25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yakabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milini 25 wilayani Same

Na Mwandishi Wetu, Same

Mkuu wa Wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro, Rosemary Senyamule amepokea vifaa mbalimbali vya kusaidia miundombinu ya elimu kutoka Benki ya NMB katika  Shule tano za halmashauri hiyo  vyenye thamani ya Sh milioni 25.

Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kwakoko, Rosemary alisema NMB imekua ikisaidia huduma za jamii ikiwemo kuboresha miundombinu ya elimu nchini ambayo inachangia kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.

Mkuu wa wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro,Rosemary Senyamule(kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Same,Anastazia Tutuba moja ya meza na viti kwaajili ya Shule ya Sekondari Kwakoko vilivyotolewa na benki ya NMB kuunga mkono sekta ya elimu na kurejesha sehemu ya faida kwa wateja, wa pili kulia ni Meneja wa benki hiyo kanda ya Kaskazini, Aikansia Muro.Jumla ya viti 180 na mabati 192 vyenye thamani ya Sh.25 milioni zilikabidhiwa na benki hiyo.

Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wa Shule za Msingi na Sekondari wilayani humo wanakua na mazingira rafiki  ya kujifunzia na kuhimiza uongozi wa Shule zilizopata meza na viti kuvitunza ili vitumike kwa muda mrefu zaidi.

“Serikali inatambua michango ya mara kwa mara ambayo NMB mmekua mkitoa kwa jamii nchi nzima,imekua ikigusa na kusaidia maisha ya wanufaika kwa kiwango kikubwa naamini mtaendelea kuchangia hata maeneo mengine,”alisema Senyamule

Wakati huo huo alitaka benki hiyo kuona umuhimu wa kufungua tawi lingine kwenye ukanda wa milimani hasa vijiji vinavyojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanakua na utamaduni wa kuhifadhi fedha zao benki.

Mkuu wa wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro,Rosemary Senyamule(kushoto) akipokea sehemu ya mabati 192 kutoka kwa Meneja wa benki ya NMB kanda ya Kaskazini,Aikansia Muro(kulia) kwaajili ya Shule ya nne kuunga mkono sekta ya elimu na kurejesha sehemu ya faida kwa wateja wao,katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo,Anastazia Tutuba .Jumla ya viti 180 na mabati 192 vyenye thamani ya Sh 25 milioni zilikabidhiwa na benki hiyo.

Alisema maeneo hayo yana vikundi visivyo rasmi ambavyo wenyeviti wake wamekua na utamaduni wa kutunza fedha ndani ya nyumbani zao badala ya benki na kumekua na malalamiko ya upotevu wa fedha za wana vikundi jambo ambalo halipaswi kuendelea kufumbiwa macho.

Awali Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Aikansia Muro alisema benki hiyo imetoa meza na viti 180  pamoja na mabati 192 kwaajili ya Shule za Sekondari Kwakoko, Bemko, Chauka, Vumari na Shule ya Msingi Mwenge.

“Changamoto za sekta ya elimu kwa NMB ni jambo la kipaumbele, hii ni kutokana na ukweli kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha na kichocheo kikuu cha maendeleo ya wananchi hapa nchini,tunatambua juhudi za serikali za kusimamia elimu kwa nguvu zote kwa kuboresha utoaji wa huduma mijini na vijijini,” alisema Aikansia

Alisema licha ya benki hiyo kupokea maombi mengi ya kuchangia miradi ya jamii imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu za majanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles