25.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Nipo tayari kulipa “kodi ya maendeleo” Tanzania

humor

UZALENDO ni ule uungwana wa kuona kwamba nchi yetu inatuhitaji na kuweka maslahi yake mbele. Watanzania tupo wengi Ughaibuni na kama nilivyoandika kwenye makala zangu za nyuma, Wanaughaibuni wengi hali zao sio mbaya.

Ndio kuna baadhi ambao nao pia wangehitaji misaada mikubwa na baadhi ambao wamefungwa kwa kuvunja sheria pale wanapoishi, hata hivyo wengi wanajitahidi sana kuishi katika mazingira yenye changamoto nyingi, kujielimisha na kufanya kazi kusaidia familia zao Ughaibuni na nyumbani.

Jitihada hizi zinahitaji sana pongezi sio maisha ya starehe, kama wengi wanavyofikiria, upweke mara nyingi ni sehemu ya maisha hayo ingawa tunajitahidi sana kujenga jumuiya zetu na kutuleta karibu tuweze kusaidiana kiurahisi.

Uzalendo wa Watanzania Ughaibuni ni madhubuti sana na uhusiano kati ya nchi yetu na Wanaughaibuni unazidi kuimarisha na kupanuka lakini bado tunahitaji kuweka nguvu zaidi kwenye kujenga miundombinu ambayo italeta uratibu mzuri kuunganisha shughuli zote za Wanadiaspora na kutengeneza taasisi ambayo itawawezesha Wanaughaibuni kuchangia katika maendeleo ya nchi yao kama wapo hapa nchini.

Ni kazi kubwa lakini inawezekana. Balozi tunazo ambazo zinafanya kazi kubwa kweli za kuwahamasisha Watanzania Ughaibuni kujipanga na kujiwezesha kwa njia moja au nyingine katika kujenga jumuiya zao na hata kushiriki kwenye mikutano ambayo inawagusa wao kama Watanzania Ughaibuni na wazalendo.

Hakuna kitu ambacho ni rahisi kuanzisha kukiendeleza na kukiweka hai ambacho kinahusisha watu wengi, changamoto utakuta ni nyingi na kama huna roho ngumu ya kustahimili migongano ya mawazo na mitazamo tofauti basi utajikuta hauna mshikamano mzuri katika mazingira ya kiughaibuni. Shinikizo ni kubwa sana na hapa hauna wazee, shangazi mjomba au baba wa kukushauri na kukupa mwongozo. Hapa uko peke yako katika mazingira mageni.

Katika haya mawazo yote hapo juu ni kuzingatia kwamba bila kujipanga ni vigumu kutoka katika hali hii, wakati wote bila kuelimishana na kufahamu madhumuni na malengo ya mfumo  unaowekwa na bila kulingana na haja itokayo kwenye ngazi za chini basi itakuwa ni kama mbio za sakafuni. Hatufiki mbali.

Ni nguzo gani ambazo tutaweka na kutengeneza hiyo miundombinu na kurahisisha Wanaughaibuni waweze kuchukua nafasi hii kusaidia katika maendeleo ya nchi yetu na kurahisishiwa na kuondoa urasimu ambao ni gharama kwa wanaosimamia kazi hiyo na watumizi wa huduma kutoka miundombinu ambayo itakayoundwa.

Je, kama Wanaughaibuni wakianza kulipa “kodi ya maendeleo” kwa  hiyari kama ishara kwa maoni yangu ni jambo la busara sana. Sio lazima iwe hela nyingi itaweza kuwa ni asilimia ndogo ya mshahara au mapato yako Ughaibuni au kiasi kidogo tu, basi hii itasaidia sana. kwa mfano kila Mtanzania anayeishi Ughaibuni wakijitolea kulipa Sh. 25, 000 kila mwezi kwenye akaunti maalumu ya “kodi ya hiyari ya maendeleo” WanaDiaspora wataweza kulipa.

Kwa kuchangia kodi WanaDiaspora wanaweza; kupata Tin number  na kusajiliwa kama walipa kodi na wakapewa fursa kama Watanzania wengine nchini, kuvuka kutoka nchini na kuingia nchini bila vikwazo, wakatengenezewa vitambulisho maalaumu. Ulipaji kodi utaleta hela za kuendesha hiyo taasisi na hela zinazobaki kusaidia na kuingizwa katika miradi tofauti ya elimu na afya kwa mfano. Kodi hii sio ya lazima ni ya hiyari na wale watakaolipa wapewe kipaumbele.

Mazingira kama haya yatatuwezesha Wanaughaibuni kuona kwamba tunachangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi. Ni kodi ya uzalendo. Kuja kwa hii kodi kutaleta manufaa na kuwa msingi wa ushirikiano kati ya Wanaughaibuni na Serikali. Watu wengi  wanafikiria kwamba kazi kubwa ya Serikali sio kujenga ajira, kumbe hapa Serikali ni kujenga mazingira kwa ajili ya watu kuendeleza kazi zao wenyewe au kujiendeleza. Mazingira mazuri yakiwapo basi ajira zitakuwapo nyingi. Muhimu kuelewa kwamba umaskini si ukosefu wa fedha, lakini ukosefu wa mawazo. Mawazo ya Wanaughaibuni watayokuja nayo na nguvu ambazo watakazokuja nazo zitachangia sana katika mazingira mazuri ya kuleta ajira nyingi.

 

“Kodi ya maendeleo” ambayo pia ni kodi ya hiyari itasaidia sana  kuwapa Wanadiaspora nguvu ya kuwekeza zaidi nyumbani. Nina imani kwamba Serikali ya Awamo ya Tano itaendelea kujenga hayo mazingira wakishirikiana na Watanzania Ughaibuni. Tusiogope kutafuta ushirikiano na maarifa ya kuondoka kwenye hali hii, iwe kutoka kwa Watanzania ndani au nje ya nchi. Mtazamo wetu uwe  wa kutafuta  na ule wa kuanzisha shughuli; si kusubiri  mambo kufanyika.

 

Katika kila jamii kama taasisi sahihi kukosekana  kwa utulivu wa kijamii au usawa katika jamii kwa njia moja au nyingine hurejesha uwiano kiasili. Lakini kwa gharama ya maisha ya watu wengi na pengine uharibifu wa mali. Watu au mifumo ya kisiasa wanaonekana kamwe kujifunza kwa watu kudhulumiwa. Ni kama mpira wa Yanga na Simba.

 

Ni muhimu tuwe na “Kodi Ya hiyari ya maendeleo” 

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga..

 

Tengo Kilumanga Email: [email protected] Tel: +46705263303 Twitter: @tengo_k​

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles