30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi hewa wamezaa ahadi hewa?

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam

MIONGONI  mwa mambo ambayo mzazi au mlezi anaweza kufanya kosa ni pale ambapo atashindwa  kutimiza ahadi kwa  mtoto endapo alimwambia kuwa akifanya jambo fulani mfano kufaulu mtihani  atampatia zawadi.

Hakika mtoto huyo pamoja na kuwa hana uwezo wa kumwadhibu mzazi au mlezi kwa kitendo cha kutotimiziwa,  lakini ni wazi atanung’unika  huku akipoteza imani kwa yule aliyemuahidi.

Ni dhahiri watumishi wa Serikali ni kama watoto wadogo kwa Serikali wanayoitumikia. Watumishi hawa kufananishwa na watoto  ni kwa sababu  hutumia muda wao mwingi kuitumikia nchi.

Rais akiwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi,  anachukuliwa kama mzazi au mlezi wa watu wote anaowaongoza wakiwamo watumishi wa umma ambao kimsingi hutimiza wajibu kwa  Serikali iliyoko madarakani.

Katika muktadha huu wa Rais kuwa mzazi au mlezi hakika kila jambo atakalolisema au kuliahidi huchukuliwa na wananchi kwa namna ya pekee na kwa uzito mkubwa.

Rais John Pombe Magufuli kutokana na historia yake ya  uadilifu na uchapa kazi huku akitimiza kwa vitendo  anayoyatoa kinywani,  kumesababisha wananchi waendelee kumuamini  hata baada ya kuchaguliwa kuiongoza dola.

Ikumbukwe Rais huyu mara baada ya kuingia madarakani aliwaahidi watumishi wa Serikali ya kuwa wakifanya  kazi kwa bidii na kwa  uadilifu  atajitahidi kuboresha maslahi yao.

Msisitizo wa maboresho ya kipato cha watumishi ulidhihirika wazi  wakati wa kusoma Bajeti ya Serikali ya 2016/2017 ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Rais Magufuli na hivyo kuchukuliwa kama dira ya kupima uelekeo wa uongozi mpya.

Ni katika bajeti hiyo palijitokeza mabadiliko makubwa ikiwamo  mfumo mpya wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya dola hususani majeshi kwa kufuta utaratibu wa awali wa motisha kupitia vinywaji  na maduka.

Mfumo huu  wa kufuta motisha katika majeshi  ulikuja kutiwa asali na mwenye nchi ambaye  ndiye Amiri Jeshi Mkuu Jumatatu ya Julai 18, mwaka huu, wakati maafisa mbalimbali  wa polisi wakila kiapo cha uadilifu  Ikulu.

Katika hafla hiyo ya kuwapandisha vyeo maafisa wa polisi,  Rais alisema pesa ambazo zilikuwa zinapitia kwenye mgongo wa motisha zitatolewa kama kifungashio ili kila afisa au askari  ajipangie bajeti yake mwenyewe.

Baada ya hapo zilianza kujitokeza hadithi nyingine ya kwamba Serikali haitapandisha vyeo, kuajiri au kuongeza mishahara kwa muda wa  miezi miwili ili kutoa nafasi ya kuondoa  watumishi hewa.

Ajabu ni kwamba pamoja na kuwa watumishi walivumilia na kuendelea kumuamini Rais,  lakini hata baada ya miezi miwili kumalizika hakuna mabadiliko yoyote yamefanyika zaidi  ya kusikia Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella  Kairuki  akisema nyongeza itatangazwa baadaye kana kwamba suala la watumishi hewa limekuja kama mvua.

Ni ukweli usiopingika  Rais wetu ameonyesha njia kwa kupinga hujuma  na hivyo anastahili pongezi na kutiwa moyo lakini hata hivyo kuna  sababu ya kuchukua tahadhari katika kutoa ahadi. Kwa mambo yasiyo na uhakika ni heri kunyamaza ili yatekelezwe kwa kushtukiza.

Ili kuondoa hali ya sintofahamu ambapo wafanyakazi  wameanza kulia kwamba maisha ni magumu  na kuhisi  Serikali inajitapa kumbe  haina pesa,  huku wengine wakisema  inataka misifa kwa kununua haraka vitu vya bei ghali kama ndege, kuna haja Baba wa kaya kutimiza ahadi zake kama anataka kupambana  na ufisadi, rushwa na uzembe kazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles