27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SERA MPYA YAPAISHA MAUZO MAKAA YA MAWE

Kiwanda cha Dangote kimeanza kutumia makaa ya mawe tanzania
Kiwanda cha Dangote kimeanza kutumia makaa ya mawe tanzania

Na  Joseph Lino,

Kampuni ya uchimbaji makaa ya mawe nchini  ya Tancoal Energy, imefanikiwa kuuza tani 38,877 za makaa ya mawe Desemba mwaka jana, katika mgodi wake wa Ngaka Coalfield uliopo mkoani Ruvuma.

Kampuni ya kutoka Australia ya Intra Energy Corporation ambayo inamiliki asilimia 70 ya hisa za Tancoal, imesema mafanikio hayo yametokana na sera mpya ya Serikali kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje. Zamani viwanda nchini vilikuwa vinaagiza makaa ya mawe nje ya nchi kwa kutumia vigezo mbalimbali vya uongo kuonesha kuwa makaa ya mawe  nchini hayafai.

Ukweli ulipodhihiri na vilevile uthibitishaji wa Dangote Cement kupitia mwenye mali, Aliko Dangote, kuwa makaa ya mawe yanafaa Serikali ilipiga marafuku kuagiza nje na zuio hilo linahusu pia madini ya jasi (gypsum).

Katika taarifa yake iliyotolewa na Intra Energy Corporation, inasema Tancoal ilifanikiwa kufanya vizuri katika mauzo yake Oktoba na Novemba mwaka jana ambapo mauzo ya Novemba mwaka jana ambayo yalifikia tani 35,370 kutoka tani 29,797 ya Oktoba.

Kampuni hiyo imesema wateja wake wameonesha nia ya kuagiza wastani wa tani 60,000 za makaa ya mawe kwa mwezi huu.

Kwa hiyo, Tancoal inaongeza uzalishaji na katika hifadhi yake ili kufikia mahitaji na mauzo.

Hata hivyo, ili kufikia hilo, Tancoal itaongeza vifaa vipya vya uchimbaji vikiwemo 40T excavator, 85T excavator, 55T dump trucks na grader kwa ajili ya utengenezaji wa barabara.

Kabla ya Serikali kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje hasa Afrika Kusini, Tancoal ilikuwa ikipata hasara.

Uzalishaji wa jumla kwa mwaka ulikuwa tani 248,468 na mauzo yalikuwa tani 246,197 kwa wastani wa asilimia 10, ambayo ni kiwango  cha chini.

Mapato ya mauzo ya mwaka jana yalikuwa Dola ya Australia (AUD) milioni 14.408 sawa na Sh bilioni 23.9, hii ilitokana na nchi  kuagiza makaa ya mawe na kuingiza katika soko la ndani ambayo yalikuwa yanaathiri  mauzo na bei.

Takribani tani 150,000 ziliingia nchini kati ya Desemba 2015 na Aprili mwaka jana ambayo ilisababisha kushuka kwa mauzo kutoka tani 137,055 kufikia 109, 142 katika nusu  mwaka badala ya kuongezeka.

Matokeo hayo yalisababisha hasara ya AU$ million 2.1 sawa na Sh milioni 718.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka.

Hata hivyo, mbali na mwenendo wa mafanikio, baada ya Serikali kuzuia makaa ya mawe kutoka nje, Tancoal wametakiwa kujieleza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya ripoti yao ya mahesabu kutoendana na uhalisia.

Hatua hiyo ilimlazimu Waziri mkuu kumwagiza Msajili wa Hazina  kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) katika mapato na matumizi ya kampuni ya Tancoal kama yanaendana na mahesabu yaliyotolewa awali. Serikali ya Tanzania ina asilimia 30 kwenye mgodi huo na hivyo ina haki ya kuingilia mwenenedo wa kampuni hiyo ili kulinda masilahi ya umma.

Waziri Mkuu ang’aka

Waziri Mkuu alitembelea mgodi huo wiki mbili zilizopita alisema: “Mahesabu ya kampuni hiyo yanaonesha kuwa mmepata faida kila mwaka, lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 kampuni ilipanga kuzalisha tani 50,000 na iliuza zaidi ya hapo.

“Desemba mwaka 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa Kampuni ya Saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni za saruji za Tanzania na mliuza. Mbona ‘financial statement’ zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?

“Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha,” alihoji Waziri Mkuu.

MTANZANIA lilimtafuta Emanuel Constantino ambaye ni Meneja Masoko wa Tancoal, ili kupata ufafanuzi  wa tuhuma hizo na namna itakavyoweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani, lakini alipokea simu yake mara moja na kudai kuwa wupo kwenye kikao, lakini alipotafutwa tena hakuweza kupokea simu  kwa siku mbili mfululizo.

Oktoba mwaka jana, kampuni ya kutoka China ya Sino Hydro Corporation waliingia makubaliano ya kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 270 kwa kutumia makaa ya mawe, Ngaka Power Station.

Mitambo ya Ngaka Power Station inatarajia kutumia kiasi cha tani milioni 1.2 kwa mwaka kutoka Tancoal, ambayo ina hifadhi ya tani milioni 423.

Mradi wa Ngaka utakapomalizika utaweza kuchangia asilimia 15 ya umeme katika gridi ya Taifa. Kwa maelezo yaliyopo, Tancoal inaonesha kuwa bonde la Ngaka linakadiriwa kuwa na hifadhi ya tani bilioni moja ya makaa ya mawe.

Aidha, Tancoal huuza makaa ya mawe katika nchi jirani, kama Malawi asilimia 1.5, Kenya asilimia 2.8 na Rwanda asilimia 9.

Inakadiriwa kuwa sekta ya saruji inahitaji tani 500,000 kwa mwaka ambapo Tancoal ina uwezo wa kufikia kiwango hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles