25.3 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

NKURUNZIZA AVUTIWA UBORA BIDHAA ZA TANZANIA

Na Mwandishi Wetu

-Bujumbura

RAIS wa Burundi, Pierre Nkurunziza amesifu ubora wa bidhaa zinazotengenezwa  nchini akisema kuwa sasa zitakuwa mkombozi kwa wananchi wa nchi hiyo.

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki alipotembelea maonyesho ya kwanza ya biashara ya Tanzania yaliyofanyika nchini hapa.

Maonyesho hayo  yanalenga kuangalia soko pana la bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali kutoka Tanzania.

Maonyesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Tempete vilivyopo jijini Bujumbura  yalianza Septemba 28, na kuhitimishwa juzi.

Yaliandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuongeza fursa za biashara katika nchi za ukanda   wa Afrika Mashariki na Kati.

“Hii ni ishara ya kukomaa kwa undugu kati ya Tanzania na Burundi, wananchi wa Burundi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata bidhaa hadi Dar es Salaam, lakini sasa wameletewa mlangoni.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukifurahia bidhaa aina hii lakini bei zilikua kubwa kutokana na gharama za usafiri, kwa sasa mambo yamekua mazuri.

“Uhusiano wetu unazidi kuimarika, naamini ile dhana ya utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatekelezwa kwa vitendo. Naahidi kuunga mkono juhudi zote za kuimarika katika uchumi kati ya nchi mbili hizi,” alisema Rais Nkurunziza

Katika maonyesho hayo, ubalozi wa Tanzania nchini Burundi, ukiongozwa na Balozi Rajabu Gamaha  kwa kiasi kikubwa umeshiriki kufanikisha maonyesho hayo.

Gamaha  ndiye aliwisihi maofisa wa TanTrade kuwa na maonyesho aina hiyo kutokana na maombi ya kupata bidhaa kutoka Tanzania kuwa mengi ofisini kwake.

Awali katika hotuba yake ya ufunguzi Septemba 27 mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Bitore alisema biashara ni kitu kinachounganisha mataifa mawili katika uchumi hivyo watatumia  maonyesho hayo kujifunza lakini pia kutanua wigo wa uhusiano wa  uchumi kati ya Tanzania na Burundi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TanTrade, Christopher Chiza alisema uamuzi wa kupeleka bidhaa Burundi ulipofika mezani kwake hakutaka kusita kwa sababu alijua hiyo ni njia pekee ya kufikisha mbali bidhaa za Tanzania.

“Tunapofanikiwa kufika Burundi maana yake tunalenga soko pana la ukanda huu, tunatarajia kufikia soko la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  kwa sababu hata wao tumearifiwa kuwa wananunua bidhaa kutoka Burundi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles