NJIA YA KUONGEZA KIPATO KATIKA BIASHARA

0
658
Kuweka akiba ni muhimu
Kuweka akiba ni muhimu

Na FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM

HAKUNA mtu ambaye hapendi kuongeza kipato katika biashara yake, awe ameajiriwa au amejiajiri mwenyewe.

Na sheria ya kipato ni kwamba inabidi kiongezeke kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda, gharama za maisha zinaongezeka na hata mfumuko wa bei unapunguza thamani ya fedha. Milioni moja ya miaka mitano iliyopita, si sawa na milioni moja ya mwaka huu.

Pamoja na  kujua umuhimu wa kuongeza kipato, lakini bado watu wengi hawajui njia sahihi ya kuongeza kipato katika biashara zao.

Na hii ni kwa sababu hakuna sehemu ambapo somo la kuongeza kipato linafundishwa moja kwa moja. Badala yake tunaangalia wengine wanafanya nini ili kuongeza kipato chao na sisi tunaiga.

Kuna njia nyingi sana ambazo watu wamekuwa wakitumia kuongeza vipato vyao, lakini njia hizi si bora na zimekuwa haziwapatii kile kipato ambacho wanakitaka kweli. Leo kupitia makala hii tutakwenda kujifunza njia bora sana ya kujiongezea kipato chako ambayo kama ukianza kuitumia sasa utakwenda juu zaidi kwenye kipato.
Lakini kabla hatujaangalia ni njia ipi bora, kwanza tuanze kwa kupitia njia zilizozoeleka ambazo hazileti matunda bora.

Kwa waajiriwa, suala la kuongezewa kipato lina changamoto nyingi sana, hii ni kwa sababu si wao wenyewe wanaoamua moja kwa moja ni kiasi gani walipwe, hivyo kuna baadhi ya njia ambazo waajiriwa wamekuwa wakizitumia kutaka kuongeza kipato chao.

Japo njia hizi zimekuwa hazizai matunda, bado wamekuwa wakizing’ang’ania. hizi ni baadhi ya njia za kuongeza  kipato. Hapa waajiriwa huja na madai ya kuongezewa kipato na kuwataka waajiri wao wawaongeze mshahara au cheo ili kuongeza kipato au marupurupu.

Kugoma na kushinikiza ikiwa waajiri hawatakubali mapendekezo, waajiriwa huwa wanagoma na kushinikiza kuongezewa kipato. Kufanya kazi kwa kiwango cha chini, hawa waajiriwa hufikiri kwamba kwa kuwa kipato ni kidogo, basi na wao wafanye kazi ndogo, japo hii ni njia mbovu zaidi kwani ni hujuma.

Kuiba na kupokea  rushwa kwa kuwa kipato hakitoshelezi, basi waajiriwa huamua  kujiongeza wenyewe  ili waweze kukidhi mahitaji yao, hivyo  hujiingiza kwenye vitendo vya wizi, ubadhirifu au rushwa. Njia hii pia ina madhara makubwa zaidi siku za usoni.

Hizi ni baadhi ya njia ambazo waajiriwa wamekuwa wakitumia kutaka kuongeza  kipato chao lakini njia zote hizi si za uhakika na zimepelekea hali kuwa mbaya zaidi  na  ilivyokuwa hapo awali kwani malengo yake ni ya kubomoa.

Vilevile  waliojiajiri  nao wamekuwa wakifanya jitihada za kujiongezea kipato  japokuwa  wamekuwa  wakitumia njia ambazo haziwaletei matunda mazuri, kuna  baadhi ya njia wanazotumia kuongeza vipato vyao kama vile kuongeza bei ya bidhaa au huduma zao ili kupata faida kubwa, hii inaweza kuongeza kipato kwa muda mfupi lakini baadaye inaleta madhara kwa kupunguza ushindani wa hiyo biashara kwenye soko husika.Kwani kuwalipa  kidogo wale wanaowasaidia kwenye shughuli zao, hii pia haina matunda mazuri kwa siku za usoni, kulangua na kutapeli,  kwani kuna baadhi ya watu wanawashawishi watu wanunue bidhaa fulani huku wakijua kabisa haiendi kuwasaidia  na hivyo kuzidi kuharibu biashara zao kwani wateja  hujisika wamedanganywa na hivyo hupoteza imani kwake.

Kufanya kinyume na sheria pamoja na kukwepa kulipa kodi au kupunguza kiasi sahihi kinachotakiwa, njia hii  hufika mwisho pale ambapo wanagundulika na kupelekea biashara kufungiwa au kufa kabisa. Hizi ndizo njia mbalimbali ambazo watu wanapenda kuzitumia kuongeza kipato chao. Lakini cha kusikitisha ni kwamba njia hizi nyingi hazileti kipato cha uhakika ingawa bado watu  wengi wanapenda  kuzitumia.

Tumeshaona njia ambazo si bora na ambazo wengi wanapenda kuzitumia, ni  njia ipi  ambayo hata wewe ukianza kuitumia utapata matokeo bora zaidi  katika kuinua biashara yako?

Njia bora zaidi na ya uhakika ya kuongeza kipato ni wewe kuongeza thamani ya kile unachotoa au unachofanya, ni hivyo tu;  iwe umeajiriwa au umejiajiri au unafanya biashara.

Kadiri unavyoongeza thamani ya kile unachotoa katika soko, ndivyo unavyojihakikishia   kupata kipato kikubwa zaidi.
Kama umeajiriwa, ongeza thamani ya kazi unayofanya weka ubora zaidi,  jitume na uongeze ufanisi wako na uzalishaji wako, usiangalie ni kiasi gani unalipwa  au wengine wanafanya nini jiangalie wewe kwanza. Kumbuka kuwa ukijali kazi utajaliwa.

Unachohitaji kufanya ni kuongeza thamani, weka thamani kubwa ambapo yule anayepokea unachofanya, anaona hiki ni bora. Unapofanya hivi kwa muda mrefu ndivyo unavyojiweka katika  mazingira ya kupata kipato kikubwa zaidi, kwa sababu thamani yako pia itaongezeka na hata kama mwajiri wako wa sasa hatakuongezea kipato, utaziona fursa nyingi za kuongeza kipato. Hata wateja watakujali.

Kwa waliojiajiri na wafanyabiashara, ongeza thamani kwa wateja wako. Kwa bidhaa na huduma unayotoa, hakikisha ina thamani kubwa na inakwenda kumsaidia kweli yule ambaye anainunua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here