30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nsokolo: Rais Dk. Samia ametoa matumaini Sekta ya Habari nchini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Sekta ya Habari nchini imeelezwa kuwa na mwelekeo chanya tangu kuingia madarakani kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan nakwamba hatua hiyo inatoa matumaini kwa wadau.

Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini Tanzania(UTPC), Deogratius Nsokolo wakati akitoa maoni yake leo kuhusu mwenendo wa mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini ambapo amesema kuwa Rais Dk. Samia ni rafiki wa waandishi wa habari.

Amesema maendeleo ya mchakato huo yanatokana na kuridhiwa na Serikali ya Dk. Samia.

“Rais Dk. Samia tangu alipongia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hi ya mwaka 2016. Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari na serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani tungependa viondolewe,” amesema Nsokolo.

Nsokolo amesema utayari huo umeoneshwa wazi hasa baada ya wasaidizi wa kiongozi huyo namba moja wa nchi kuonyesha kwa vitendo hatua kwa hatua katika kukutana na wadau kwenye vikao vya pamoja.

“Upande wa serikali na wadau umeishamaliza kazi yake ya kuainisha vipengele hivyo, kilichotarajiwa ni mwaka huu mwezi wa tisa mapendekezo hayo kupelekwa bungeni lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana.

“Serikali kwa uwazi kabisa ilieleza sehemu mkwamo kwamba, Waziri (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) alisema, mapendekezo hayo hayakufikishwa bungeni kwa kuwa kuna hatua zilikuwa hazijakamilika. Hii ni dhamira ya wazi kabisa ya serikali hii,” amesema Nsokolo.

Amesema kazi iliyobaki sasa ni upande wa serikali kukamilisha mchakato na kisha mapendekezo hayo kupelekwa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi kwa sababu, vile vitu ambavyo tuliviona ni vikwazo, vitakuwa vimeondolewa.

“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, yatasaidia sana maendeleo ya nchi yetu kwa sababu, habari ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” amesema Nsokolo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema mchakato huu unakwenda kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.

Na kwamba, baada ya wadau wa habari kufanya vikao serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” amesema Balile na kuongeza:

“Tulifanya mkutano wa mwisho mwezi Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni,” amesema.

Hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike.

“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake,” amesema Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles