23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

OCD, Ofisa Ushirika matatani kwa tuhuma za rushwa

Na DERICK MILTON -MEATU

MKUU wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Dk. Joseph Chilongani ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) wilayani humo, kuwachunguza Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Elsante Olomi na Ofisa Ushirika wa Wilaya, George Budodi.

Viongozi hao wanatuhumiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni mbili kutoka kwa viongozi wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kijiji cha Mbushi, fedha zilizokuwa maalumu kwa ajili ya kulipa madeni ya wakulima wa pamba.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Mazao ya Wilaya, mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa mbali na kuchunguzwa Takukuru ameagiza Ofisa Ushirika kutojihusisha na kazi yeyote ya serikali hasa inayohusu ushirika.

Kuhusu Mkuu wa Polisi, Dk. Chilongani alisema kuwa watatoa taarifa kwenye mamlaka zake zinazohusika ili aweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na tuhuma hizo.

Akitoa maelekezo jinsi walivyoomba rushwa hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa viongozi hao wa Amcos ya Mbushi walikuwa wanadaiwa na wakulima kiasi cha Sh milioni 15.

“Nilitoa maagizo kuwa viongozi hao wa Amcos wanatakiwa kurejesha pesa hizo za wakulima Shilingi milioni 15 mara moja, na walifanya hivyo kwa kurejesha kidogo kidogo.

“Katika deni hilo walibakiza kiasi cha Shilingi milioni tano, ambazo walitakiwa kuzirejesha kabla ya Desema 31, 2019, na walifanikiwa kuzipata na kuzileta polisi,” alisema Dk. Chilongani.

Alisema kuwa katika maelekezo ya awali, aliagiza viongozi hao wa Amcos wakimaliza kurejesha fedha hizo za wakulima wanatakiwa kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria ikiwemo kufikisha mahakamani.

Alisema baada ya viongozi hao wa Amcos kurejesha fedha za mwisho Sh milioni tano kwenye deni hilo la milioni 15, waliombwa Sh milioni mbili na OCD pamoja na Ofisa Ushirika huyo ili wasiwafikishe mahakamani.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa Amcos walikataa kutoa rushwa hiyo akiwemo Katibu Mathias Manunda, na kuamua kwenda ofisini kwake kutoa taarifa hizo za kuombwa Sh milioni mbili kama rushwa kutoka kwenye Sh milioni tano ambazo ni fedha za wakulima wa pamba.

Dk. Chilongani alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo waliwaita kwenye kikao OCD na Ofisa Ushirika, ambapo OCD hakuweza kutokea na Ofisa Ushirika alipoulizwa alikiri waliomba fedha hizo huku akiahidi kuzirejesha.

“Baada ya kukiri tumegundua kuwa ni kweli hicho kitendo kilifanyika, na lazima hatua kali zichukuliwe kwa wahusika wote, wakulima wetu wanahangaika sana kulima lakini wapo viongozi kazi yao ni kuwanyonya,” alisema Chilongani.

MTANZANIA ilimtafuta katibu huyo wa Amcos ya Mbushi, Mathias Manunda, ambaye alikiri kuombwa kiasi hicho cha fedha ili wasipelekwe mahakani, ambapo walimtumia mtendaji wa kijiji hicho, Salumu Makongo kuwashawishi watoe rushwa hiyo.

“Tulishawishiwa sana na Mtendaji wa Kijiji, lakini mimi nilikataa nikasema ni bora nipelekwe mahakani, nimehangaika kupata hizi Shilingi milioni 15, leo tena wanataka rushwa ya Shilingi milioni mbili nikasema siwezi kutoa.

“Baada ya kukataa niliamua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya na kuelekeza jambo hilo, wao walitaka kwenye zile Shilingi milioni tano, zitolewe Shilingi milioni mbili wasitupeleke Mahakamani na wakulima tuwapelekee Shilingi milioni tatu na baadaye tuhangaike wenyewe kutafuta Shilingi milioni mbili nyingine ili kufidia,” alisema Manunda.

Alipotafutwa OCD kueleza tuhuma hizo hakupatikana, huku Ofisa Ushirika Budodi, akikana kuomba rushwa bali alishirikia zoezi la kupokea Sh milioni tano kutoka kwa viongozi wa Amcos hao kama deni ambalo walikuwa wakidaiwa na wakulima.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza Mtendaji wa Kijiji Salum yeye alikiri kuwashawishi viongozi hao wa Amcos watoe rushwa ya Sh milioni mbili ili wasifikishwe mahakamani baada ya kuagizwa afanye hivyo na OCD pamoja na Ofisa Ushirika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles