31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

NONDO APATA DHAMANA

Na FRANCIS GODWIN – IRINGA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, imemwachia kwa dhamana mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo, anayetuhumiwa kwa kosa la kudanganya alitekwa.

Aliachiwa mahakamani hapo jana kwa dhamana ya Sh milioni 5 za maneno.

Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, alifikishwa mahakamani hapo jana saa tatu asubuhi, akitokea katika Gereza la Iringa Mjini alikokuwa akishikiliwa.

Hakimu wa Mahakama hiyo, John Mpitanjia, alifikia uamuzi wa kutoa dhamana hiyo baada ya kueleza sababu mbalimbali ikiwamo haki aliyonayo mtuhumiwa.

“Kosa analotuhumiwa mtuhumiwa linadhaminika kwa mujibu wa sheria na hivyo hakuna sababu ya kuzuia dhamana yake.

“Kitendo cha kuendelea kumnyima dhamana mshtakiwa ambaye ni mwanafunzi, kutamfanya akose muda wa kuendelea na masomo yake.

“Kwahiyo, dhamana ya mshtakiwa ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili  wanaotoka ndani ya Mkoa wa Iringa.

“Kati ya wadhamini hao, mmoja awe ni mtumishi wa umma na mwingine awe ni mtu binafsi na wote watasaini dhamana ya maandishi ya shilingi milioni tano,” alisema Hakimu Mpitanjia.

Baada ya uamuzi huo, mahakama hiyo ilitoa muda wa saa tatu kwa upande wa mawakili wa utetezi kukamilisha taratibu za dhamana.

Baada ya taratibu za dhamana kukamilika, hakimu aliruhusu Nondo adhaminiwe hadi Aprili 14, mwaka huu, kesi yake itakapoendelea.

Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, mawakili wa Nondo, Jebra Kambole na Chance Luoga, waliipongeza mahakama hiyo kwa nyakati tofauti kwa kutenda haki dhidi ya mteja wao.

Kwa upande wake, Nondo akizungumza nje ya mahakama hiyo, aliwashukuru Watanzania wote ambao walikuwa wakimwombea pamoja na  vyombo vya habari kwa jinsi vilivyotoa ushirikiano katika kuripoti suala lake.

Pamoja na hayo, alisema hajawahi kusema au kuandika mahali popote kwamba ametekwa.

“Nilipokuwa polisi Dar es Salaam, nilikuwa nikihamishwa mahabusu za polisi zaidi ya mara tatu, lakini kitendo cha mahakama kuruhusu nidhaminiwe, mahakama imetenda haki na hadi sasa siamini kama nimedhaminiwa.

“Hapa Iringa nimeishi vizuri na wenzangu pamoja na askari magereza kwa sababu hawakunifanyia ubaya wowote, ndiyo maana baada ya kudhaminiwa, nilikwenda gerezani kuwaaga  wenzagu.

“Katika hili, naendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu maana ndiye aliyesababisha nipewe dhamana,” alisema Nondo huku akitokwa na machozi.

Wakati Nondo akipata dhamana, hakukuwa na ndugu yake mahakamani hapo zaidi ya wanaharakati wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mjini Iringa.

Wakati huo huo, Nondo alitarajiwa kuondoka jana kurudi Dar es Salaam ambako anatarajia kufanya mtihani chuoni kwake leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles