26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kubenea ataka mchakato kuondolewa Meya urudiwe

ASHA BANI -DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema),  amejitosa sakata ya kung’olewa kwa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita huku akitaka mchakato huo urudiwe upya ili kuondoa tatizo.

Pamoja na hali hiyo amesema kwa sasa hakutakuwa na kazi yoyote inayofanyika mpaka pale Mwita atakapoendelea na nafasi yake ama laa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kubenea alisema kuwa kwa wale wasiotaka kufanyakazi na Mwita inawalazimu kurudiwa upya kwa mchakato wa kumuondoa kuliko kubaki hali ya utata kama ilivyo sasa.

Kubenea ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, alisema hakutakuwa na kazi yoyote hadi pale Meya Mwita atakapoendelea na wadhifa wake kwani maamuzi ya kuondoa yalikuwa batili na kinyume cha sheria.

“Mchakato wote ulikuwa ni batili na wa kupangwa kwa sababu  akidi ya wajumbe 17 ilikuwa haijatimia ambapo Mkurugenzi Sipora Liana alifanya kughushi kwa kuandika jina la diwani ambaye hakuwepo katika kikao kile na ilitolewa sababu kuwa ni mgonjwa lakini waliendelea na kufanikiwa kumtoa meya kwa uonevu.

“Wajumbe waliofanya maamuzi hayo si halali kwa kuwa kikao kilihudhuriwa na wajumbe 18 ambapo 16 walikuwa CCM na wawili walikuwa upinzani, lakini ili iweze kupata sifa kumuondoa Meya ilitakiwa wajumbe 17 waseme ndio, ila akidi hiyo haikutimia na kufanyika ubabaishaji wa hali ya juu,” alisema Kubenea.

Hata hivyo alisema kwa mujibu wa Meya wa Temeke Abdallah Chaurembo na Sipora kumtuhumu Mwita kwa makosa matano ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mali za ofisi ikiwamo gari, kushindwa kufanya matumizi ya fedha za hisa za UDA, kuingiza mameya kwenye vikao mbalimbali vya kamati ambao wamedai hawakuruhusiwi kwenye kamati ya fedha, kushindwa kuzuia vurugu zilizokuwazinatokea katika mikutano huku akijua kwamba mkurugenzi yeye ndiyo msimamizi.

“Hata hivyo namshangaa Chaurembo anayofanya wakati kwenye kuanzisha fujo yeye amekuwa mstari wa mbele hivyo akae akijua siku nitamweka wazi maovu yake ambayo amekuwa mtu asiye maana katika vikao mbalimbali hasa vya maamuzi ikiwemo kuchochea vurugu ambazo anadai kuwa Mwita anashindwa kusimamia ,’’alisema Kubenea.

Alisema yeye akiwa kwenye Kamati ya Fedha wameshuhudia Sipora akitaka kuingiza mikataba mingi mibovu ya ulaji wa fedha ukiwemo ule wa upanuzi wa Stendi ya Mabasi Ubungo na ndiyo maana amekuwa akipingwa kila akitaka kufanya hivyo na maamuzi yalikuwa ya madiwani wote na si meya pekee.

KAULI YA MKURUGENZI

Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo Mkurugenzi  Sipora alisema kama yeye amefanya hicho wanachomtuhumu ikiwa ni pamoja na ufujaji wa fedha amewataka kwenda katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili achunguzwe.

Pia aliwataka wanaoona kama aliyekuwa Meya wa Jiji,  Isaya Mwita kaonewa wakate rufaa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa (Tamisemi)  na kufuata taratibu zingine hawazuii.

“Simzuii mtu anayenituhumu mimi anatakiwa kwenda Takukuru, kuko wazi na wengine wanaweza kwenda kwa Waziri wa Tamisemi kupinga uamuzi huo na kufuata taratibu zinavyosema,’’alisema Sipora.

UAMUZI WA MAHAKAMA

Wiki ikiyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iligoma kuwazuia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa huo kumuondoa madarakani Meya wa Jiji, Isaya Mwita.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega baada ya kusikiliza hoja za mwombaji na wajibu maombi.

Akisoma uamuzi Hàkimu Mtega alisema kabla ya kufikia uamuzi mahakama imejiuliza maswali kadhaa.

Alisema mahakama imejiuliza ni kweli shauri hilo liikuja Mahakamani Januari 8, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na je, mwombaji alikuwa na wajibu wa kueleza sababu ya kuleta maombi ya kuwazuia wajibu maombi wasimuondoe katika nafasi yake na kuthibitisha hasara ambayo anaweza kuipata endapo mahakama itakataa kutoa uamuzi huo.

“Nimengalia hoja kwa umakini, shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa, lilifunguliwa Januari sita, mahakama ilitoa barua za wito kwa wajibu maombi kufika mahakamani, Januari nane ilikuwa inatajwa.

“Ubadilishanaji wa nyaraka haijakamilika hivyo mahakama isingeweza kusikiliza shauri hilo, ombi la Wakili wa mwombaji, Hekima Mwasipo lilikuwa la msingi kwamba wanahitaji muda wa kujibu kiapo kinzani na kwamba shauri lilikuwa linadaiwa.

“Wakili wa wajibu maombi, Gabriel Malata alijipotosha kwa kusema kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa wakati ubadilishanaji wa nyaraka haijakamilika,”alisema Hakimu Mtega.

Alisema hoja ya pili ni kuthibitisha hasara atakayopata mwombaji iwapo mahakama haitatoa zuio.

Akifafanua alisema kuomba hali ibaki kama ilivyokuwa ni kwamba mwombaji abakie katika nafasi yake kabla haujatokea mfarakano mpaka pale jambo lake litakapotolewa uamuzi.

Wakili Mwasipo alisisitiza kwamba wajibu maombi wanaweza kumuondoa katika nafasi hiyo wakati wowote na kwamba hakuona sababu ya kutoa maelezo wala kueleza hasara kwani anaomba zuio, mteja wake abaki katika nafasi yake mpaka kesi ya msingi itakapomalizika.

“Maoni yangu kwamba, wakili wa mwombaji alikuwa na wajibu wa kuthibitisha uwepo wa kikao cha kumuondoa meya huyo katika nafasi yake, alitakiwa kuleta ushahidi kuonesha jambo hilo lipo ni halisi.

“Lazima uthibitisho uwepo, mahakama haiwezi kutoa amri hiyo bila mwombaji kuleta sababu za msingi za kutaka mwombaji asiondolewe katika nafasi yake.

“Maelekezo ya kutosha lazima yatolewe Mahakamani kuthibitisha kwamba Maombi hayo yana msingi, mahakama inaona wakili ameshindwa kutoa hoja za kusimamia maombi haya, kutokana na sababu hizo maombi ya zuioa yamekataliwa,”  alisema.

Baada ya kutoa uamuzi huo, mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi leo hii Januari 13 mwaka huu ambapo kesi ya msingi ya kupinga kuvuliwa madaraka itakapoanza kusikilizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles