nguvukazi iliyopo inalindwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles