28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Niyonzima, Twite waanza kuchanga karata zao

Mbuyu-TwiteharunaaJENNIFER ULLEMBO NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
WACHEZAJI wa Kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite, wameanza kuchanga karata zao kuelekea katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2014/2015, wakijiwekea malengo ya hatima yao katika soka.
Niyonzima, ambaye mkataba wake umebakiza mwezi mmoja kwisha, amedai kwa klabu yake ya Yanga dau la dola Elfu 50, sawa na Sh milioni 100 za Tanzania, ili kuingia mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo msimu ujao, wakati Twite yeye ametua nchini Kenya kwa mazungumzo na klabu ya Gor Mahia.
Habari za kuaminika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo zililiambia MTANZANIA jana kuwa, Niyonzima anahitaji kiasi hicho cha fedha ili kuendelea kuitumikia Yanga, huku akiwa tayari ameanza mazungumzo na viongozi wa Azam FC.
“Milioni 100 ndizo zitakazombakisha Niyonzima Yanga, lakini tayari ameanza kufanya mazungumzo na uongozi wa Azam, kwani hao ndio wanaoweza kumlipa kiasi hicho cha fedha,” kilisema chanzo hicho.
Kiongozi huyo aliendelea kusema, mchezaji huyo hawezi kwenda Simba, kwani wekundu hao wa Msimbazi hawawezi kumlipa fedha anazohitaji, pia hawatashiriki michuano ya kimataifa kwa kukosa nafasi ya pili.
Gazeti hili lilipomtafuta Niyonzima kupata ukweli juu ya tetesi hizo, alikana kuwa hakuna kitu, licha ya kukubali mkataba wake kufikia tamati mwezi Juni.
“Mkataba wangu unakwisha Juni, viongozi wa Yanga hakuna chochote walichosema wala maongezi waliyoanza kuzungumza na mimi, hadi sasa wapo kimya,” alisema Niyonzima.
Kwa upande wa Twite, ameanza mazungumzo rasmi na uongozi wa timu ya Gor Mahia ili kuitumikia klabu hiyo, baada ya mkataba wake na Wanajangwani kumalizika.
“Amekwenda Kenya, akimaliza atakwenda Sudan kuzungumza na viongozi wa El Merreikh, hivyo timu atakayokubaliana nayo atasaini mkataba,” kilisema chanzo hicho.
Wakati huo huo, Uongozi wa Yanga umeanza kusugua kichwa juu ya kumrudisha mshambuliaji wake wa zamani, Didier Kavumbagu, ambaye anaitumikia klabu ya Azam FC.
“Mikakati ya kumrudisha Kavumbagu imeanza, lakini hapo hapo uongozi unafikiria kusajili mshambuliaji kutoka timu ya BDF XI, ingawa haijafahamika jina lake,” alisema.
Kavumbagu aliichezea Yanga kwa kipindi cha misimu miwili, kabla ya Azam kumsajili baada ya kumaliza mkataba na Wanajangwani hao.
Mnigeria Stand United ataka mil.30
Mshambuliaji Mnigeria, Chidiebere Abasirim, amesema atakuwa tayari kusaini mkataba na klabu yoyote kati ya Simba, Yanga na Azam, endapo watamlipa kitita cha shilingi milioni 30, nyumba ya kuishi, gari na tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi kwao Nigeria.
Chidiebere, aliyeichezea Stand United msimu uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, tayari mkataba wake wa kuichezea klabu hiyo umemalizika, hivyo anasubiri uongozi umalizie kumlipa stahiki zake.
Mchezaji huyo aliyeiwezesha Stand kubaki kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, alisema kama uongozi utakubali kumlipa kiasi hicho hatakuwa na pingamizi la kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Alieleza wakati anajiunga na timu hiyo malengo yake yalikuwa ni kuhakikisha inafanya vizuri na kubaki Ligi Kuu, hivyo sasa anaweza kuwa huru kuondoka mara baada ya ndoto zake kutimia.
Chidiebere aliifungia bao pekee la ushindi Stand katika mchezo wa funga dimba wa michuano ya Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga na kuiwezesha kubaki kwenye ligi hiyo, huku wapinzani wao wakishuka daraja.
“Pamoja na kuwa na ndoto za kutaka kuzichezea timu kubwa hapa Tanzania, lakini pia nilikuwa nikijituma kwa juhudi za dhati kuhakikisha Stand inapata mafanikio ambayo sasa ninaweza kujivunia kwa kutimiza ahadi yangu,” alisema.
Mnigeria huyo, ambaye anatamani kucheza pamoja na mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi ili aweze kutikisa nyavu mara nyingi, alifanikiwa kufunga mabao 11 na kushika nafasi ya tatu kwenye kinyang’anyiro cha ufungaji bora msimu huu.
Winga machachari wa Yanga, Simon Msuva, ndiye aliyempiku Chidiebere na kuibuka mfungaji bora msimu huu, kwa kupachika wavuni mabao 17, akifuatiwa na Amissi Tambwe, aliyefunga mabao 14.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles