24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA yaagizwa kupanua wigo wa Programu za Wajasiriamali wadogo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umegizwa kupanua wigo wa  programu atamizi za wajasiriamali wadogo ili waweze kuyafikia makundi mengi zaidi katika sekta zote za uzalishaji mali nchini.

Maagizo hayo yametolewa Desemba 20, 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, kupitia hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dk. Adelhelm James Meru katika kikao cha Tano (5) cha Baraza la Nne (4) la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika jijini Arusha.

Agenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kutathmini utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha uliopita (2021/22) pamoja na nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023.

“Ninawaagiza kupanua zaidi wigo wa programu atamizi ya wajasiriamali (SMEs Incubation Programme) ili muweze kuyafikia makundi mengi zaidi ya wajasiriamali wadogo katika sekta zote kiuchumi. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumeisadia sana nchi yetu kwani sekta isiyo rasmi yenye makundi mengi ya wajasiriamali wadogo ndiyo inayoajiri idadi kubwa ya Watanzania,” amesema Dk. Meru.

Kwa mujibu wa taaarifa ya utekelezaji majukumu ya Taasisi ya OSHA kwa mwaka wa fedha uliopita (2021/2022), OSHA iliwafikia wachimbaji wa madini na wajasiriamali wadogo 11,204 zaidi ya lengo la wajasiriamali 10,000. Hivyo, Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi kuwataka kuweka malengo ya kufikia idadi kubwa zaidi katika kipindi kijacho.

Aidha, Dk. Meru amewataka wafanyakazi wote wa OSHA kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubunifu zaidi ili waweze kuongeza tija katika Taasisi na Taifa kwa ujumla.

“Natambua kwamba Taasisi hii yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa letu bado ina kazi kubwa ya kufanya kwani maeneo ya kazi hapa nchini ni mengi na yanazidi kuongezeka kila siku hivyo tunahitajika kujituma zaidi na kuwekeza zaidi katika miundombinu na rasilimali muhimu zitakazotuwezesha kufikisha huduma hizi muhimu za masuala ya Usalama na Afya kwa watanzania wote,” amesema Dk. Meru.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 Taasisi anayoiongoza ilitekeleza majukumu yake kikamilifu na hivyo kuvuka baadhi ya malengo iliyojiwekea katika mwaka huo wa fedha.

“Tulifanikiwa kusajili maeneo ya kazi 7,260 ukilinganisha na lengo la kusajili maeneo ya kazi 7,000 na hivyo kufikia asilimia 103.7. Mafanikio mengine ni pamoja na kufanya kaguzi 217,102 ukilinganisha na kaguzi 200,000 zilizopangwa kufanyika, kupima afya jumla ya wafanyakazi 252,733 zaidi ya lengo la kupima wafanyakazi 250,000, kutoa mafunzo kwa maafisa 14,661 ikilinganishwa na maafisa 10,000 waliolengwa,” amesema Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA.

Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, wakati akifunga kikao hicho cha tano cha baraza la nne la wafanyakazi wa OSHA, amewataka watumishi wote kuendelea kuchapa kazi huku akiwahakikishia kuwa ataendelea kushirkiana na viongozi wa Taasisi hiyo kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao. 

“Nitumie fursa hii kuwahakikishia kwamba sisi viongozi wenu tupo pamoja nanyi na tutajitahidi kwa kadri inavyowezekana kusaidia kutatua changamoto zilizoainishwa ili kuiwezesha Taasisi yenu yenye dhamana kubwa ya kulinda nguvukazi ya Taifa kuweza kufanikisha malengo yake. Hivyo, nisisitize kila mmoja wetu kuchapakazi pamoja na kuzingatia weledi na maadili ya utumishi umma kwa maslahi mapana ya OSHA na Tanzania kwa ujumla,” amesema Prof. Jamal Katundu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles